Nini? Victoria Paschal Kamata ‘Vicky Kamata’ ni Mbunge wa Viti Maalum
akiwakilisha Mkoa wa Geita kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), katikati
ya wiki iliyopita, aligeuka mbogo na ‘kutoa povu ambalo siyo la nchi
hii’ kufuatia swali aliloulizwa na Wikienda juu ya madai ya kufulia,
kuuza baadhi ya mali zake ikiwemo lile ghorofa lake kisha kutimkia
mkoani Geita kutengeneza makazi mapya.
Habari kutoka kwa chanzo ambacho ni mbunge mmoja ambaye aliwahi kuwa
rafiki wa karibu na Vicky, zilieleza kuwa, kwa sasa mwanasiasa huyo
ameamua kuuza baadhi ya vitu vyake ikiwemo magari na kujikita kwenye
kilimo.
Siku za nyuma, mwandishi wetu aliwahi kuwasiliana na Vicky ambaye
alimjuza kuwa yupo mkoani Morogoro ambako anasimamia kilimo cha mazao ya
tikiti-maji na kumtania mwandishi amtafutie wateja, jambo ambalo
liliishia kwenye vicheko kwani yalikuwa ni mazungumzo ya kawaida.
Kama aya ya kwanza inavyojieleza vyema, baada ya madai ya ‘kulikimbia
jiji’, mwandishi alimtafuta tena Vicky na kumtaka afafanue kwa kina juu
ya manenomaneno hayo ili kuondoa ukakasi kwani nyuma yake kuna wadau na
wapenzi wengi wa kazi zake kama mbunge, msanii na Mkurugenzi wa Taasisi
ya Victoria Foundation.
“Unajua wewe (akilitaja jina la mwandishi), mimi na wewe tunafahamiana,
tena ni mdogo wangu, sasa mimi nataka nikuulize swali dogo sana,
ulipoambiwa maneno hayo, kabla hata ya kunipigia simu na kuniuliza
ulipima na kuona kama yanafanana na mimi kweli unayenijua? “Sikutarajia
kwa kweli ninavyokuamini kama ungethubutu kuniuliza jambo la kama hilo.
“Hivi unatarajia mimi niolewe na kiongozi mkubwa mwenye wadhifa na
maisha yake mazuri (aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk
Servacius Likwelile) halafu nimhamishe aje nimuoe na kuishi naye
nyumbani kwangu?
“Sawa, inaweza kutokea lakini kama sijafanya hivyo? Mambo mengine yanatia hasira sana,” aliwaka Vicky.
Huku akitweta kwa hasira, Vicky aliongeza: “Sikiliza mdogo wangu, kuna
watu wanaomba kila kukicha niishiwe na kufilisika, okey, kwani
wanaoishiwa si ni binadamu kama mimi? Nenda pale Sinza ukaone Victoria
Foundation inavyozidi kufanya kazi.
“Nataka niwaambie hivi, wanaoombea niuze kila kitu, watauza wao na
hatimaye kujiuza na wao na Vicky ataendelea kudunda kwa kumtegemea
Mungu,” alisema Vicky.
Post a Comment