KIONGOZI wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe amesema mwaka
mmoja na nusu wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano umekuwa ni wa
manyanyaso na uonevu kwa baadhi ya viongozi na watendaji wao kuuwawa au
kupotea na Serikali ikiwa kimya.
Mbowe aliyasema hayo katika hotuba ya kambi hiyo bungeni kwa Ofisi ya
Waziri Mkuu, mwishoni mwa wiki ambapo alitolea mfano mauaji na kesi
zinazowakumba wapinzani kila kukicha.
Alisema katika kipindi hicho wameshuhudia mauji ya wanachama, kutekwa,
kukamatwa kwa wabunge na wanachama na kesi mbalimbali ambazo hazina
msingi zikiwa na lengo la kuwakatisha tamaa.
Alitolea mfano kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Geita
Alphonce Mawazo na kusema aliuawa mchana kweupe, huku watu wakishuhudia
na kwamba waliohusika wanajulikana, lakini hakuna hatua ambazo
zilichukuliwa.
“Msaidizi wangu Ben Saanane alipotea baada ya kupokea vitisho kadhaa
vyenye asili ya kisiasa na hadi sasa vyombo vya dola havijatoa maelezo
ya kina ya Ben kapelekwa wapi,” alisema.
Mbowe alisema pamoja na changamoto hizo, Mwenyezi Mungu ameendelea kuwa
upande wao na hila hizo za baadhi ya wenye mamlaka, hazijawaondoa kwenye
lengo kubwa la kuwavusha wananchi wa Tanzania kuifikia ndoto zao.
Alisema wabunge wa upinzani hawajawa salama kwa kile alichodai kuwa
kifungo cha Mbunge wa Kilombero Peter Lijualikali kilikuwa cha uonevu
mkubwa na Mbunge wa Arusha Godbless Lema kunyimwa dhamana kwa zaidi ya
miezi minne kwa shtaka lenye dhamana.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai alisema katika kipindi hicho pia
wameshuhudia Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu akikamatwa mara
kwa mara na vyombo vya dola na kufunguliwa mashtaka mbalimbali yasiyo na
nia njema wala afya kwa ujenzi wa demokrasia katika nchi yetu.
“Tunaamini mapito haya mazito ya kisiasa katika nchi yetu yanalenga
kujaribu kufifisha ndoto ya Taifa ndoto ya kuwa taifa huru
linalosimamia misingi ya haki za binadamu, uhuru wa maoni ya kila raia,
demokrasia ya kweli, kuwa taifa linaloheshimu Katiba ya Nchi na taifa
lenye uchumi unaomnufaisha kila mwananchi,” alisema.
Mbowe alisema tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani,
zimeonekana dalili za wazi za Serikali hiyo kuvunja Katiba ya Nchi kwa
kutupilia mbali misingi ya utawala wa sheria, demokrasia na uhuru wa
kupata habari jambo ambalo linaweza kuitumbukiza nchi yetu kwenye dola
la ki- dikteta.
Alibainisha matukio mahsusi ya ukandamizaji wa haki na demokrasia
yaliyofanywa na serikali kinyume cha Katiba na Sheria za nchi kuwa ni
pamoja na kupiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa.
Serikali kupitia Waziri Mkuu na Rais, ilitangaza kwamba ni marufuku kwa
vyama vya siasa kufanya mikutano ya kisiasa mpaka mwaka 2020 ili kuipa
Serikali nafasi ya kufanya kazi.
”Huu ni uvunjaji wa Ibara ya 20 (1) ya Katiba aidha, katazo la mikutano
ya siasa linakiuka Sheria namba 5 ya Vyama vya Siasa ya 1992 ambayo
imetoa haki kwa vyama vya siasa kufanya kazi ya siasa,” alisema.
Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema kupiga marufuku urushwaji wa moja kwa
moja wa Mijadala ya Bunge ni kinyume na Ibara ya 18 ya Katiba inayotoa
uhuru wa maoni na uhuru wa kupata habari kwa kila mwananchi.
Alisema pia bungeni yamekuwapo matukio kadhaa yanayoashiria kutaka
kuwadhibiti wabunge wa upinzani kwa lengo la kuwanyamazisha wasiikosoe
Serikali.
Kiongozi huyo alisema jambo hilo limefanyika kwa namna mbalimbali,
ikiwamo kuwazushia kesi wabunge wa upinzani na kuwapeleka kwenye Kamati
ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambako hukumu ya kuwaadhibu
inakuwa imeshaandaliwa.
Alibainisha kuwa changamoto nyingine ni Serikali kuingilia muhimili wa
Mahakama, kupuuza utawala wa Sheria, uonevu aliodai kufanywa na vyombo
vya Dola dhidi ya Wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba.
Post a Comment