WAKILI machachari, Tundu Lissu, amechaguliwa kuwa Rais wa Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS) baada ya kupata ushindi wa kishindo katika
uchaguzi uliofanyika mkoani hapa jana.
Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), sasa ataiongoza TLS kwa muda wa mwaka mmoja.
Ushindi wa Lissu unatajwa kuchagizwa na mambo mengi, huku makubwa kati
ya hayo yakitajwa kuwa ni kauli ya Rais Dk. John Magufuli aliyoitoa
Februari 2, mwaka huu akiwa katika maadhimisho ya Siku ya Sheria,
Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, pale aliposema TLS imeshakuwa
kama chama cha siasa baada ya kupata taarifa ya kuwapo kwa mgombea wa
nafasi ya urais ambaye ni mwanasiasa na kutokana na hilo hawezi kuwateua
majaji kutoka ndani ya chama hicho.
Kutokana na kauli hiyo, Lissu aliibuka na kusema hiyo ndiyo ilikuwa
sababu ya msingi iliyomsukuma kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo.
Jambo jingine linalotajwa, ni kauli ya Waziri wa Katiba na Sheria, Dk.
Harrison Mwakyembe, aliyoitoa Februari 15, mwaka huu mjini Dodoma, pale
aliposema kwamba Serikali haiwezi kuona TLS inajiingiza katika siasa na
kama watataka hivyo, hatosita kuifuta Sheria ya TLS sura ya 307
iliyosababisha kuanzishwa kwa chama hicho.
Dk. Mwakyembe alitoa kauli hiyo mjini Dodoma alipozungumza na wanachama
wa TLS wakiongozwa na aliyekuwa Rais wao, John Seka, walipomtembelea
ofisini kwake.
Alisema kitendo cha kuwaingiza wanachama wanasiasa au viongozi wa vyama vya siasa ni kuruhusu mgongano wa masilahi.
Jambo jingine linalotajwa ni kitendo cha Lissu kukamatwa Februari 6,
mwaka huu mjini Dodoma akiwa anahudhuria vikao vya Bunge kwa maagizo ya
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na ilidaiwa alikamatwa ili
achelewe kuchukua na kurudisha fomu za kuwania nafasi hiyo.
Kitendo cha mawakili Godfrey Wasonga na Onesmo Mpinzile ambao ni
wanachama wa TLS, kufungua kesi Dar es Salaam na Dodoma wakipinga
uchaguzi huo, ambazo hata hivyo zilitupwa ni sababu nyingine inayotajwa
kuchangia ushindi wa Lissu.
Si hilo tu, pia jambo jingine linalotajwa kusababisha ushindi wake ni
kitendo cha Lissu kukamatwa Machi 16, mwaka huu nyumbani kwake mjini
Dodoma akiwa anajiandaa kwenda Arusha na kusafirishwa hadi Dar es Salaam
kwa kosa la kutotii sheria na juzi kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu alikosomewa mashitaka matano ikiwamo kutoa maneno ya uchochezi
yenye hisia za kidini.
Lissu alifikishwa mahakamani hapo, ikiwa ni siku moja kabla ya uchaguzi
huo kufanyika jana na kulikuwa na taarifa kwamba pengine asingeweza
kushiriki, lakini baadaye taarifa zilisema taratibu na kanuni za TLS
zinaruhusu mgombea kuchaguliwa hata kama hatokuwapo katika ukumbi wa
kupigia kura.
Baada ya kuachiwa kwa dhamana Lissu alisafiri kwa ndege ya kukodi na
kuwasili Arusha jioni na kwenda moja kwa moja Ukumbi wa Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) ambako alisababisha wajumbe wa
mkutano huo kulipuka kwa shangwe wakimshangilia huku wakimwita ‘jembe’,
hali iliyomlazimu Seka kuwatuliza kwa kuwaambia kitendo hicho
kitawakatisha tamaa wagombea wengine.
MATOKEO YA UCHAGUZI
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo katika Ukumbi wa Simba uliopo AICC,
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Dk. Kibuta Omung’wana, alisema idadi
ya wajumbe waliojisajili walikuwa 3,556 na kati yao waliohudhuria ni
2,560 huku waliopiga kura ni 1,682 – zaidi ya nusu ya wajumbe
waliohudhuria mkutano huo.
Kwa mujibu wa Dk. Omung’wana, nafasi ya urais iligombewa na wajumbe
watano ambao ni Victoria Mandari, Godwin Mwaipongo, Fransis Stolla,
Lawrence Masha na Lissu.
Licha jina la Masha kujitokeza katika karatasi ya wagombea. lakini
wajumbe hawakumpigia kura baada ya kujitoa wakati akiomba kura.
“Naomba nianze kutangaza matokeo nafasi ya rais, Mwapongo amepata kura
23, Mandari amepata kura 176, Stola amepata kura 64 na Lissu amepata
kura 1,411.
“Hivyo namtangaza Lissu kuwa ndiye mshindi katika nafasi ya Rais wa TLS,” alisema Dk. Omung’wana.
Pia alisema mshindi wa nafasi ya Makamu wa Rais ni Godwin Ngwilimi
aliyepata kuwa Mwanasheria Mkuu wa Tanesco kabla kufukuzwa baada ya yeye
mwenyewe kudai kupinga sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow. Alipata kura
1,269 na Wakili Mary Mwasongwe kura 414.
Wajumbe waliochaguliwa ni Lambaji Madai, Jeremia Mtobesi, Aisha Sinda,
Steven Aweso, Husein Mtobwa, Goodluck Walter na Madeline Kimei.
MWELEKEO MPYA TLS
Akizungumza baada ya kuapishwa, Lissu alisema chini ya uongozi wake
itakuwa ni mwisho kwa chombo au mtu yeyote kukitishia chama hicho.
“Ni sisi wenyewe tulioruhusu Serikali ituingilie, iwe ni mwisho. hivyo tuanze mwanzo mpya na turuhusu siku mpya ije.
“Iwe mwisho sasa kwa chama hiki kutishwa na mtu au chombo chochote, iwe
mwisho kwa mawakili kutishwa na kukamatwa ovyo, iwe mwisho kwa mahakimu
na majaji kupokea maelekezo.
“Mimi ni mwanachama wa Chadema ni kiongozi, ni mbunge, ni Mnadhimu Mkuu
wa Kambi ya Upinzai Bungeni, nawahakikishia sitaileta Chadema ndani ya
TLS na sitaipeleka TLS ndani ya Chadema.
“Sijagombea kama mwanachama wa Chadema bali nimegombea kama mwanachama
wa TLS aliye ndani ya Chadema,” alisema Lissu ambaye pia ni Mbunge wa
Singida Mashariki.
Akizungumzia uchaguzi huo, Wakili James Marenga, alisema umefanyika kwa
uhuru, haki, uwazi na kwa kutumia kanuni zote za uchaguzi wa TLS za
mwaka 2016.
Marenga alisema uchaguzi huo umeonyesha ni jinsi gani mawakili wanataka
kuona mabadiliko ndani ya TLS itakayokuwa na uwezo wa kutoa maoni juu ya
utawala wa sheria na masuala ya haki za binadamu.
LOWASSA
Naye Waziri Mkuu wa zamani na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, amempongeza Lissu kwa ushindi mkubwa alioupata.
Lowassa alisema ushindi wa Lissu ni joto la moto mkubwa wa mabadiliko uliotuama ndani ya mioyo ya Watanzania.
“Uchaguzi ule naweza kusema ulikuwa kama kura ya maoni kwa wanasheria
dhidi ya Serikali jinsi inavyoheshimu demokrasia ya umma na utawala wa
sheria,’’ alisema Lowassa.
PROFESA MKUMBO
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitila Mkumbo,
akizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa simu jana, alimpongeza Lissu kwa
kushinda nafasi hiyo na alisisitiza kuwa ushindi wake umechangiwa na
Serikali iliyokuwa ikimfanyia kampeni.
“Ushindi wake ulitarajiwa, ulifanyiwa kampeni na Serikali, tunampongeza
na tunawapongeza wanasheria kwa weledi katika kusimamia taaluma na
kuonyesha wanaweza kufanya uamuzi wao binafsi bila kujali mashinikizo ya
viongozi,” alisema Profesa Mkumbo.
Pia alisema wanasheria wameonyesha utashi wa kitaaluma jambo ambalo ni
la kishujaa na endapo matokeo yangempa ushindi mtu tofauti na Lissu
yangeleta picha mbaya katika jamii.
RIPOTI YA FEDHA
Pia mkutano huo umetishia kuuburuza mahakamani uongozi unaomaliza muda
wake kutokana na kunusa harufu ya ufisadi wa Sh milioni 78 za ada na Sh
milioni 34 zilizokosa viambatanisho katika taarifa ya fedha ya mwaka
2015/2016.
Kutokana na kuibuka kwa mjadala mzito juu ya fedha hizo kwa zaidi ya saa
tatu bila kufikia makubaliano, ndipo waliamua kuunda kamati ya watu
watano itakayoshirikiana na uongozi mpya kuchunguza tuhuma za ufisadi
huo.
Katika mkutano huo uliokuwa ukiongozwa na Seka, uliwasukuma wajumbe
kutoa hoja mbalimbali zilizolenga kujua juu ya fedha zao wanazochanga
kupitia ada za uanachama, baada ya taarifa hiyo kuwasilishwa mbele yao
huku ikiwa imeonyesha makosa ya kiuhasibu.
Wajumbe watano wa kamati itakayoshughulikia kuchunguza tuhuma hizo
ikishirikiana na uongozi mpya inaudwa na Rweikiza Rweikama, Lawrance
Masha, Nicholaus Duhia, Magdalena Sylvester na Ana Julia.
Post a Comment