Katika
hali ambayo haijazoeleka na iliyoonekana kuwa ngeni, Balozi wa Tanzania
Mhe. Philip Marmo alimvisha Cheo Kanali Joseph Bakari aliyepandishwa
Cheo hivi karibuni kutoka Luteni kanali.
Hafla
hiyo fupi iliyohudhuriwa na ujumbe wa Watanzania waliohudhuria
Maonesho ya Kimataifa ya Utalii Jijini Berlin Ujerumani akiwemo Waziri
wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar Mhe. Rashid Ali Juma, Mshauri wa Rais wa Zanzibar mambo ya
Utalii na Utamaduni Mhe. Chimberi Heri, Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya
Utalii Tanzania Mhe. Geofrey Meena, Maafisa wa Ubalozi na wageni
wengine ilifanyika karibuni katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania zilizopo
Berlin nchini Ujerumani.
Akitoa
maelezo mafupi kuhusu tukio hilo Mhe. Balozi alitanabaisha kuwa kwake
ni tukio la kwanza na la la aina yake kupewa dhamana hiyo na kwamba
amepokea maelekezo husika kutoka Makao Makuu ya Jeshi kupitia Wizarani.
Akisoma
sehemu ya maelekezo hayo alisema “ kwa kawaida Afisa anapopanda cheo
akiwa nje ya nchi iwapo hataweza kwenda Tanzania kuvalishwa cheo hicho
na viongozi husika wa JWTZ, cheo hicho kipya huvishwa na Afisa Mkuu au
Balozi wa Tanzania katika Nchi aliyepo”.
Hivyo,
kwa mujibu wa sheria na mamlaka aliyekuwa nayo anatakiwa kumvisha Cheo
kipya cha ukanali mhusika kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi
Tanzania. Kwa mujibu wa maelekezo hayo Kanali Bakari alipandishwa cheo
na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi kuanzia tarehe 31 Januari 2017.
Akitoa
nasaha fupi na salam za pongezi kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi,
wageni waliohudhuria hafla hiyo na Watanzania wote kwa ujumla kwa
Kanali Bakari aliyefuatana na Mkewe Bi Lucy Mlingi, Mhe. Balozi
alimkumbusha Kanali Bakari kuwa ni dhahiri kuwa kupandishwa kwake cheo
kumetokana na imani ya Mkuu wa Majeshi na viongozi wengine wakuu katika
utendaji wake,uadilifu, bidii katika kazi na utii. Hivyo ni vizuri
ahakikishe kuwa anafanya kazi kwa weledi, bidii zaidi na moyo wa
kujituma ili kuleta tija na ufanisi zaidi kwa manufaa ya JWTZ, Tanzania
na Dunia kwa ujumla. Mwisho aliipongeza familia yake hususani Mkewe kwa
mafanikio hayo na kuwatakia heri, Baraka na afya njema.
Kanali
Joseph Bakari ni mwakilishi wa JWTZ katika Sekretarieti ya Baraza la
Michezo ya Majeshi Duniani (International Military Sports Council-CISM)
kama Mshauri na msaidizi wa Mkurugenzi wa Michezo katika Baraza hilo.
Baraza
hilo liliundwa tarehe 18 Februari 1948 mara baada ya vita kuu ya pili
ya dunia. Dhima kuu ikiwa ni kutumia shughuli za michezo na utimamu wa
mwili kama njia ya kueneza amani duniani badala ya vita. Baraza hilo
lina jumla ya nchi wanachama 134 Tanzania ikiwemo. Miongoni mwa
shughuli za Baraza hilo ni kuandaa mashindano ya michezo ya majeshi ya
Dunia.
Balozi wa Tanzania Mhe. Philip Marmo na Acting Colonel Joseph Bakari wakisikiliza maelezo kabla ya hatua ya kumvua cheo cha zamani na kumvika kipya
Balozi wa Tanzania Mhe. Philip Marmo akimvisha cheo kipya Colonel Joseph Bakari
Balozi wa Tanzania Mhe. Philip Marmo akipikea zawadi maalumu ya Sekretarieti ya Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani (International Military Sports Council-CISM) toka kwa Kanali Joseph Bakari wakati wa hafla hiyo
Balozi wa Tanzania Mhe. Philip Marmo akiwa na Kanali Joseph Bakari na mkewe
Balozi wa Tanzania Mhe. Philip Marmo akiwa na Waziri
wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar Mhe. Rashid Ali Juma (kushoto) Mshauri wa Rais wa Zanzibar
mambo ya Utalii na Utamaduni Mhe. Chimberi Heri (wa pili kulia) Colonel Joseph Bakari na mkewe
Tukio hilo la kuvisha Cheo lilihitimishwa na kuimbwa wimbo wa Taifa wa Tanzania.
Picha
ya pamoja na ujumbe wa Watanzania waliohudhuria Maonesho ya Kimataifa
ya Utalii Jijini Berlin Ujerumani akiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni,
Utalii na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Rashid Ali
Juma, Mshauri wa Rais wa Zanzibar mambo ya Utalii na Utamaduni Mhe.
Chimberi Heri, Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania Mhe.
Geofrey Meena, Maafisa wa Ubalozi na wageni wengine ilifanyika karibuni
katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania zilizopo Berlin nchini Ujerumani. Source: Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania Berlin Ujerumani
Post a Comment