Jeshi la Polisi mkoani Tanga linamshikilia mwalimu wa Shule ya Sekondari
Mkwakwani kwa kumpiga na kumsababishia madhara ya kiafya mwanafunzi,
Suleyman Mohamed (18).
Mwanafunzi huyo inadaiwa alichapwa viboko juzi asubuhi na mwalimu huyo
wa zamu aliyekuwa akiwaadhibu wanafunzi waliochelewa na waliokuwa
wakipiga kelele darasani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba amesema tayari
mwalimu huyo yuko mikononi mwa jeshi hilo na upelelezi wa suala hilo
unaendelea.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa amewataka
walimu kuwa waangalifu wakati wakiwaadhibu wanafunzi ili kukwepa madhara
kwa wanafunzi.
“Tunalifuatilia kwa karibu tukio hili. Niseme kwamba tutachukua hatua
stahiki ikithibitika kuwa umefanyika uzembe,” amesema Mwilapwa.
Baada ya kuchwapwa, mwanafunzi huyo amelazwa katika Hospitali ya Rufani
ya Bombo ikielezwa kwamba tayari amepatiwa rufaa kuhamishiwa Hospitali
ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.
Post a Comment