Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
amewasili mjini Mbabane - Swaziland jana16-Mar-2017 kwa ajili ya
kuhudhuria mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC).
Mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Kimataifa wa Mfalme Mswati III
mjini Mbabane – Swaziland, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan
amepokelewa na Viongozi mbalimbali ambao wameongozwa na Waziri wa
Utumishi wa Umma wa Serikali ya Swaziland Owen Nxumalo.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan baada ya kuwasili uwanjani hapo
amekagua gwaride la heshima lililoandaliwa kwa ajili yake na kushuhudia
vikundi mbalimbali vya burudani uwanjani hapo.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan atamuwakilisha Rais wa Jamhuri ya
Muungano Tanzania Dakta JOHN POMBE MAGUFULI ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama inayojulikana kama SADC DOUBLE TROIKA
kwenye mkutano huo.
Leo tarehe 17-Marchi-2017,Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan atahudhuria mkutano wa Wakuu na
Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama unaojulikana kama SADC
Double Troika ambao utajadili kwa kina hali ya ulinzi na usalama katika
nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)na Falme ya Lesotho.
Mkutano huo wa SADC Double Troika utafanyika kwa kuzingatia mapendekezo
ya mkutano wa Mawaziri wa Kamati Ndogo ya Siasa na Diplomasia
uliofanyika Dar es Salaam tarehe 24 februari 2017 ambapo mawaziri hao
walionyesha ipo haja ya kuitisha mkutano huo ili kujadili kwa kina hali
ya ulinzi na usalama kwenye hizo.
Mkutano wa SADC Double Troika utahusisha nchi Sita wanachama wa asasi
hiyo ambazo ni Tanzania,Swaziland,Afrika Kusini,Angola,Botswana na
Msumbiji.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan katika msafara wake amefuatana na
Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Kikanda na
Kimataifa Dakta Augustine Mahiga,Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji
Charles Mwijage na Waziri wa Biashara,Viwanda na Masoko wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Amina Salum Ali.
Post a Comment