BAADHI YA WAKULIMA WALIOPO VCHINI YA MRADI WA AFRICA RISING |
Na Ferdinand Shayo,Morogoro.
Asilimia 20
mpaka 40 ya mazao yanayovunwa na wakulima hasa mahindi hupotea kuanzia kipindi
cha uvunaji mpaka kuhifadhi. kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo mbinu
hafifu za uhifadhi wa mazao hayo.
Mazao ya Wakulima huanza kupotea yakiwa
shambani kipindi cha uvunaji,usafirishaji ,kuanika na kuhifadhi.
Wakulima wengi wamekuwa wakitumia mbinu duni za
kuhifadhi mazao yao na kujikuta wakipoteza kiasi kikubwa.
Wengine wamekuwa wakitumia madawa makali ya
viwandani kwa kuhifadhia na yenye
kemikali ambayo hubaki kwenye mazao na kusababisha madhara kwenye mwili wa
binadamu ikiwemo magonjwa ya saratani.
Kutokana na changamoto
hiyo mradi wa Africa RISING unaosimamiwa
na Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA) kwa kushirikiana na
wadau mbali mbali unatoa elimu kwa wakulima kuhusu kuzuia upotevu wa mazao hasa
mahindi, jamii ya mikunde na karanga.
Pia unafanyauhimizaji
wa matumizi ya mifuko ya kinga njaa maarufu
kama “mifuko ya PICS” kwa kushirikiana na wasambazaji wa teknolojia hiyo rafiki kwa wakulima ambayo
haihusishi matumizi ya kemikali za kuhifadhia mazao.
Mkulima hutakiwa kuhifadhi mahindi yake katika
mfuko maalumu ambao haupitishi hewa na hauruhusu mdudu wa aina yoyote kupenya
katika mfuko huo.
Wakulima wa Kilosa kutoka kikundi cha Kwimage
kilichopo Kijiji cha Maguha wameeleza
kunufaika na teknolojia hiyo ambapo awali kabla ya kutumia teknolojia hiyo
walikuwa wakipoteza kiasi kikubwa cha mazao yao.
Andrew Chahunga ni Mkulima Anasema kuwa baada ya kupatia elimu juu ya
kutumia mifuko hiyo wakulima waliamua kuhifadhi mahindi yao kama kikundi na
baada ya miezi 6 waliyakuta mahindi yao yakiwa katika hali nzuri tofauti na
yale yanayohifadhiwa kwa kutumia madawa ya viwandani.
“Kwa kweli tumetumia njia hii ya kuhifadhi
mazao na imekuwa msaada mkubwa sana kwetu. Mahindi tuliyoyahifadhi ni salama
kwa chakula kwenye familia zetu na hata kwenda masokoni kwa ajili ya
kuuza” Alisema
Anaeleza kuwa
uhifadhi huo umesaidia kuepukana na njaa katika kaya nyingi ambazo ni masikini
na ambazo hutegemea kilimo kama njia ya kujipatia chakula pamoja na kipato.
Alex Mbigo, Mwenyekiti wa Kikundi cha Kwimage
anasema kabla ya kutumia teknolijia hii mahindi yao yalikua yakiharibiwa vibaya
na wadudu (kubunguliwa). Katika gunia
moja lenye debe saba 7 huambulia debe tano 5 pekee huku madebe mawili
yakiliwa na wadudu alieleza.
“Mradi wa Africa RISING kutoa mifuko ya
kuhifadhia chakula umetufariji sana hivi sasa tunao uwezo wa kutumia mahindi
hata kwa kusaga dona “
Fanuel Sinyagwa anaeleza kuwa teknolijia hiyo
bado ilikua haijafika kijijini hapo ,mifuko hiyo inafanana na magunia yao ya
asili kwa ujazo hivyo imekua rahisi kutumia teknolojia hiyo.
Licha ya Kutumia mifuko hiyo Changamoto
tunayokutana nayo ni ukosefu wa maghala ya kuhifadhia chakula kwani upotevu
mkubwa wa mahindi hutokea majumbani zaidi .
“Teknolojia hii ni rahisi haitumii gharama
kubwa ,gharama yake ni mfuko na mfuko unaweza kuutumia kwa muda wa miaka mitatu
na mahindi yako yakabaki salama” Alisema
Hellen Lezi ni Mwanakikundi wa Kwimage
anaeleza kuwa mifuko hiyo inasaidia kuhifadhi chakula na kuepukana na njaa
katika kaya .
Mtafiti Msaidizi wa Mradi wa Africa RISING
Audifas Gaspar anasema kuwa licha ya juhudi zinazofanywa na serikali pamoja na
mashirika binafsi bado mkulima anapoteza hadi asilimia 40% ya mazao yake tangu
yanapokuwa shambani mpaka yanapovunwa ,wakati wakipakia
kwenye vyombo vya usafiri ,upukuchuaji, kuanika na kuhifadhi.
Mifuko ya kinga njaa ni mkombozi wa Mkulima
ambapo inaweza kupunguza upotevu sambamba na teknolojia nyingine za upukuchuaji
na uanikaji kutoka asilimia 40 mpaka chini ya asilimia 3.
Utumiaji wa madawa katika uhifadhi una
changamoto nyingi ikiwemo dawa feki zilizopo sokoni na matumizi mabaya ya dawa
hizo zinazoweza kuwa sumu kwa binadamu na kuleta athari.
“Sisi kama Wataalamu tunashirikiana na
Wakulima juu ya namna bora ya kuhifadhi mazao yasiharibike,tunatoa elimu kwa
njia ya vikundi vya wakulima” Alisema Audifas.
Post a Comment