SERKALI ipo katika mazungumzo na Benki ya Dunia kwa ajili ya kusaidia
miradi ya maendeleo inayoandaliwa kwa mwaka ujao wa fedha itakayogharimu
dola milioni 785 ambayo ni sawa na Sh trilioni 1.747.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ameyasema hayo jana jijini
Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya
kuzungumza na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya
Afrika, Makhtar Diop.
Dk Mpango alisema kwa upande wa kuboresha Bandari ya Dar es Salaam,
mradi mzima ulikadiriwa utahitaji dola milioni 600, lakini kwa awamu ya
kwanza ambayo Benki ya Dunia wamekubaliana watakwenda kuharakisha
mchakato na kutoa dola milioni 305 ili kazi ianze mapema.
Alisema ipo miradi mingine ambayo ni ya kisera ambayo ni kwa ajili ya
kuboresha mazingira ya kufanya biashara ambayo ina thamani ya dola
milioni 80 na kuna miradi mingine ambayo baada ya kumaliza majadiliano
itatekelezwa.
Akitolea mfano, alisema kuna mradi wa elimu ambao utagharimu dola
milioni 100, mradi wa kusaidia kuimarisha menejimenti ya bajeti na uwazi
katika masuala ya bajeti ambao ni dola milioni 80, mradi wa awamu ya
pili ya maji ambao ni dola milioni 100.
Dk Mpango alisema miradi hiyo inatekelezwa kwa awamu na mingine ipo
kwenye maandalizi ambapo kwa upande wa makutano ya barabara uya Ubungo
alisema kuwa bado hawana makubaliano ila haitapungua dola milioni 60.
Pia alisema wamelenga kuboresha sera na kufanya kuwa sehemu nzuri ya
kufanyia biashara, na wamekubaliana kuongeza uwezo katika miradi ya ubia
kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) na kusaidia kuongeza
uwezekano wa kupata wabia.
Post a Comment