Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu itatoa uamuzi wa malalamiko ya washtakiwa wa
mauaji ya dada wa bilionea Erasto Msuya, mnamo Septemba 27.
Mahakama ilipanga kutoa uamuzi huo jana baada ya kusikia majibu ya hoja za upande wa mashtaka.
Washtakiwa
katika kesi hiyo, Miriam Stephen Mrita (41) na mfanyabiashara Revocatus
Evarist Muyela (40) wanadaiwa kumuua kwa makusudi Anathe Msuya, kwa
kumchinja, nyumbani kwake, Kibada Kigamboni Mei 25, 2016.
Miriam
ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo alikuwa mke bilionea
Msuya. Bilionea Msuya aliuawa kwa risasi Agosti, 2015 eneo la
Mijohoroni, kando ya Barabara ya Arusha – Moshi wilayani Hai mkoani
Kilimanjaro.
Washtakiwa
hao kupitia kwa Wakili wao Peter Kibatala wamedai kuwa walikubali kosa
hilo baada ya kuteswa na polisi na kulazimishwa kukubali.
Mbele
ya Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Magreth Bankika, Wakili Kibatala
amedai kuwa washtakiwa hao wana vielelezo vya mateso waliyoyapata
ikiwamo kuvimba miguu na majeraha ya mwili.
Kutokana
madai hayo, ameiomba Mahakama iamuru uongozi wa Magereza kuwafanyia
uchunguzi wa afya na matokeo ya uchunguzi huo yawasilishwe mahakamani na
kuwekwa katika kumbukumbu.
Hata
hivyo, upande wa mashtaka umepinga madai hayo na Wakili wa Serikali,
Diana Lukondo ameieleza Mahakama kuwa shtaka linajitosheleza kiasi
kwamba washtakiwa wanaelewa kile wanachoshtakiwa.
Wakili
Lukondo amedai kuwa si kweli kwamba waliteswa na kama ingekuwa hivyo,
wangefuata taratibu na kwamba uongozi wa Magereza hauwezi kumtibu mtu
ambaye hana Fomu namba tatu ya Polisi (PF3).
Post a Comment