NA: SIMON MJEMA, Same.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,George Jackson Mbijimi,amewataka
vijana na Wananchi nchini kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya kwa kuwa
yamekuwa na athari kubwa katika maendeleo ya Taifa kwa kuharibu nguvu kazi ya
Taifa pamoja na kusababisha maambukizi mapya ya ukimwi.
Akizungumza na Wananchi wa Wilaya ya Same katika Kata ya
Hedaru, eneo la mkesha wa mbio za
mwenge,alisema Wananchi wa Wilaya ya Same wamejijengea sifa mbaya ndani na nje
ya nchi kwa kilimo cha madawa ya kulevya aina ya mirungi,na kuwataka vijana na
wananchi hao,kuachana na kilimo hicho
pamoja na matumizi ya mirungi kwa kuwa yanaathiri afya zao.
Mbijima amesema,maendeleo ya uchumi wa kati,ambayo Taifa linataka kuyafikia mwaka
2025,hayataweza kufikiwa endapo changamoto ambazo kwa muda mrefu zimekuwa
zikilikabili Taifa la Tanzania zitaendelea kupewa nafasi ya kutawala katika
Jamii;Ambapo miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na Matumizi ya madawa ya
kulevya na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,Said Meck Sadick,akiwasalimu
wananchi katika eneo la mkesha wa Mwenge,amewaambia wananchi wa Same waache kilimo cha mirungi kwa kuwa kinaharibu
Afya,akili na kudhoofisha nguvu kazi,huku akiagiza viongozi wote wilayani Same kuwahimiza wananchi kutunza na kununua
chakula kabla bei hazijapanda ili kuepukana na njaa.
Akisoma risala ya Utii ya Wananchi wa Same,Mkuu wa Wilaya ya
Same,Rosemary Stak Senyamule, amesema wameendelea kupambana na matumizi ya
madawa ya kulevya kwa kuchukua hatua mbalimbali,ikiwemo kufyeka na kung`oa
mimea ya mirungi,kwa kufanya misako endelevu ya wakulima,wauzaji na watumiaji
wa mirungi,ambapo jumla ya ekari kumi za mirungiziliteketezwa.
Mwenge wa Uhuru umezindua jumla ya miradi saba ya
kimaendeleo wilayani same Mkoani Kilimanjaro jumamosi iliyopita na kuweka jiwe
la msingi,ikiwemo kituo cha kulelea watoto yatima kilichopo kata ya Mabilioni
kabla Mwenge wa uhuru kukabidhiwa Mkoani Manyara.Kauli mbiu ya mwenge mwaka huu
ni VIJANA NI NGUVU KAZI YA TAIFA,WASHIRIKISHWE NA KUWEZESHWA.
Post a Comment