Kanda ya Pwani ya chama hicho inajumuisha mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Bendera hizo ni kwa ajili ya kuweka kwenye ofisi, kwenye nyumba na maeneo ya biashara na kupeperusha kwenye magari.
Katibu wa Kanda ya Pwani, Casimir Mabina amewaambia waandishi wa habari kwamba wanafanya hivyo kama ishara ya kuunga mkono tamko la Kamati Kuu ya Chadema ya kufanya maandamano ya amani na mikutano nchi nzima.
“Chadema Kanda ya Pwani tunaunga mkono kauli na tamko la Kamati Kuu ya Chadema la kupinga kwa nguvu zote, msimamo wa utawala huu wa awamu ya tano wa kukandamiza demokrasia. Sisi Kanda ya Pwani tutashiriki kikamilifu katika operesheni hiyo,” amesema Mabina.
Amewataka wafuasi wa chama hicho kanda hiyo kutundika kila eneo bendera watakazopewa katika kile alichokiita amshaamsha kuelekea Septemba Mosi.
“Mwenye gari aweke bendera, mwenye ofisi, mwenye duka, kila kona tandazeni bendera za chama kama ishara ya kuunga mkono uamuzi wa chama chetu wa kupinga uminywaji wa demokrasia unaofanywa na serikali ya awamu ya tano,” alisema.
Hata hivyo, Rais John Magufuli ameonya mara kadhaa kwamba asijaribiwe, mikutano ya siasa hadi mwaka 2020. Mikutano pekee aliyoruhusu ni ya ndani na wabunge katika majimbo yao lakini si ya wanasiasa.
Chadema inasema tamko hilo la Rais Magufuli ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992, na Kanuni za maadili ya vyama vya siasa za mwaka 2007, kwani zinaruhusu mikutano na maandamano kwa ajili ya kutafuta wanachama na kunadi sera mradi watoe taarifa polisi kwa ajili ya ulinzi. Katika siku za hivi karibuni, mikutano kadhaa ya Chadema imesambaratishwa na Jeshi la Polisi.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Mabina amesema anashangaa wakati Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM anakataza wapinzani kuandamana, wafuasi na wanachama wake wameonekana wakifanya maandamano kutoka uwanja wa ndege kuelekea yalipo makao makuu ya chama chao.
“Nasema haya kutokana na taarifa iliyotolewa na Ole Sendeka kuwa Rais alikuwa akifanya ziara ya chama ambayo ilianzia Dodoma makao makuu ya CCM baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa wa mwenyekiti wa Taifa… leo (jana) amemalizia mtaa wa Lumumba zilipo ofisi ndogo za chama,” alisema
Kwa mazingira hayo, Mabina alisema Chadema Kanda ya Pwani inaunga mkono operesheni hiyo iliyopewa jina la Ukuta na kuwa watahakikisha inafanyika kama ilivyokusudiwa na kwamba kwa umoja wao watasimama imara.
“Kutokana na Serikali ya awamu ya tano kuonekana kukandamiza demokrasia nchini, sisi Chadema Kanda ya Pwani tumeazimia kushiriki kwa nguvu zote kwenye operesheni Ukuta” alisema.
Aliongeza kuwa nia yao ni kuungana na wenzao nchi nzima kupinga ukandamizaji wa demokrasia na uhuru wa vyama vya upinzani kufanya siasa kama Katiba na sheria za nchi zinavyoruhusu.
Post a Comment