Kambi ya aliyekuwa Mgombea Urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
kwa tiketi ya Chadema, Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowasa imemfungukia
muigizaji wa Bongo Movie, Jacqueline Wolper, siku chache tu baada ya
kutangaza kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma.
Wakizungumza na Risasi Mchanganyiko kwa nyakati tofauti juzi jijini Dar
es Salaam, wasemaji wa kambi hiyo walisema alichokifanya Wolper ni
utashi wake wa kisiasa, unatokana na hisia zake, ingawa pia walimsema
kama mtu asiyefahamu misingi, sera, itikadi, imani wa ilani za Chadema.
Msemaji binafsi wa Lowasa, Aboubakary Liongo, aliliambia gazeti hili
kuwa ni vigumu kwa kiongozi huyo kumzungumzia Wolper kwa sababu
hakukuwahi kuwa na ‘connection’ ya moja kwa moja baina yao, isipokuwa
msanii huyo alijiunga na wanamabadiliko kwa utashi wake mwenyewe.
“Mzee hawezi kumzungumzia, alikuja huku kama ambavyo vijana wengine
wengi walikuja wakifuata mabadiliko, kama kuna wa kumzungumzia, labda ni
viongozi wa chama kwa sababu operesheni zote zilizokuwa zikifanywa
wakati ule, ziliratibiwa na chama.
“Wao ndiyo wanaweza kuwa na la kusema kuhusu yeye, ila ninachokiona mimi
ni kuwa Wolper ni mtu mzima, mwenye akili timamu, alikuja kwa utashi
wake na kama anaondoka, pia anafanya hivyo kwa utashi wake,” alisema
Liongo, ambaye ni mtangazaji mwandamizi wa redio nchini.
Kwa upande wake, msemaji wa Chadema, Tumaini Makene, alisema Wolper ni
mtu asiye na msimamo, asiyeelewa misingi, ilani, sera wala itikadi za
Chadema, ndiyo maana haelewi nini anafanya.
“Sisi tuko na watu wanaoishi kwa matendo, siasa ni maisha ya binadamu,
mtu ‘siriaz’ anajua misingi, itikadi, falsafa, imani na ilani za chama
chake, hawezi kuwa leo anaamini hivi kesho vile, ukiona mtu kama huyo,
ujue hana msimamo, anayumbishwa na ni mtu anayefuata mkumbo,” alisema
Makene.
Lowassa 2Aliyekuwa Mgombea Urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
kwa tiketi ya Chadema, Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowasa
Msemaji huyo alitolea mfano wa vyama viwili vikubwa vya siasa nchini
Marekani, Republican na Democrat, akidai waumini wa taasisi hizo mbili
za kisiasa, ni watu wenye weledi wanaojua nini wanafuata, hivyo siyo
rahisi kuona mtu akihama ovyo kutoka upande mmoja kwenda mwingine.
Wolper ambaye aliwahi kuwasuta waigizaji wenzake walioamua kujiunga na
CCM kwenye kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, akisema ni watu
wasioitakia mema taifa kwa kushindwa kuungana ili kulikomboa, hivi
karibuni alitangaza kurejea chama tawala, akisema anarudi nyumbani kwani
alipotea njia.
“Nimerudi na sifikiri tena kugeuka nyuma, nimeona jinsi rais wetu
anavyopigana na chama hiki kuwakomboa wanyonge na sasa hivi kina kasi ya
ajabu na nitaendeleza niliyoyaacha,” alisema msanii huyo wakati wa
hafla ya kumuaga Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete mjini Dodoma.
About Author
Journalist , Enterpreneur, Lecturer and Blogger. Email :ngoboleaa@gmail.com.
Advertisement
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment