Akizungumza baada ya Waziri wa Fedha na Mipango kuwasilisha mapendekezo ya ukomo wa bajeti hiyo pamoja na mpango wa maendeleo kwa mwaka huo, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ambaye pia ni Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema), alisema mambo mema yamefanywa.
Alisema mambo matatu makubwa yakitekelezwa, itakuwa imetibu kiu ya watanzania ya muda mrefu, moja ni kupeleka fedha nyingi kwa maendeleo na kubana matumizi ya kawaida na pili imepunguza utegemezi wa wafadhili, kufadhili bajeti ya nchi. Alisema hilo ni jambo jema na kusisitiza kuwa msingi iwekwe ya kuimarisha.
“Ukomo wa bajeti ni kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, hili nalo katika serikali ya awamu ya tano wameliona na kweli tuwaunge mkono, sio kila kitu tuone kibaya, cha msingi tuwape nafasi tuone watamalizaje huko mbele kwenye utekelezaji”, aliongeza Mbowe.
Kwa upande wa Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT-Wazalendo) alisema serikali imethubutu kupanga kiwango kikubwa cha bajeti na ni vyema kuwatia moyo na kuacha tabia ya kukosoa jambo kwa hatua ya awali.
Alisema kitendo cha kuweka asilimia 40 kwenye bajeti ya maendeleo ni hatua kubwa na kwamba mpango wa serikali kurasimisha sekta isiyo rasmi, wakiwemo wafanyabiashara ndogo na wengine ambao hawakuwa wakilipa kodi, utasaidia kuongeza mapato ya kodi.
“Ni hatua kubwa sana, cha msingi ni kuhakikisha bajeti ya maendeleo ambayo imetengewa asilimia 40 ya mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2016/17 inatekelezwa, ni vyema tuwatie moyo”, alisema Zitto .
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (CCM), alisema mapendekezo hayo yametoa mwanga na unafuu kwa watanzania kwa kuwa kupitia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17, ambao umegusa maeneo mengi nyeti yanayowagusa wananchi.
“Ni bajeti nzuri, kwa kweli imezingatia zaidi matakwa ya wananchi hasa katika eneo la matumizi ya maendeleo. Si kwamba bajeti za nyuma zilikuwa mbaya. La hasha. Lakini kutokana na utegemezi mkubwa wa fedha za nje, zilionekana kuwa hazitekelezeki,” alisema Ngeleja.
Kwa upande wa Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda (CCM) alisema mapendekezo hayo, yametoa matumaini na mwanga mpya kwa watanzania, kwani kwa mara ya kwanza Serikali inaonyesha nia ya dhati ya kuachana na utegemezi.
“Bajeti imeweka wazi utegemezi wa wahisani uko asilimia 12 tu ya bajeti yote, miradi mingi ilikuwa haitekelezeki au kumaliza kutokana na wahisani wengi kutotimiza ahadi zao, lakini sasa Serikali imeamua kujikita katika ukusanyaji wa mapato yake na kutegemea zaidi fedha za ndani,” alisisitiza Mapunda.
Mbunge huyo alipongeza hatua za Serikali ya awamu ya tano za kuhakikisha matumizi yote ya fedha za Serikali yanafuatiliwa, ikiwa ni pamoja na kuweka mfumo wa kuhakiki matumizi na mapato yake kila mwezi ili kuona kama yanawiana.
Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM) alisema kwa sasa yapo matumaini ya miradi ya maendeleo kukamilika kutokana na bajeti nzima kujikita katika fedha za ndani, kwani kiasi kinachotarajiwa kutoka kwa wahisani, hata kisipotolewa, upo uwezekano wa fedha hizo kupatikana kupitia mapato ya ndani.
“Hata hao wahisani mara nyingi wamekuwa wakitoa ahadi, lakini utekelezaji wao unaambatana na masharti mengine ambayo hayana hata msingi. Na upatikanaji wa hela yao umekuwa mgumu. Sio hata hizi Shilingi trilioni tatu hata wasipoleta tuna uwezo wa kuzikusanya kutoka humu ndani,” alisema.
Aliongeza kuwa, “Mimi naunga mkono jitihada za serikali ambazo zimefanya na kutuondoa katika utegemezi wa misaada sana. Mimi naamini kuwa nchi yetu ni tajiri ina vitu vingi sana, ambavyo vinaweza kutufikisha mahala tukajitegemea”.
Kwa upande wake, mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisema mapendekezo ya bajeti hiyo, hayana uhalisia na huenda yasitekelezeke, kwa kuwa yameegemea zaidi katika mafanikio ya muda mfupi yaliyopatikana katika ukusanyaji wa kodi na faini za wakwepa kodi.
Kuhusu ushauri wake wa namna ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kukwamisha utekelezaji wa mapendekezo ya bajeti hiyo, mbunge huyo alisema “waulizeni CCM, hiyo si kazi yangu”.
Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF) alisema baada ya kumaliza habari ya faini za kodi na wale waliokwepa kulipa kodi, makusanyo yatashuka kwa kiasi kikubwa. Alishauri kuibuliwa kwa maeneo mengi, yaliyotekelezwa yanayoweza kulipishwa kodi, ikiwemo eneo la bahari ambalo kwa mujibu wake kwa sasa limegeuzwa kama shamba la bibi.
Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly (CCM), alisema mpango na mapendekezo ya bajeti ni mzuri, kwa kuwa vitu vingi vimelenga mahitaji ya wananchi na sasa kiu ni kuona utekelezaji wake.
Post a Comment