Makubaliano hayo baina ya Acacia na TRA ni kilele cha mchakato uliofanywa kwa lengo la kuendeleza dhamira ya utendaji ya kampuni hiyo nchini Tanzania na kuongeza ushirikiano na wadau mbalimbali wa kampuni hiyo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Bradley Gordon, alitoa taarifa hiyo kwenye mawasiliano na wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Alisema kutokana na makadirio, kampuni hiyo italipa kodi ya ushirika ya miaka mitatu, endapo kampuni hiyo mwaka huu itaingiza mapato yanayofikia kiasi cha dola za Marekani milioni 80.
Alisema mkataba kati ya Acacia na TRA umetiwa saini na umetambuliwa na pande zote mbili kwamba hakuna kodi yoyote ya mapato yatokanayo na faida ambayo Acacia inastahili kulipa, haitalipwa.
Gordon alisema Acacia Mining ambayo iliingia nchini katika sekta ya madini ikijulikana kama Barrick na baadaye kama African Barrick Gold miaka 15 iliyopita, imekuwa ikitengeneza faida lakini haijarejesha mtaji iliowekeza wa dola za Kimarekani bilioni 3.8.
Hivi karibuni, Baraza la Rufaa za Kodi (TRAT), liliamua katika rufaa iliyokatwa na Acacia kwamba kampuni hiyo ilijenga mazingira ya kukwepa kodi ya dola za Marekani 41,250,426 (Sh bilioni 89) kwa kipindi cha miaka minne mfululizo.
Katika hukumu hiyo iliyotolewa na Mwenyekiti wa TRAT, Jaji Dk Fauz Twaib, ilielezwa kuwa fedha hizo zilizopaswa kulipwa na ABG kwa TRA kama kodi ya zuio katika kipindi hicho, lakini ikakata rufaa kupinga kodi hiyo na baraza hilo kuipa haki TRA.
Hata hivyo, Acacia imepinga uamuzi huo katika Mahakama ya Rufaa. Akizungumzia historia ya mgodi huo, Gordon alisema wakati Barrick ilipoingia Tanzania miaka zaidi ya 15 iliyopita, kulikuwa na shughuli za kiwango kidogo za migodi nchini.
Gordon alisema tangu wakati huo, Barrick, African Barrick Gold na kisha Acacia Mining zimewekeza kiasi cha dola bilioni 3.8 katika ujenzi na uendelezaji wa migodi mitatu iliyopo hadi sasa.
Alisema Tanzania sasa ni mzalishaji mkuu wa nne wa dhahabu duniani, na kwamba kampuni yao ndiyo wazalishaji wakubwa nchini jambo alilosema hawana budi kujivunia.
Akizungumza madai kwamba wanatoa taarifa za uongo za kupata hasara ili kukwepa kulipa kodi nchini , alisema akaunti zao pamoja na zile za migodi mingine duniani hufanyiwa uhakiki makini.
“Kwa Tanzania peke yake, kuna mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Shirika la Uhakiki wa Migodi, Mahakama ya Udhibiti na Mamlaka ya Mapato Tanzania –taasisi zote hizi zinapembua hesabu zetu.
"Kwa kuwa tuna Soko la Hisa la London lenye umahiri mkubwa nalo pia linafanya kazi makini kuhakiki shughuli zetu,” alisema.
Alisisitiza kuwa hawajakwepa kulipa kodi bali katika biashara, panahitajika kwanza kuondoa gharama zote katika mapato kabla ya kutangaza kwamba wamepata faida.
Alisema katika miaka sita iliyopita pekee, tumelipa zaidi ya dola za Kimarekani milioni 750 kama kodi na mrabaha nchini Tanzania, karibu mara mbili ya kiasi ambacho wanahisa wamepokea kama mgao.
Gordon alisema wamewekeza dola za Kimarekani milioni 65 kwenye miradi ya maendeleo ya jamii . Alisema hivi sasa wanatoa ajira zaidi ya 45,000 nchini.
Post a Comment