Siku chache tangu kamati ya nidhamu ya TFF iwaadhibu baadhi ya viongozi wa vilabu vya ligi daraja la kwanza na kuvishusha vilabu hivyo kutokana na kupatikana na hatia ya kupanga matokeo ya michezo ya kundi C Katibu wa TFF aibuka baada ya kuhusishwa.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mwesigwa Selestine amekanusha kuhusika na njama za upangaji matokeo ya michezo ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.
Licha ya kukanusha Mwesigwa ametishia kulifikisha mahakamani gazeti moja la kila siku nchini lililochapisha habari za kumuhusisha na mpango huo mchafu.
"Nimeshitushwa na kusikitishwa sana na habari hiyo juu yangu ambayo ni ya kutunga, yenye nia mbaya isiyokuwa ukweli wowote, kwani sijawahi kukaa na watu wowote kupanga njama yoyote iliyo kinyume na maadili ya mchezo wa mpira wa miguu,"amesema Mwesigwa.
Gazeti moja la leo nchini, limechapisha habari katika ukurasa wake wa 24 chini ya kichwa cha habari "Vigogo TFF wajikaanga" likisema katika ibara ya 7 kuwa kwenye mazungumzo yaliyochukua zaidi ya dakika 10 yalimhusisha pia Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa.
Yamkini hali bado si shwari TFF, baada ya kuvuja kwa sauti za maofisa wa shirikisho hilo wakiomba rushwa ya shilingi milioni kutoka kwa viongozi wa timu moja ya Daraja la Kwanza ili waisaidie kupanda Ligi Kuu.
Na jana TFF imetoa tamko la kusikitishwa na taarifa hizo na kuahidi kuwachukuliwa hatua kali maofisa wake waliohusika, ingawa imesema taarifa hizo hazihusiani na kesi ya kupanga matokeo iliyoamuliwa Aprili 3.
TFF imesema kwanza inachunguza kubaini uhalisia (authenticity) wa taarifa hizo na itachukua hatua kali sana kwa watumishi wa shirikisho na viongozi wa timu husika watakaobainika kushiriki vitendo vilivyo kinyume na maadili ya mpira wa miguu.
Tayari Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano TFF, Martin Chacha, mmoja wa watuhumiwa ameacha kazi tangu juzi. Katika barua yake aliyomwandikia Katibu Mkuu wa TFF, Chacha amesema amepata majukumu mapya ya kikazi ambayo pamoja na majukumu ya kifamilia yatamfanya akose muda wa kutumika vema katika nafasi yake katika Shirikisho.
Chacha alijiunga na TFF Julai 2014 kama Ofisa Mashindano na baadaye kuteuliwa kukaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Mashindano, kufuatia aliyekuwa anashikiria nafasi hiyo Boniface Wambura kuteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).
Post a Comment