Katibu Mkuu mpya wa Chadema Dk Vincent Mashinji.
Licha ya Katibu Mkuu mpya wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji, kutokuwa na jina kubwa katika ulingo wa siasa na wengi kumwona mgeni, ndiye aliyekuwa 'kichwa' (think tank) wa Ukawa, imefahamika.
Juzi, Chadema ilimteua Dk. Mashinji kuwa Katibu Mkuu mpya kushika
nafasi ya Dk. Willibrod Slaa, aliyejiuzulu nafasi hiyo Julai 30, mwaka
jana, kwa kile akichokieleza kuwa ni utaratibu kutofuatwa wa
kumkaribisha Edward Lowassa, aliyehamia katika chama hicho kutoka Chama
Cha Mapinduzi (CCM).
Hata hivyo, uteuzi wake umepokelewa kwa mtazamo tofauti kutokana na
kutokuwa na jina kubwa katika ulingo wa siasa, lakini imefahamika kuwa
ni mmoja wa watu waliofanikisha mipango mikakati ya Ukawa katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kupata mafanikio makubwa, baada ya kuwa
na wabunge 113 bungeni ikiwa ni wale wakuchaguliwa na viti maalumu.
Idadi hiyo ni kubwa zaidi kupatikana tangu kurejeshwa kwa mfumo wa
vyama vingi mwaka 1992 na kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa kwanza
unaojumuisha vyama vingi mwaka 1995.
Katika mafanikio hayo, Dk. Mashinji alikuwa Makamu Mwenyekiti wa
Kamati ya Sera na Wanataaluma wa Ukawa na ndio walioandaa Ilani ya
Chadema katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Akielezea uwezo wake na anavyomfahamu, Mwenyekiti wa Kamati ya
Sera na Wanataaluma wa Ukawa, Dk. Rodrick Kabangira, ambaye amefanya
kazi kwa karibu na Dk. Mashinji, alisema ni mtendaji mwenye malengo ya
kimkakati na kufuatilia kwa karibu anayoyatenda.
"Nilifahamiana naye mwaka 2011 tulipokuwa tunaandika majarida
mbalimbali ambayo tuliyawasilisha Chadema kama la namna ya kuboresha
sekta ya afya na baadaye kuandika ilani, lakini katika Kamati ya Ufundi
ya Ukawa, tumefanya kazi pamoja. Namfahamu vizuri ni mtu sahihi kwa
Chadema katika kuelekea mwaka 2020," alisema.
Alisema wakati wa kampeni za uchaguzi, alikuwa mzungumzaji wa namna
Sera na Ilani ya Chadema inavyoweza kutekelezwa kwa kuwa anaijua
kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho na kwamba kwa mwonekano ni
mpole na anayezungumza taratibu, lakini anatoa neno zito.
AMWAGA SERA FURAHISHA
Akihutubia mamia ya wananchi wa Mwanza katika viwanja vya Furahisha
jana, Dk. Mashinji alisema ataongoza kimkakati zaidi kwa kuwa na
mabadiliko ya kimfumo ndani na nje ya chama kwa kujenga matawi ya chama
katika kila eneo.
"Naagiza kila kata kuwe na kamati za ufuatiliaji palipo na diwani
na ambako hakuna ili kuhakikisha masuala ya wananchi yanafuatiliwa kwa
karibu katika sekta mbalimbali kama elimu, maji na mengine. Madiwani
wafanye kazi, hatukuwapeleka kuuza sura bali kusimamia kwa karibu
maslahi ya wananchi," alisema
Aidha, aliagiza wabunge wote wa Ukawa kugeuza suala la Katiba Mpya
ni agenda ya kudumu kwa kila dakika wanazopata ndani ya Bunge na kwamba
kikosi cha kimkakati ndani ya chama kitaimarishwa katika utekelezaji wa
shughuli zinazolenga kutetea maslahi ya wananchi.
Dk. Mashinji alisema ni lazima maeneo yanayoongozwa na Ukawa,
ustawi wa wananchi uonekane na kwamba mambo yatakayosimamiwa ni
mabadiliko ya wananchi ili washike hatamu ya chama na viongozi
washirikiane nao.
Lingine ni kujiandaa kwenda kwa kasi kwani kwenda pole pole jua
litazama na giza kuingia na kushindwa kusonga mbele kufikia malengo ya
kuchukua dola m,waka 2020.
ATAJA VIPAUMBELE VYAKE
Dk. Mashinji ameweka wazi vipaumbele vitano ambavyo ataanza navyo
baada ya kuingia ofisini katika kuhakikisha Chadema inafanikiwa kushika
dola katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, ikiwamo kukipeleka chama hadi
kwa wananchi wa kawaida.
Akizungumza jana na Nipashe, aliwashukuru wajumbe wa Baraza Kuu
waliompigia kura za ndiyo kwa asilimia 100 huku alitaja vipaumbele hivyo
kuwa ni utekelezaji wa ilani ya Chadema katika halmashauri
wanazoongoza, kupinga rushwa na makundi yanayotaka kumea, Katiba Mpya na
kusimamia mabadiliko ndani na nje ya chama.
Alisema wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu kaulimbiu kubwa ya chama
hicho ilikuwa mabadiliko ambayo hayajahitimishwa kwa kushindwa uchaguzi
bali yametajwa katika ilani na yatatekelezwa kwa vitendo.
"Baraza Kuu na wengine bado tuna jukumu la kuwasimamia na kuwatetea
Watanzania. Tusiogope licha ya watu kunakili mambo yetu na kutaka
kuyatekeleza, hawawezi kutufikia sisi ambao ndio tunajua utekelezaji
wake, twendeni katika kiini cha tatizo," alisema.
Dk. Mashinji ambaye aliambiwa uteuzi wake na Mwenyekiti wa Taifa,
Freeman Mbowe, wakiwa hotelini, alitaja kingine ni kukisogeza chama kwa
wananchi zaidi kwani kufanya operesheni mbalimbali na mikakati ya
kichama kwa kuwa mtaji mkubwa wa chama ni watu.
"Msingi wa chama uko chini, mtaji wa chama ni watu na siyo
vipeperushi, magari. Hezekiah Wenje akishinda kesi si yeye ni
Wananyamagana wameshinda, hivyo ni lazima tuwafikie wannachi huko waliko
ili 2020 tuweze kushinda uchaguzi,"alisisitiza.
Alisema kazi iliyoko mbele yake si nyepesi, lakini watafikaje Ikulu
itajulikana baada ya kufika mtoni, na kuwataka wanachama na viongozi
kutoogopa polisi na vyombo vingine vya dola vinavyotumika kuwanyanyasa.
Kipaumbele kingine ni kusimamia mabadiliko ya Katiba Mpya ambayo
yalianza kwa kuhakikisha mifumo iliyopo inabadilika kwa kuwa imekuwa
chanzo kikubwa cha kuwanyima haki za msingi na ukuaji wa uchumi wa
Watanzania.
"Hatuwezi kupiga hatua kubwa kimaendeleo kwa katiba tuliyonayo au
iliyopendekezwa na Bunge Maalumu. Tuna matatizo nyeti ya kitaifa ambayo
chanzo chake kikubwa ni mfumo. Ukiangalia suala la rushwa utabaini shida
ni mfumo uliopo na ambao tunahitaji kuubadili kwa kutumia Katiba Mpya,
hivyo nikiiingia ofisini litakuwa kipaumbele," alisema.
Aliongeza kuwa: "Lengo letu ni nguvu ya umma, tuiwezeshe kutambua
haki zao mfano mgogoro mkubwa baina ya wenyeviti na mameya wa
halmashauri ni wakuu wa wilaya na mkoa kuingilia utendaji wa halmashauri
kwa kuwa kuna mifumo ya kikoloni kwa Katiba Mpya tutaiondoa."
Dk. Mashinji alisema lingine ni kusimamia utekelezaji wa Ilani ya
Chadema 2015, ambayo alishiriki kuiandaa tangu mwanzo na anajua
inavyoweza kutekelezwa kivitendo katika halmashauri zinazoongozwa na
Chadema katika kuleta maendeleo endelevu ya wananchi.
Katibu huyo ambaye ni Daktari wa Binadamu, alisema pia ni lazima
kuwa pamoja katika ujenzi wa chama na kushika hatamu, huku akitumia
mfano wa maji ambayo huenda pamoja na yanapofika kwenye maporomoko
hushuka pamoja.
Jambo lingine ni kupinga rushwa na makundi ambayo yameanza kumea
ndani ya chama, ili kuendelea kukitofautisha chama hicho na kingine na
kudhihirishia umma kuwa wamejipanga kushuka dola ifikapo 2020.
WABUNGE CHADEMA WAMZUNGUMZIA
Mbunge wa Moshi Mjini, Jaffary Michael, alisema chama kimepata mtu
sahihi kwa wakati sahihi kwa kuwa moja kwa moja inakwenda kuvunja
propaganda zilizopandikizwa kuwa ni chama cha Kaskazini.
Alisema ataleta mawazo mapya ndani ya chama kuliko kuendelea na
watu wale wale wenye mawazo yale yale na akipewa ushirikiano ataweza
kuvaa viatu vya Dk. Slaa, kwa kusimamia maono yake ambayo alitumia muda
wake mwingi katika ujenzi wa chama imara.
Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro, alisema uwezo wa mwenyekiti
wa taifa kuficha siri ni ushahidi tosha kuwa chama kinasiri na
intelejensia ya hali ya juu na kina sifa za kushika dola kwa mwaka 2020.
Alisema Dk. Mashinji si mgeni katika utendaji serikalini na
harakati mbalimbali ikiwamo kutetea maslahi ya madaktari na sekta ya
afya ambayo inakabiliwa na matatizo mengi hadi sasa, hivyo kwa kumtumia
wataweza kunyonya ujuzi na kuupeleka katika halmashauri zinazoongzwa na
Chadema.
Naye Mwalimu alisema siku zote duniani hakuna mbadala wa mtu kwa
kuwa kila mmoja ana uwezo, uimara na udhaifu wake, kinachotakiwa ni
kutekeleza majukumu kwa viwango vinavyotakiwa.
"Nimeshika nafasi ya kaimu katibu, haikuwa kazi rahisi kwa kuwa
nafadi hii ni nyeti sana, kila mtu anakuangalia wewe, lakini naamini
bosi mpya tuliyempata ni mtu imara, anaijua Chadema siyo kwa kuisoma,
bali kushiriki ikiwamo kuandika ilani na machapisho mbalimbali,"
alibainisha.
Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Kiwelu, alisema kwa kiongozi huyo
anaiona Chadema mpya kwa kuwa ni mtu mwenye uwezo na anafahamu
anachokitenda.
Awali, akizungumza wakati wa kumuombea kura kwa Baraza Kuu, Mbowe,
alisema ameona Dk. Mashinji anastahili kuendeleza guruduma la chama
hicho kwa kuwa ni mtu makini, mwenye maono na anayejua atendalo.
Mjumbe wa Kamati Kuu, Lowassa, alisema Mbowe amedhihirishia umma
kuwa uamuzi wake ulikuwa makini sana kwa kuwa ameleta mtu kijana na
shupavu hasa katika nyakati za mabadiliko.
"Tumekupa imani kubwa, chama kinachofuata kuongoza nchi ni
Chadema, lengo letu ni kukamata dola na rafiki yetu wa kweli ni
kutuwezesha kufika Ikulu 2020," alisema.
WADAU WAPONGEZA
Uteuzi wa Dk. Mashinji kuwa Katibu Mkuu wa Chadema umepokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wanasiasa na wasomi nchini.
Baadhi ya makundi hayo, wameeleza kuwa Chadema imemteua mtu ambaye
alikuwa hafahamiki kwa wananchi, hivyo imekuwa ‘surprise’ kwa wanachama
wao, kwa kuwa walikuwa wanatarajia kusikia jina kubwa.
Mtaalamu na mchambuzi wa masuala ya siasa, Abdulhakim Atiki,
alisema pamoja na kuwa Mashinji hafahamiki kwa wananchi, lakini alikuwa
ni mmojawapo wa wanachama walioshiriki katika kutengeneza Ilani ya Ukawa
wakati wa uchaguzi mkuu.
Alisema ni kijana mwenye uwezo wa kuongoza Chadema kama makatibu wakuu wengine waliotangulia.
Alisema tangu kuondoka kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho,
Dk. Aman Kabourou, aliyetokea Kanda ya Ziwa, hakukuwa na katibu mkuu
mwingine aliyetokea upande huo, hadi alipoteuliwa Mashinji.
“Nadhani Chadema wamezingatia ukanda zaidi, tena ukizingatia wakati
wa uchaguzi mkuu maeneo ya Kanda ya Ziwa hawakufanya vizuri, hivyo
wamemteua Mashinji ili kujiimarisha zaidi,” alisema.
Naye mwanazuoni kutoka Chuo cha Diplomasia, Israel Sosthenes,
alisema hamfahamu Dk. Mashinji vizuri, lakini Chadema hadi kumteua
kushika nafasi hiyo ya juu watakuwa wako sahihi na uhakikia na mtu huyo.
Alisema katibu mkuu ndiye mtendaji mkuu katika usimamizi wa chama, na kwamba ni mapema kumzungumzia kama ataweza au la.
Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Anna Mghwira, alisema hakuwa
anamfahamu Dk. Mashinji, na kwamba amemfahamu mara baada ya kuteuliwa.
Alisema Chadema ni chama kikubwa nchini, hivyo hakiwezi kumtemteua
mtu kushika nafasi hiyo kubwa ndani ya chama kama uwezo wake ni mdogo.
Naye Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya
Siasa ya Sayansi, Dk. Bashiru Ally, alisema hamfahamu Dk. Mashinji
utendaji wake kiundani, kwa kuwa ni mara ya kwanza kumsikia.
Alisema anawafahamu viongozi wakuu wote wa Chadema, alisema Dk.
Mashinji hakuwahi kumwona kumwona wala kumsikia akishiriki katika
masuala ya chama, alisema kama aliwahi kushiriki itakuwa ngazi za chini.
Alisema uteuzi wake unaweza kuwa na faida ndani ya Chadema, kwa
kuwa ni mtu ambaye hana mambo mengi kama walivyo viongozi wengine
wakubwa ndani ya chama hicho.
Aliongeza kuwa, Dk. Mashinji ni jina jipya pia, ni kijana ambaye anaweza kumudu kazi ya ukatibu mkuu wa chama.
Post a Comment