Msanii
wa nyimbo za injili nchini, Rose Mhando, ameshtakiwa kwa Waziri wa
Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye, kwa kitendo cha
utapeli na kushindwa kutekeleza mkataba wa kuhudhuria na kutumbuiza
kwenye Tamasha la Pasaka lililofanyika jijini Mwanza licha ya kulipwa
gharama zote alizotaka.
Mkurugenzi
wa Kampuni ya Msama Promotions inayoongozwa na Alex Msama, ambayo ina
mkataba naye imekuwa ikiuza na kuandaa matamasha ya msanii huyo pamoja
na tamasha la Pasaka la kila mwaka, alimweleza Waziri Nnauye, mbele ya
halaiki ya wananchi alipokuwa mgeni rasmi wa sherehe za tamasha hilo
lililofanyika kwa mara ya kwanza jijini Mwanza na mikoa ya Kanda ya
Ziwa.
Msama
alieleza kusikitishwa na kitendo cha Rose Mhando kuingia mitini ilihali
akiwa ameingia mkataba na kulipwa gharama zote pamoja na nauli alizodai
kabla ya kuanza safari kufika Geita, Mwanza na Kahama kujiunga na
wasanii wenzake kwa ajili ya kutumbuiza katika tamasha hilo.
“Mheshimiwa
Waziri, Rose Mhando naye amekuwa ni jipu kwa kuwa amefanya utapeli kwa
kukubali kulipwa gharama zake zote lakini ameshindwa kuhudhuria na
kutumbuiza kama wenzake wakina Solomon Mkubwa, Bonny Mwaitege, Upendo
Nkone na wengine uliowashuhudia hapa.
“Hii
ni mara ya tatu amekuwa akifanya hivi na mara kwa mara nimekuwa
nikimsamehe,” alisema bila kutaja kiasi alichomlipa katika mkataba
waliokubaliana ili aweze kufanya onyesho hilo.
Msama
pia akatumia fursa hiyo kuwaomba radhi wananchi waliofika katika Uwanja
wa CCM Kirumba kwa kutegemea mwimbaji huyo angekuwepo na kutumbuiza na
wenzake lakini kilichotokea ni aibu na utapeli wa msanii huyo mkubwa wa
nyimbo za injili aliyejizolea umaarufu ndani na nje ya nchi.
“Kuanzia
leo mtu yeyote asije akaingizwa mjini na Rose Mhando kwa kuingia naye
makubaliano akidhani yupo chini ya Kampuni ya Msama Promotions, kwa
kitendo alichoendelea kukifanya naomba kutangaza rasmi kuvunja mkataba
wa kufanya kazi na msanii huyo ili kulinda hadhi na heshima ya Kampuni
yangu,” alisisitiza Msama.
Msama
aliomba wananchi waendelee kuipa sapoti kampuni yake kwa kuwa imekuwa
ikirejesha mapato ya viingilio na sadaka katika tamasha hilo kwa jamii
hasa kwa watu wasiojiweza, makundi maalumu pamoja na kuendeleza vipaji
vya wasanii chipukizi wa nyimbo za injili nchini kote.
Hata
hivyo, wadau mbalimbali waliokuwepo katika uzinduzi huo walisikitishwa
na kutokutokea kwa mwanamuziki huyo huku wengine wakimlalamikia kuwa na
tabia hizo kwa muda mrefu na kufanya bila woga na hofu yoyote.
Mwanamuziki
huyo aliwahi kuripotiwa kutuhumiwa kufanya udanganyifu kwa kupokea
zaidi ya Sh milioni 3 na kisha kushindwa kufanya onyesho katika tamasha
la nyimbo za injili lililoandaliwa mkoani Njombe mwaka jana.
Mkurugenzi
wa Kampuni ya The Comfort Gospel Promotions, Seth Sedekia, ndiye
alimfungulia kesi hiyo katika kituo kikuu cha polisi Njombe na akapewa
RB namba: NJ/RB/1793/2015.
Kushindwa
kutokea kwa mwanamuziki huyo siku hiyo ya Jumapili iliyopita,
kuliwafanya mashabiki waliokuwa wamelipa kiingilio cha shilingi 5,000
kila mmoja kuzusha vurugu kubwa kwa mwandaaji huyo wakidai wametapeliwa
huku wengine wakionyesha kuchukizwa na kitendo cha mwanamuziki huyo
kushindwa kutokea kufanya onyesho hilo.
Mwandaaji
wa onyesho hilo, Sedekia alisema amefikia hatua ya kufungua kesi kituo
cha polisi kufuatia kumlipa fedha zote shilingi milioni tatu Mhando
ambazo alisaini mkataba naye akiwa mjini Dodoma kwa ajili ya kufanya
onyesho mjini Njombe. Katika onyesho hilo, Mhando alitarajiwa
kushirikiana na msanii wa nyimbo za injili, Happy Kamili kutoka jijini
Mbeya ambaye alifika katika tamasha hilo akishirikiana na wasanii
wengine kutoka mjini Njombe.
Ofisa
Habari wa Kamanda wa Polisi mkoani Njombe, Franco Malimba, alipoulizwa
juu ya kuwepo kwa taarifa hizo katika kituo cha polisi, alikiri kuwepo
lakini alisema hawezi kulizungumzia kwa sababu halijafika ngazi za juu.
Post a Comment