Ikiwa ni miezi minane tangu Waziri Mkuu
wa zamani, Edward Lowassa, kuhamia CCM na kutua Chadema, jana alitoa
sadaka yake ya kumshukuru Mungu kwa mambo mengi aliyomtendea na
anayoendelea kumtendea.
Hata hivyo, wakati Watanzania wengi
wakisubiri kauli ya Lowassa aliyegombea urais 2015, kwa tiketi cha
Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa, kuhusu uchaguzi wa Zanzibar, akiwa
katika Kanisa Kuu la Kilutheri la Azania Front jijini Dar es Salaam alisema: "Niacheni kwanza".
Lowassa ambaye alishiriki ibada hiyo
maalum ya kutoa sadaka ya shukrani yake na familia, alipoulizwa juu ya
maoni yake kuhusiana na uchaguzi huo, alisema “Tungoje kidogo
kitakachoendelea huko. Niache kwanza nitaongea.”
Aidha, aliwapongeza viongozi wa dini kwa
kuhuribi amani nchini na kwamba ndiyo tunu pekee inayotakiwa kulindwa
kwa kiasi kikubwa.
“Nawatakia sherehe njema wabarikiwe katika sherehe hii ya Pasaka, tuendelee kuhubiri amani ndiyo tuzo pekee tuliyonayo.
Nawashukuru viongozi wa dini kufanya wajibu wao, ni wajibu wetu nasi kufanya wajibu wetu kwa hayo tuliyohubiriwa,” alisema.
Juzi wakati wa ibada ya Pasaka katika
kanisa hilo, kulikuwa na tetesi za Lowassa kuwapo na wangekutana uso kwa
uso kwa mara ya kwanza na Rais Dk. John Magufuli, ambaye alisali
kanisani hapo kwa kushtukiza.
Katika ibada hiyo iliyoongozwa na Askofu
wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa, aliwatangazia
waumini kuwa Lowassa na familia yake watatoa sadaka maalum ya shukrani
kwa Mungu kutokana na mambo mbalimbali aliyowatendea na anayoendelea
kuwatendea.
Kama Lowassa angeshiriki ibada ya juzi,
ingekuwa ni mara ya kwanza kwa wawili hao ambao walikuwa wagombea
wanaochuana kwa karibu zaidi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kukutana
na kukaa katika eneo moja.
Katika uchaguzi huo Okotoba 25, mwaka
jana, Dk. Magufuli aliibuka mshindi kwa zaidi ya kura milioni nane dhidi
ya Lowassa aliyepata kura zaidi ya milioni sita.
Hata hivyo, Lowasaa amekuwa akipinga matokeo hayo akidai kuwa alishinda uchaguzi huo kwa zaidi ya asilimia 64.
Duru za kisiasa zinaeleza kuwa Lowassa
angeweza kugusia hali ya kisiasa Zanzibar na hasa uchaguzi wa marudio
uliofanyika bila wapinzani wakuu wa CCM, ambao ni CUF sambamba na
utendaji kazi wa Serikali ya Magufuli, lakini alikwepa.
Pia Lowassa ni msharika wa Azania Front, lakini katika ibada iliyohudhuriwa na Rais hakuwapo.
Akitoa salamu za Pasaka, Rais aliwaomba
Watanzania kumuombea kwa kuwa kazi ya uongozi aliyonayo siyo ndogo na
kuacha kubaguana kwa vyama, dini na makabila ikiwa ni pamoja na kufanya
kazi kwa bidii kuiwezesha Tanzania kupiga hatua kubwa kimaendeleo.
Katika ibada ya jana, Lowassa
aliambatana na familia yake, watoto na wakwe zake akiwamo Sioi Sumari,
huku viongozi wa Ukawa wakiwakilishwa na James Mbatia, ambaye pia ni
Mbunge wa Vunjo na Mwenyekiti wa NCCR-Magaeuzi.
Wengine waliohudhuria ni Meya wa Jiji la
Dar es Salaam, Isaya Mwita, Meya wa Ilala, Charles Kuyeko na Meya wa
Kinondoni, Jacob Boniface, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani,
Lawrance Masha na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji.
Watu maarufu waliohudhuria ibada hiyo ni
pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Malecela, Balozi Emmanuel Ole
Naiko na Askofu wa Dayosisi ya Morogoro, Jacob Ole Mameo.
Katika ibada hiyo, ilitarajiwa kuwa
Lowassa angezungumza, lakini Askofu Malasusa alimkaribisha Askofu Mameo
kuzungumza kwa niaba ya wageni wote ambaye alimpongeza kiongozi huyo kwa
kuwa mtoaji.
“Nimekuja kumsindikiza kaka yangu
Lowassa kutoa sadaka yake ya shukurani ya pekee maana ni jambo la busara
na hekima kumtolea Mungu, nilimkaribisha wakati natoa shukrani yangu ya
pekee Ubungo kanisani, nakumbuka maneno aliyoniambia,” alisema na
kuongeza:
“Baba Askofu Mameo umekuwa mfano wa
viongozi wa juu wa Kanisa wanaokumbuka kutoa shukrani kanisani maana
Wakristo raia tumezoea kutoa na ninyi (viongozi wa kanisa) hamtoi, nami
nasema ni bahati ya pekee kuwa na watu wacha Mungu wanaokumbuka
kumrudishia Mungu shukrani zao kwa mambo aliyowatendea.Tunapoona watu wa
aina hiyo, ni lazima tuwaunge mkono na Mungu ndivyo anavyotaka,
tunafanyiwa mambo mengi sana na Mungu.”
“Namshukuru sana kaka yangu Lowassa
anamtolea Mungu mara kwa mara na anatendewa mambo mengi na Mungu na
ndiyo maana hadi sasa yupo na Mungu, anapenda watu wanaotoa shukrani.
Katika vitabu vya Ijinili, Yesu aliwaponya watu 10, mmoja ndiye alirudi
kushukuru, sote tuna sababu ya kumshukuru Mungu kwani tunatendewa mengi
sana,” alisisitiza.
“Lowassa tutaendelea kukuunga mkono,
umetendewa mambo mengi sana, kutoa siyo jambo la kuiga ni la moyoni na
kama siyo la kuiga utaendelea kulitenda kila mara siyo kwa kuambiwa,”
alisisitiza.
SAFARI YA LOWASSA MILIMA NA MABONDE
Machi 20, mwaka 2014, CCM ilitangaza
kuwafungia kwa miezi 17 makada wake sita waliodaiwa kuanza kampeni za
urais kabla ya muda ulioruhusiwa na chama na walifunguliwa Mei 22, mwaka
jana.
Chama hicho kilisema kitafanya tathmini kama walikiuka kanuni za adhabu hiyo na iwapo ingebainika wangechukuliwa hatua zaidi.
Baada ya kufunguliwa na kabla ya
kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama chake (wakati huo) kupeperusha
bendera ya chama hicho, makundi mbalimbali yalikwenda nyumbani kwake
mjini Dodoma kumshawishi kuchukua fomu ya urais na ilipoelezwa kuwa
makundi hayo yaliandaliwa naye, alisema hawezi kuzuia mafuriko kwa
mikono.
Lowassa alikutana na wahariri na
waandishi wa vyombo mbalimbali nchini Mei 27, mwaka jana na kutoa
ufafanuzi wa masuala mbalimbali ikiwamo kueleza safari ya matumani.
Lowassa akiwa ameambatana na makada
mbalimbali wa chama hicho katika Uwanja wa Shekhe Amri Abeid jijini
Arusha Mei 30, mwaka jana na kutangaza kuanza safari ya matumaini ambayo
itatimiza ndoto za Watanzania kupata elimu bure, majisafi na salama na
maendeleo kwa ujumla, kisha kutangaza rasmi nia ya kuwania urais kwa
tiketi ya CCM wakati huo.
Mafuriko ya Lowassa yaliteka jiji hilo
na kuvunja rekodi ya mikutano iliyowahi kufanyika nchini huku kukiwa na
viongozi maarufu kama kada wa zamani Kingunge Ngombale-Mwiru, wenyeviti
wa CCM wa mikoa mbalimbali na waliowahi kuwa mawaziri na watumishi
serikalini.
Lowassa alichukua fomu katika makao
makuu ya CCM mjini Dodoma Juni 4, mwaka jana na kutembeza kuomba
wadhamini kwenye mikoa yote nchini huku kukiwa na mafuriko ya watu na
alirejesha Julai mosi, mwaka jana.
Hata hivyo, safari ya matumaini ya
kiongozi huyo kwa CCM iliishia Julai 10, mwaka jana, baada ya kikao cha
Kamati Kuu (CC) kukata jina lake na kupitisha jina la Dk. Magufuli,
jambo lililozua taharuki na maandamano ya wafuasi wake katika mji wa
Dodoma na viunga vyake kiasi cha polisi kuingilia kati kuwatawanya.
Julai 27, mwaka jana, Lowassa alijiunga
rasmi Chadema na kukabidhiwa kadi ya uanachama wakati wa kikao cha
Kamati Kuu ya chama hicho na baadaye alitangaza kupeperusha bendera ya
Ukawa katika uchaguzi huo.
Baada ya kuhama, makada wengine akiwamo
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, walimfuata na alichukua fomu ya
kuomba ridhaa ya Chadema kuwania nafasi hiyo.
Agosti 10, mwaka jana, Lowassa alichukua fomu ya kuwania urais katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
Nec ilipuliza kipenga cha kampeni Agosti
22, mwaka jana, Lowassa alifanya kampeni kwa gari na helkopta katika
maeneo mbalimbali nchini, huku kukiwa na vita kali ikiwamo ya kueleza
udhaifu wa afya yake na kutuhumiwa kwenye majukwaa ya kisiasa ya
wapinzani wake wa karibu.
Oktoba 29, mwaka jana, Nec ilimtangaza
Dk. Magufuli mshindi wa nafasi ya urais kwa kura 8,882,935 sawa na
asilimia 58.46 dhidi ya Lowassa aliyepata kura 6,072,848 sawa na
asilimia 39.97.
Baada ya matokeo hayo, Lowassa alikuwa
kimya na licha ya kushawishiwa na makundi ya vijana kutoa tamko kali,
hakufanya hivyo na kuwataka kuwa watulivu.
Kutokana na hali hiyo, Desemba 19, mwaka jana, Lowassa alitunukiwa tuzo ya amani na taasisi za kidini 1,200.
Post a Comment