Kwa mara ya kwanza tangu Kamati Kuu ya CCM ilipomuengua kwenye
kinyang’anyiro cha uspika, Samuel Sita ambaye alikuwa Spika wa Bunge la
Tisa, jana ameweka bayana mustakabali wake; ameamua kustaafu siasa.
Sitta aliongoza kwa mafanikio Bunge la Tisa kiasi cha kumfanya apewe
kirahisi uenyekiti wa Bunge la Katiba na hivyo kujijengea jina miongoni
mwa wana-CCM kiasi cha kujitumbukiza kwenye mbio za urais na baadaye
kutaka kurudi tena kuliongoza Bunge la Kumi na Moja.
Lakini hakufanikiwa kupitishwa kuwania urais wala kugombea uspika, ambao aliahidi kuwa angeengulkiwa angefika hata mahakamani.
Lakini jana alikuwa na kauli tofauti.
“Mambo ya siasa kwa sasa basi,” alisema Sitta alipoulizwa na kuhusu
mipango yake ya baadaye baada ya kutopitishwa na CCM kuwania uspika.
Sitta ambaye amewahi kuongoza wizara mbalimbali, alisema kwa sasa
anajikita katika uandishi wa vitabu na kwamba kwa umri alionao na
utumishi wake serikalini, umefika wakati kwake kupumzika na kutoa
ushauri wa masuala mbalimbali kwa wale watakaohitaji mchango wake.
Novemba 15, Kamati Kuu ya CCM ilimtosa Sitta na wengine waliojitokeza
kuwania uspika na badala yake ikateua majina matatu kwa ajili ya
kupigiwa kura na wabunge wa CCM, ambao walimchagua mbunge wa Kongwa, Job
Ndugai kuwa Spika.
Kuenguliwa kwa Sitta kulikuwa ni pigo lake la pili katika nafasi ya hiyo
baada ya kukatwa na kikao hicho mwaka 2010 alipokuwa akitetea nafasi
yake. Wakati huo Anne Makinda alichaguliwa kuongoza Bunge la Kumi
lililomaliza muda wake mwaka huu.
Sitta alijizolea sifa wakati akiwa Spika wa Bunge la Tisa kuanzia mwaka
2005 hadi 2010, baada ya kuliongoza kuibua mijadala mbalimbali dhidi ya
Serikali na kashfa ya Richmond iliyomfanya Edward Lowasa kujiuzulu
uwaziri mkuu.
Baada ya kung’atuka
Alipoulizwa atajishughulisha na nini baada ya kustaafu, Sitta ambaye pia
alikuwa mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba alisema: “Nipo tu
nyumbani nimepumzika. Naridhika na niliyoyafanya kwa Taifa. Wale
watakaotaka kupata ushauri wakinifuata nitawasikiliza.”
Alisema kwa sasa anaandika makala ambazo baadaye ataziweka katika kitabu
chake kitakachoeleza hali ya nchi na historia za masuala mbalimbali.
“Ninachokiandika ni mtazamo wangu binafsi, ni jinsi ambavyo mimi ninaona kwa macho yangu,” alisema.
Alipoulizwa kama atakubali kuongoza wizara iwapo Rais John Magufuli
atamteua kuwa mbunge na kisha waziri alisema: “Tusizungumze jambo ambalo
halina mwelekeo huo.”
Hata hivyo, alisema kwa mtazamo wake hadhani kama anaweza kufikiriwa kuwamo katika baraza hilo.
Kupinga uspika kortini
Kuhusu sakata la uspika, Sitta alisema angekwenda mahakamani kupinga
kuondolewa kwake, kama tu mchakato wa chama hicho ungefanyika bila
kufuata taratibu na watu kuonewa.
Katika mazungumzo yake na Radio Uhuru FM wakati wa mchakato wa uspika,
Sitta alisema kutokana na hali ya joto la kisiasa ilivyo, ambayo
ilidhihirika zaidi wakati wa uchaguzi, wabunge walioshinda ni vijana na
ni wazi spika anayehitajika ni mwenye uzoefu.
Alisema licha ya kwamba wapo waliojaribu kumshawishi asigombee nafasi
hiyo tena, badala yake awe anatoa ushauri pale inapobidi, alisisitiza
bado ana wito wa kuwatumikia wananchi kwa njia hiyo.
“Niliposema (nitakwenda mahakamani) kama nisipoteuliwa na CCM kuwania
uspika nililenga kama kitatokea kitu kama uonevu. Yaani kama vingeletwa
vigezo ambavyo havipo katika mchakato,” alisema.
“Kama unakumbuka mwaka 2010 kililetwa kigezo cha ‘spika mwanamke’. Hicho
ndicho kitu ambacho nilikilenga kwamba kikijitokeza sitakikubali. Uzuri
ni kuwa hakikuwapo na kumbuka kuwa jambo lile (la kupitishwa kuwania
uspika) lilikuwa ni uamuzi wa chama si mtu,” alisema Sitta.
Post a Comment