Mkuu
wa Wilaya ya Karatu, Mkoani Arusha Omary Kwaang’ (katikati mwenye
kaunda suti) akiwa na baadhi ya watumishi wa wilaya hiyo, akikagua lambo
la maji eneo la Endesh, linalotumiwa na mifugo na binadamu,
lililogharimu sh169 milioni kwa ufadhili wa shirika la World Vision.
Mkuu
wa Wilaya ya Karatu, Mkoani Arusha Omary Kwaang’ (kushoto) akiwa na
baadhi ya watumishi wa wilaya hiyo, akikagua lambo la maji eneo la
Endesh, linalotumiwa na mifugo na binadamu, lililogharimu sh 169 milioni
kwa ufadhili wa shirika la World Vision.
WANANCHI
12,082 wa Kata ya Baray Wilayani Karatu Mkoani Arusha wamekabidhiwa
miradi nane ya elimu na afya ambayo imegharimu sh447.8 milioni kwa
ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la World Vision Korea.
Mratibu
wa mradi wa World vision Karatu John Massenza akikabidhi jana miradi
hiyo kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo John Mabula
alisema itawanufaika wakazi wa vijiji vitatu vya Dumbachang, Mbuga
Nyekundu na Jobaj.
Massenza
alitaja miradi hiyo kuwa ni madarasa matatu, ofisi ya walimu na choo
cha wanafunzi ya shule ya msingi Mbuyuni iliyogharimu sh83 milioni na
madawati 200 kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo iliyogharimu sh13
milioni.
Alitaja
mingine ni samani na vifaa zahanati ya Endesh sh11 milioni, madawati
100 ya shule ya msingi Mohedagew Gidamilanda sh13 milioni na vifaa vya
vikundi 11 vya hisa vijiji vya Dumbecha, Jobaj na Mbuga Nyekundu sh5
milioni.
“Mingine
ni lambo kwa matumizi ya binadamu na wanyama sh169 milioni, zahanati na
choo Endesh sh83 milioni, vitabu na vifaa vya ufundishaji 1,570 vya
sh11 milioni na madarasa mawili sh53.9 Endesh,” alisema Massenza.
Alisema
katika wilaya hiyo, World vision ilianza kufanya shughuli zake mwaka
2009 kwenye tarafa za Endabash na Lake Eyasi ambapo imekuwa ikitekeleza
miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye sekta tofauti.
“Miradi
hiyo iliyotekelezwa ni ya upande wa sekta ya elimu, afya, kilimo, maji
na ufadhili wa watoto kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya ya
Karatu na wana jamii wa eneo hili,” alisema Massenza.
Kwa
upande wake, mkuu wa wilaya ya Karatu Omary Kwaang’ alipongeza shirika
la World vision kwa kufanikisha ujenzi wa miradi hiyo ya thamani ya
sh447.8 milioni ambayo itanufaisha jamii ya wafugaji na wakulima.
Kwaang’
aliwataka wananchi wa kata hiyo kuhakikisha kuwa wanaitunza miradi hiyo
ili iwe endelevu na kudumu kwa faida ya kizazi kilichopo na kijacho,
kwani shirika la World vision limetumia gharama kubwa kufanikisha miradi
hiyo.
Alisema
kwenye suala la zahanati wilaya ya Karatu imepiga hatua kwenye
kutekeleza sera ya wizara ya afya inayotaka kila kijiji kiwe na zahanati
kwani wamejenga zahanati kwenye vijiji 45kati vijiji 58 hivyo vimebaki
vijiji 13.
“Nawapongeza
viongozi na wananchi wa wilaya ya Karatu kwa kupiga hatua kwenye ujenzi
wa zahanati, ila tujitahidi kwenye elimu kwani vyumba vya madarasa
vinahitajika 1,109 na vilivyopo ni 875,” alisema Kwaang’.
Alisema
kwenye ujenzi wa nyumba za walimu kuna hitajika 694 na zilizopo ni 578
na matundu ya choo yanahitajika 1,221 na pungufu ni matundu 975 hivyo
wajitahidi kumalizia mapungufu yote wakishirikiana na serikali ya wilaya
hiyo.
Post a Comment