Baba Mtakatifu Francis jana aliwasili nchini Marekani kuanza ziara ya kwanza kuwahi kuifanya nchini humo maishani mwake.
Baba Mtakatifu Papa Francis akiwa katika mapokezi chini ya Rais Obama na familia yake
Kwa kawaida marais wa Marekani huwapokea wageni rasmi Ikulu ya nchi hiyo, lakini alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Kijeshi wa Andrews ulioko nje kidogo ya jiji la Washington, Baba Mtakatifu alipata heshima ya kulakiwa na Rais Obama na familia yake.
Mbali na gwaride la heshima, miongoni mwa waliokuweko kwenye mapokezi hayo rasmi ni pamoja na Makamo wa Rais wa Marekani Bwana Joe Biden na aila yake, watoto wa shule, na viongozi wa Kanisa Katoliki.
Akiwa jijini Washington, Baba Francis atafanya mazungumzo na Rais Obama, kukhutubia kikao cha pamoja cha Mabaraza ya Bunge la Marekani pamoja na kuongoza Ibada mbalimbali.
Ziara yake hiyo ya siku sita, pia itamfikisha kwenye miji ya New York na Philladelphia.
Akiwa jijini New York, Baba Francis ambaye ni kiongozi wa nne wa Vatican kuitembelea Marekani, atatembelea Umoja Wa Mataifa na eneo la Kituo Cha Biashara kiclichoteketezwa kwenye mashamulizi ya Septemba 11, 2001.
Kiongozi huyo wa Kanisa la Katoliki, atamalizia ziara yake katika jiji la Philladelphia, ambako anatarajiwa kuhudhuria kwenye Mkutano wa Familia wa Wakatoliki Duniani.
Miongoni mwa mambo yatakayopewa kipaumbele katika mzungumzo na khotuba zake nchini humu, ni pamoja na utoaji mimba, ndoa za jinsia moja, usawa katika maswala ya kiuchumi na kijamii, mazingira na uhamiaji.
Baba Francis amewasili Marekani akitokea Cuba baada ya kukamilisha ziara yake nchini humo.
Wachambuzi wanaona kuwa kuanza ziara yake nchini Marekani akitokea nchini Cuba, kunatoa ujumbe fulani kukhuasian na kuanza tena kwa mahusiano ya Kibalozi kati ya Marekani na Cuba baada ya kuvunjika kwa muda usipungua nusu karne.
Aidha kuingia Marekani akitokea Cuba kunatoa ishara juu ya mgogoro wa wakimbizi wanaoingia Marekani wakitokea nchi za Amerika ya Kusini.
Kwa upande mwengine, ziara hiyo inakuja katika wakati ambao Kanisa Katoliki limekuwa likikabiliwa na kashfa za ngono katika miaka ya hivi karibuni.
Aidha, inakuja katika wakati ambao harakati za ndoa za jinsia moja zikiwa zimepamba moto nchini Marekani.
Maswala hayo pia yamekuwa yakichukua nafasi za mbele katika kampeni za wagombea urais wa Marekani ambazo tayari zimeshamiri nchini humu.
Mbali na baraka inazotarajiwa kuletwa na Baba Mtakatifu chini humu, ziara hiyo pia itakuwa na athari zake za kiuchumi kutokana na usalama wa hali ya juu utakaokuwepo wkati wa ziara hiyo.
Baadhi ya mashirika ya utumaji vifurushi na mizigo kama vile UPS na Fedex, tayari yametangaza kutotoa huduma katika baadhi ya maeneo ambayo Baba Francis atatembelea.
Post a Comment