MGOMBEA Ubunge Jimbo la Ilala, Mussa Hassan Zungu amemweleza mgombea mwenza nafasi ya urais Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi. Samia Suluhu kuwa jimbo hilo limetenga kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuwakopesha wajasiliamali wanawake na vijana kupitia vikundi vyao.
Zungu aliyasema hayo alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji Ilani ya CCM kwa mgombea mwenza katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya Amana katika jimbo hilo jana jijini Dar es Salaam.
Zungu alisema utekelezaji wa ilani ya CCM imefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 95 hivyo wananchi hawana budi kukipa ridhaa tena chama hicho kiendelee kufanya vizuri. Alisema upande wa elimu jimbo hilo lilikuwa na shule sita za sekondari lakini katika utekelezaji wa ilani limefanikiwa kuongeza hadi kufikia shule 145 za sekondari huku wakifanikiwa kuboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za X-Ray hospitali ya Amana, ambapo awali ilikuwa juu.
Akizungumza katika mkutano huo Bi. Samia Suluhu alisema kiasi cha shs milioni 300 kilichotengwa kwa ajili ya wajasiliamali na Jimbo la Ilala hakitoshi kutokana na wingi wa wajasiliamali hivyo kuahidi kuangalia njia ya kuwaongeza ili kitosheleze.
Alisema ilani ya CCM imepanga kurasimisha biashara za wajasiliamali ili waweze kuwa na vikundi vinavyotambulika pamoja na biashara zao kuwawezesha kunufaika zaidi. Alisema serikali ya CCM itaunda mamlaka maalumu ambayo itafanya kazi ya kusimamia biashara za wajasiliamali ili ziweze kupata masoko ya uhakika kwa bidhaa zao. Aidha alisema wamepanga kuyaboresha masoko ya Kisutu, Kariakoo na Mchikichini ili yaweze kuwa na nafasi zaidi ya wafanyabiashara pamoja na kuyaboresha kiulinzi, usafi na usalama kwa wanaoyatumia.
Alisema wanategemea kutengeneza nafasi mpya 3,150 za wajasiliamali katika masoko hayo ili kutoa fursa kwa wengine kunufaika na biashara hizo. Alisema tayari maeneo mapya pia yametengwa ili kujenga masoko mapya kwa ajili ya wajasiliamali. Bi. Samia Suluhu alisema Serikali itaboresha madawati ya bodaboda na bajaji ili waweze kufanya kazi kwa kutambulika na kuongeza mipaka ya wao kuingia mjini ili kuondoa mvutano uliopo kwa sasa.
Post a Comment