Abbas Maziku akiwa katika moja ya shughuli
zake za kusafirisha mazao kuelekea mataifa mbalimbali katika Bandari ya
Mtwara kama
makontena yaliyohifadhiwa mazao hayo
yanavyoonekana nyuma yake.
|
Mfanyabiashara wa kimataifa, Abbas Maziku Bundala akiwa ofisini kwake maeneo ya Posta Mpya jijini Dar es Salaam. |
Mfanyabiashara wa kimataifa, Abbas Maziku Bundala akiwa na mfanyabiashara tajiri na mwenye umri mdogo anayemiliki Kampuni ya Mohammed Interprises(Metl)Mo Dewji |
Magunia ya korosho yakisubiri kupakiwa kwenye makontena tayari kwa kusafirishwa kwenda nchini Vietnam ambapo mfanyabiashara, Abbas Maziku Bundala hufanya nao biashara kwa mkataba maalumu. |
NA MWANDISHI WETU
BIASHARA ya
kusafirisha mazao ina ushindani mkubwa kutokana na kutawaliwa na matajiri
wenye asili ya Kiasia.
Sababu hiyo
imewafanya Waafrika wengi kutokuwa na uthubutu katika biashara hiyo kwa
kuhofia kutofanikiwa na kujitanua kibiashara.
Mbali na ugumu huo
lakini pia wengi hasa Watanzania wamejikuta wakiishia kuwa wafanyabiashara
wa kawaida na kupoteza fursa za kimataifa.
Kupoteza fursa muhimu
za kimataifa kumefanya wakose nafasi ambazo zingeweza kuwafanya kufikiri nje ya
boksi.
Makala hii inamwangazia
mfanyabiashara wa kwanza wa Kitanzania kufanya biashara ya kusafirisha korosho
kwenda nchini Vietnam,
Abbas Maziku Bundala .
Alipoanzia
Maziku anasema alianza
biashara ya kusafirisha mazao mnamo mwaka 2013 baada ya kuvutiwa na mjomba yake
ambaye alikuwa na mashamba yaliyokuwa na mazao mbalimbali.
Miongoni mwa
mazao ambayo Maziku alianza nayo na anaendelea nayo ni korosho, ufuta, mbaazi,
choroko, mtama, alizeti, mashudu ya pamba na pilipili Manga.
Anasema mazao hayo huyakusanya
kutoka kwa wafanyabiashara wadogo wadogo, wakulima pamoja na kwenye minada
inayofanywa na vyama vya ushirika katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Dodoma, Singida, Shinyanga
na Tanga.
Anayasafirisha kwa
njia gani?
Akizungumzia jinsi
anavyosafirisha mazao hayo, Maziku anasema hutumia gari kuyatoa mikoani hadi kuyafikisha
maghalani na kuyahifadhi kabla ya kufungasha.
“Wakati wa
kuyafungasha unapofika huwa nayafungasha kwa kutumia vibarua na katika
vifungashio vyangu huwa na nembo inayoonyesha jina la kampuni yangu
na baada ya hapo sampuli hupelekwa katika maabara za kupima ubora wa mazao
kimataifa iitwayo SGS na ndipo hufuatiwa na hatua ya mwisho ya
usafirishaji ambayo huwa natumia meli za mashirika mbalimbali ikiwamo
IPTL, MAERSK na nyinginezo kwa ajili ya kwenda nchini Vietnam,”
anasema Maziku.
Anabainisha baada ya
hatua zote hizo hufuata taratibu zinazotakiwa ikiwemo kulipia ushuru kwa Mamlaka
ya mapato nchini, (TRA), wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo na ufugaji, wanasheria
pamoja na maofisa wa Usalama wa Taifa ambao huhakikisha hatua zote halali
zimefuatwa.
Maziku anasema
kwamba kwa biashara za kimataifa Shirika la Viwango (TBS) na Mamlaka
ya Chakula na Dawa (TFDA) hawahusiki bali
wahusika wakuu ni SGS.
Anajiendeshaje kibiashara?
Maziku anajinasibu kwamba
biashara ya kuuza mazao nje ya nchi ina ushindani mkubwa.
Anasema anakumbuka
alianza na mtaji wa sh. 2,000,000 na sasa anazungumzia mtaji wa sh. milioni 200.
“Si rahisi
kufika nilipofikia kwasababu biashara hii ina ushindani mkubwa, ninashindani
na matajiri wakubwa wenye uwezo wa kujipangia bei za mazao hivyo ingawa
nimepiga hatua lakini bado ninahitaji kupanua biashara yangu zaidi na
zaidi”anasisitiza .
Anaeleza kwamba mwaka
2013 alipata hasara ya baada ya ubora wa mazao aliyopeleka kupimwa na
kuonekana upo kwenye kiwango cha 48 badala ya 51 inayotakiwa hivyo ilimpa
wakati mgumu na kuyumba kibiashara na mtaji wake kukata ndipo
alipolazimika kukopa fedha benki ambapo hadi sasa bado analipa deni hilo.
“Nilipata hasara
kubwa sana ambayo hadi leo hii bado ninalipa hilo deni nililokopa
benki ingawa pia fedha kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato
ya biashara zingine ninazozifanya zinaendelea kuifanya bishahara ya mazao
kwenda nje ya nchi iendelee kuwepo,” anasema.
Vikwazo vya
kibiashara
Maziku anakwenda
mbali na kueleza katika jambo lolote lenye mafanikio vikwazo huwa havikosekani
lakini kubwa katika ni mtaji.
Pia analia na
ukiritimba unaofanywa na benki mbalimbali ambao hutaka dhamana kubwa
kuliko uwezo wa mfanyabiashara.
Ukiachilia mbali
suala la benki, Maziku anasema kikwazo kingine ni ukiritimba kwenye vyama
vya ushirika katika suala zima la upangaji wa bei ambazo hukinzana na bei
ya katika soko la dunia hivyo inakuwa ngumu kwa wafanyabiasahara kufikia
malengo kutokana na kuepuka kupata hasara.
Aidha, anataja
vikwazo vingine ni wizi wa fedha unaofanywa na baadhi ya watu anaowaamini kumnunulia mazao
ambao hutoroka na fedha hivyo kufanya suala
la uaminifu kuwa mdogo na vikwazo vya ubora wa mazao.
Mafanikio
Akizungumzia
mafanikio Maziku anabainisha, tangu alipoanza biashara ameweza kuwa na
kampuni mbili zijulikazo kama Agromart Company
Limited (GEFU) na Lyone Investment Company Limited ambazo kwa pamoja
ameajiri wafanyakazi watano akiwemo Ofisa Rasilimali Watu, Mhasibu, katibu
Muhtasi, Mwanasheria na Meneja Mwendeshaji wa shughuli za kampuni.
Anaeleza kwa biashara
anayoifanya ameweza kujenga nyumba yake mwenyewe, kumiliki usafiri na kupata
fursa za kusafiri nchi mbalimbali kuhudhuria makongamano na maonyesho ya
biashara ya mazao jambo ambalo limemkutanisha na watu na kupanua wigo wa
biashara yake kimataifa.
Maziku anasema anatarajia
kufungua kampuni ya ujenzi ili mtaji wake uzunguke pamoja na kutoa ajira kwa vijana
mbalimbali wa Kitanzania.
Matarajio mengine ni
kuanzisha kiwanda cha uzalishaji wa bidhaa ndogo ndogo za
majumbani kama vile juisi, mafuta ya alizeti, mifuko ya plasitik pamoja na maji
ya kunywa kwa ushirikiano na wawekezaji kutoka nje kwa lengo
moja tu la kukuza uchumi wa Tanzania.
Aidha anasema anajihusisha
kikamilifu na masuala ya kijamii hasa kusaidia wasiojiweza ikiwemo
yatima lakini mambo hayo huyafanya nyuma ya pazia pasipo kujitangaza.
“Kidogo nilicho nacho
huwa nakitoa kwa wenye mahitaji maalum lakini huwa sijitangazi” anasema.
Maziku ni kijana wa
Kitanzania aliyezaliwa mwaka 1990, kitaaluma yeye ni mtaalamu wa masuala ya
benki na fedha fani ambayo alisoma katika chuo kikuu cha Zanzibar.
Pia aliwahi kufanya kazi Benki ya Exim kama ofisa wa kawaida wa benki ambayo alidumu nayo kabla
ya kugeukia katika biashara ya mazao.
Maziku ni mtoto wa
mwisho kwenye familia yao yenye watoto watatu,
ndoto yake ni kuwa mfanyabiashara mdogo mwenye mafanikio makubwa kama alivyo Mohammed Dewji(Mo).
Aidha Maziku anawashauri
vijana wenzake wawe na uthubutu kama aliokuwa
nao yeye, aliiona fursa kaichangamkia.
“Vijana
tusibweteke,vikwazo ni vingi,hatupaswi kukata tamaa, hata waliofanikiwa
kama akina Mo hawakuanzia juu, walipambana na uzuri ni kwamba Mo si
mchoyo, ni mtu anayejitoa, mwenye msaada katika mambo mbalimbali ya ushauri wa
kibiashara jambo ambalo linanifanya nimuheshimu na amechangia katika
mafanikio yangu ya kibiashara hivyo sitaacha kumshukuru,” anasema.
Post a Comment