Athari zaTeknolojia kwenye uchaguzi wa 2015 - Sehemu I
Tanzania inaingia katika kipindi kigumu na cha muhimu sana kwenye historia yake. Ni kipindi ambacho kitasaidia kuamua muelekeo wa nchi kwa miaka mitano inayokuja. Mara nyingi ifikapo wakati wa uchaguzi kuna mambo mengi hubadilika. Biashara huanza kuwa ngumu kutokana na hofu miongoni mwa watu. Pia, ushiriki wa watu kwenye kampeni hufanya muda mwingi kutumika huko hivyo kutoa muda mchache kwenye shughuli kama kazi.
Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, mwaka huu tutashuhudia mabadiliko makubwa sana, mabadiliko haya siyo tu aina ya watu wanaoshiriki kwenye kugombea nafasi mbalimbali, bali pia mfumo utakaotumika kwenye kampeni hadi upigaji kura. Mwaka huu tutashuhudia matumizi ya Tehama kwa kiwango kikubwa sana kwenye kampeni za uchaguzi na hata utangazaji na uchungaji wa matokeo ya chaguzi.Tutegemee kupata updates za matokeo ya kura toka kila kituo ndani ya dakika punde tuu wanapomaliza kuhesabu.
Kwa chama chochote kinachotaka kufikia watu na hatimaye kushinda, ni ngumu kufanikisha hilo bila kutumia Tehama. kwa maneno mengine, Tehama ndiyo itakayoongoza uchaguzi wa mwaka huu. Tumeona mfano wa Obama mwaka 2008. Akiongozwa na kauli mbiu yake ya pamoja tunaweza (Yes we can) na matumizi ya mitandao, Obama aliweza kufikisha ujumbe kwa vijana wengi kama ilivyo sasa kwa Tanzania, na hatimaye kushinda uchaguzi wa kihistoria.
Kwa Tanzania, tumeona jinsi gani vijana walivyo na chachu ya mabadiliko, tumeona ni jinsi gani vijana walivyokuwa wanakesha kwenye vituo vya kujiandikisha ili kupata kadi zao za kupigia kura. Ni vijana hawa ambao wamelala kwenye matumizi ya Teknolojia. Wao wanalala na Instagram, wanaamka na Twitter mchana wanashinda Whatsapp huki jioni wakitembelea Facebook. Iwe kwa kutumia komputa mpakato (Laptop) au kwa simu za mikononi. Haijalishi kijana huyu yupo kule kwetu Nyamwimbe au Mbezi Beach Goig, wote wanafikiwa na taarifa kwa uharaka wake.
Mitandao ya kijamii, kama Facebook, Twitter, Whatsapp, Instagram nk itachukua nafasi ya kipekee kabisa mwaka huu. Nakumbuka, Uchaguzi wa mwaka 2010 mitandao kama Jamii Forums ilijizolea umaarufu sana, ila mwaka huu tutegemee mambo tofauti sana.
Hebu tuangalie sababu zitakazosukuma matumizi ya Tehama kwa mazingira ya Tanzania.
Tabia za Watanzania.
Moja ya sifa kuu ya Watanzania, ni kutopenda kusoma makala ndefu,na sifa hii inaenda nchi nyingi Africa, ndiyo sababu kuna masihala wazungu husema, ukitaka kumnyima kitu muafrica, weka kwenye kitabu. Wengi hupenda picha na maelezo mache yaliyo rahisishwa (Summary). Kwenye kitabu chake cha How to Win Campaigns, Communications for Change, Chris Rose alisema, "Moja ya nguzo muhimu ya kushinda kampeni ni kuwajua unaowafanyia kampeni".
Kuwajua haimaanishi kuwajua kwa majina, la hasha, bali kitabia na kimazoea. Hii ni kwa sababu utahitaji kuwafikishia ujumbe utakaoeleweka na wao wawe tayari kuupokea halafu ndiyo waukubali.Na kama unataka kuwafikia Watanzania, basi achana na makala ndefu, hawatosoma.
Mitandao Jamii na Blogu nyingi zimejikita kwenye nadharia hii, Picha na ujumbe mfupi, na jinsi watu wanavyotazama au kuipenda (like) makala yako, ndivyo inavyozidi kuonekana. Kwe wengi wetu, hiki si kipindi tena cha kuongea logic, ni kipindi cha emmotion hivyo wagombea wanatakiwa kucheza na emottion za watu zenye kujenga.
Uwingi wa Muda
Ukweli usiopingika ni kuwa, wengi wa Watanzania wana muda mwingi wa kujadili mambo mbalimbali,(wengi hawana kazi, hasa vijana) hii inapelekea wengi wao kutokuwa busy kwenye shughuli wanazozifanya. Hivyo muda mwingi wamekuwa online wakitafuta habari, na kama vijana wanavyosema, uchaguzi ndiyo habari ya mujini.Na wao wameshaipata.
Hivyo, kama wewe ni mmoja wa wagombea basi utahitaji kujikita sana kushibisha njaa hii ya habari wanaoitafuta kwa aina tofautitofauti.
Uwezo wa kupambanua
Kwenye ulimwengu wa Tehama, kuna lundo la taarifa, taarifa hizi zipo za kujenga na kubomoa. Leo hii tumeshuhudia kwenye mitandao ya Whatsapp taarifa jinsi zinavyozunguka tena kwa kasi ya ajabu. Na nyingi ya taarifa hizi si za kweli au hazijengi. Leo hii mtu anaweza kuamua kutunga taarifa na ndani ya dakika tano imeshasambaa nchi nzima bila kujali uhalali au umuhimu wake.
Wengi wetu tumekuwa tukisambaza bila hata kumaliza kusoma au kutafakari. Hivyo, kwenye kipindi hiki cha ushaguzi tutegemee sana mafuriko ya habari zisizo na tija.
Nimewahi kuongea na Kada mmoja wa chama fulani, akaniambia, Chama chetu kina wio mpana hadi vijijini sehemu ambazo wengi wa washindani wetu hawawezi kufika. Sikuongea mengi, nilimuambia kitu kimoja tu, ila Teknolojia imefika, hata kwa uchache wake. Na watu wa huko, wengi hawana hata huo muda wa kupoteza kupambanua, wao huamini wanachokipokea. Na moja ya nyenzo kuu kwenye kampeni ni kuwa midomoni au akilini mwa watu.Wengi hupiga kura kwa mkumbo.
Tumeshaanza kuona matumizi makubwa ya Teknolojia,lakini, kampeni ni kama biashara, lazima uwe na uwezo wa kupima maendeleo na faida ya uwekezaji (ROI) ili kuepuka kuja kushangazwa siku ya mwisho. Kuna njia bora na thabiti za kutumia na kuongoza Teknolojia ili ije kuwa na manufaa makubwa kwenye kampeni yako. Tukutane kwenye makala ya pili nitakapoongelea matumizi bora ya Teknolojia kwenye Kampeni.
Post a Comment