Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Bernard Membe, amesema hatogombea
wadhifa wowote kwenye uchaguzi mkuu ujao nchini humo na kwamba anapanga
kujishughulisha na masuala yake ya kibinafsi.
Membe ambaye alikuwa akitafuta tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili
kuwania urais mwezi Oktoba lakini akashindwa kufikia lengo hilo, amesema
kuwa, hatotafuta nafasi ya ubunge katika jimbo lake la Mtama.
Hata hivyo amesema ataendelea kukiunga mkono chama chake cha CCM na
atampigia debe mgombea urais aliyeteuliwa na chama hicho, Bw. John
Magufuli.
Awali kulikuwa na tetesi kwamba Membe angegombea ubunge baada ya kukosa nafasi ya kuwania urais kwa tiketi ya CCM.
Huku hayo yakijiri, chama tawala nchini Tanzania kinaendelea kupata pigo
baada ya baadhi ya wabunge wake kutangaza kuwa hawatogombea tena nafasi
zao kupitia chama hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Mbunge wa Kahama, James Lembeli ni mwanachama wa CCM wa hivi karibuni
kutangaza kuwa hatatetea kiti chake kupitia chama hicho kwenye uchaguzi
wa Oktoba mwaka huu.
Tayari madiwani 20 wa CCM katika jimbo la Monduli wametangaza kuhamia
Chadema na kumtaka mbunge wao, Edward Lowassa kufuata mkondo huo.
CHANZO: TEHRAN KISWAHILI
Post a Comment