Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk.Rajabu Rutengwe kushoto akifurahia jambo na Mratibu wa Mkurabita Saraphia Mgembe.
Mkuu
wa Mkoa wa Morogoro Dk.Rajabu Rutengwe mwenye suti nyeusi akiongoza
kucheza ngoma ya Sangula ya wapogolo baada ya kuzindua utoaji wa hati
miliki za kimila chini ya Mkurabita wilayani Kilombero.
Baadhi ya wananchi mbalimbali wa wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro wakimsiliza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro .
Furaha ya hati ya miliki za kimila na Mkurabita.
Baadhi ya wananchi mbalimbali wa wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro wakiwa katika picha ya pamoja.
Na John Nditi, Morogoro
WAKUU wa wilaya ,
Wakurugenzi na Wenyeviti wa halmashauri ambazo zimenufaikana Mpango
wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (
MKURABITA), wametakiwa kuitumia fursa hiyo adhimu kuwapatia wananchi wao
maendeleo kwa kutumia rasilimali ardhi katika kukuza uchumi wa taifa letu.
Rai hiyo imetolewa na Mratibu wa
Mkuratiba nchini, Saraphia Mgembe, Juni 10, mwaka huu mjini Ifakara
wakati wa uzinduzi wa kimkoa wa utoaji wa hati miliki za kimila kwa
baadhi ya wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero, ambao mgeni
rasmi alikuwa mkuu wa mkoa huo, Dk Rajab Rutengwe.
Pamoja na hayo alisema ,katika
kupambana na upungufu wa fedha, Mkurabita imejiandaa kufanya majaribio ya
kuunda Mfuko wa Urasimishaji utakaoendeshwa kwa mfumo wa dhamana.
Kwa mujibu wa Mratibu hiyo kuwa,
utekelezaji wa urasimishaji ardhi mijini uliofanyika katika Manispaa ya
Morogoro umetoa hamasa ya kuujaribu mfuko wa urasimishaji kutokana na
uzoefu uliopatikana katika Manispaa hiyo.
Hata hivyo alisema katika mpango huo
kwa mkoa wa Morogoro ni halmashauri wilaya tatu ya Kilosa,
Mvomero na Kilombero zimenufaika kwa urasimishaji wa ardhi vijijini na
jumla mashamba 9,180 yamepimwa na yameandaliwa hati za hatimiliki
za kimila 7,837.
Pia alisema , Mkurabita umeendesha
zoezi la urasimishaji ardhi mijini katika Manispaa ya Morogoro kwenye
Kata ya Mbuyuni, Mlimani, Lukobe na Kihonda ambapo idadi ya wamiliki 222
walichangia uzalishaji wa viwanja 1,122 na hati 72 zimeandaliwa ambapo Manispaa
itaendelea kurasimisha mitaa mingine na kuzalisha viwanja vingine 5,660.
Hivyo alitoa rai kwa wananchi
walionufaika na mpango huo wazitumie hati hizo katika kujikwamua na
umaskini kwa kupata mikopo na mitaji kutoka taasisi zetu za fedha na mabenki.
Mbali na hayo, aliwataka Wakurugenzi
wa halmashauri ambazo kazi ya urasimishaji imefanyika sasa waiendeleze kazi
hoyo kwa kuhakikisha watendaji wao wanafanya kazi kwa uadilifu mkubwa .
“ Tunapofika hatua hii watu wengi
hawatofaitishi maofisa wa Mkurabita na wale wa halmashauri wanapokosa uadilifu
‘vitendo vya rushwa’ wananchi husema ni Mkurabita , wananchi mnapoona utata
wowote toeni taarifa ili maamuzi stahiki kwa watumishi wasiowaadilifu “ alisema
Mratibu huyo.
Naye Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk
Rutengwe, katika hotuba yake ya uzinduzi alisema hati hizo hazina ukomo
wake, ni dhamana ambayo taasisi za fedha zinazitambua na hivyo wananchi
walirasimishwa wanapata fursa ya mikopo na mitaji ya kujiendeleza.
Hata hivyo alisema, hati za kimika
zina manufaa makubwa kwa wananchi kwa kusaidia kuinua uchumi wao ,
kuimarisha usalama wa miliki ya ardhi na dhamana ya kupata mitaji ya mikipo
itakayoongeza uboreshaji wa shughuli za uzalishaji ili kujiongezea kipato.
“ Nawasihi wananchi wote
mliopokea hati hizi mzitumie kwa manufaa yenu na kuboresha maisha na si nyaraka
za kuficha na kuhifadhi tu” alisema Mkuu wa Mkoa.
Hata hivyo pamoja na kuupongeza
Mkurabita , mkuu huyo wa mkoa aliomba mpango huo uendeleze kujenga uwezo katika
halmashauri zilizobakia ya Gairo, Ulanga na Halmashauri ya wilaya ya Morogoro.
Post a Comment