Akizungumza jana baada ya ufunguzi wa mkutano wa 12 wa Shirikisho la Taasisi za Kupambana na Rushwa (SAFAC) kwa nchi zilizopo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete, Dk Hoseah alisema: “Takukuru tumeshafanya kazi yetu, lakini siwezi kusema chochote kwani Bunge ndilo litakalotoa majibu.”
Alipoulizwa iwapo, Bunge limekwishapokea ripoti hiyo, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema hakuwa na taarifa hizo.
Alisema Serikali kupitia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ndiyo iliahidi ingefanya uchunguzi na kuwasilisha taarifa ya uchunguzi huo bungeni, hivyo kama kuna mabadiliko yamefanyika taarifa hiyo ikawasilishwa kwa Spika au Kamati ya Bunge yeye hakuwa na taarifa hizo.
Hivi karibuni, Serikali baada ya kubanwa bungeni kuhusu uchotwaji wa Dola 200 milioni za Marekani katika akaunti ya escrow iliyopo Benki Kuu ya Tanzania(BoT), iliahidi kufanya uchunguzi kupitia Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Takukuru ili kubaini iwapo kulikuwa na ufisadi au la.
Fedha hizo ziliwekwa katika akaunti hiyo ili kusubiri suluhu ya mgogoro wa kibiashara baina na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) na Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL kuhusu bei ya uzalishaji umeme, lakini baadaye zikabainika kuchotwa kwa ruhusu ya baadhi ya viongozi wa Serikali.
Awali, Rais Kikwete alisema miradi mingi ya maendeleo nchini inajengwa chini ya kiwango na mingine inashindwa kukamilika kwa wakati kutokana na kukithiri kwa rushwa.
“Tunatakiwa kupambana na rushwa kwenye sekta zote, kuna sehemu moja nilitembelea kule kijijini kwetu Msoga, nikakuta kuna daraja limejengwa chini ya kiwango, lakini niligundua tatizo ni kutoa tenda kwa watu wasiokuwa na sifa kutokana na rushwa,” alisema Rais Kikwete. Chanzo:Mwananchi.
Post a Comment