Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Steven Nana katika mahojiano na mwandishi wa makala haya alisema katika mkutano wa Baraza la madiwani uliofanyika mwezi Juni mwaka huu walipendekeza shule zote ambazo zinatumia madarasa ya vibanda vilivyojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi kuvibomoa badala yake kujenga madarasa kwa kwa kutumia tofali za kuchoma.
"Hadi sasa madiwani katika kata zenye shule ambazo wanafunzi wanasomea vibanda vya nyasi wameitikio wito vibanda vimebomolewa na kujenga vyumba kwa tofali za kuchoma kwa mfano kata za Mgombasi, Luchiri na Msindo,kata ambayo bado hawajatekeleza ni uzembe wa usimamizi wa diwani husika, vibanda vya nyasi sio mazingira rafiki kwa kusomea wakati wa mvua vinavuja na kuathiri taaluma", alisisitiza.
Vibanda vya nyasi bado vinatumika
katika shule ya msingi Selous, hapa ni wanafunzi wa darasa la tano
wakisoma katika mazingira duni
Hata hivyo alisema wananchi waliamua kujenga vibanda vya nyasi kwa
lengo la kukabiliana na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa ambapo
alisema serikali ilitoa masharti magumu kwa wananchi kwa kuwataka
wajenge vyumba vya madarasa kwa kutumia kokoto kwenye msingi na kujenga
kwa theluji badala ya udongo jambo ambalo wananchi walishindwa kumudu
gharama za ujenzi.
Kutokana na hali hiyo mwenyekiti huyo anasema walipendekeza wananchi kujenga vyumba vya madarasa kwa udongo na tofali za kuchoma ambapo serikali iliahidi kuchangia vifaa vya kiwandani ambapo hadi sasa tayari wananchi wamefyatua tofali na fedha zitakapopatikana wanapewa ili kukamilisha ujenzi.
"Halmashauri yangu inakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha katika mwaka wa fedha wa 2012/2013 ilitengewa shilingi bilioni 16 lakini hadi kufikia mwezi huu Desemba ni asilimia 14 tu ya fedha ndiyo imefika kutoka TAMISEMI, fedha ikipatikana tutazipeleka katika shule kwa ajili ya kukamilisha ujenzi", alisema
Uchunguzi ambao umefanywa katika shule tatu za msingi kata ya Rwinga wilayani Namtumbo ambazo ni Rwinga, Kidugalo na Mkapa umebaini shule hizo zimefyatua tofali 80,000 kwa ajili ya kukabiliana na upungufu wa vyumba vya madarasa na nyumba za walimu.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mkapa
Hans Mwailima akionyesha nyumba ya mwalimu mkuu ambayo inajengwa ,shule
hiyo yenye walimu 11 haina nyumba hata moja ya mwalimu
Mwandishi
wa makala haya mwezi Mei mwaka huu alifanya uchunguzi katika kata ya
Rwinga na kubaini wanafunzi 500 katika shule hizo wanasomea kwenye
vibanda vilivyojengwa kwa miti na kuezekwa nyasi na wengine wanasoma
madarasa mawili katika chumba kimoja huku wamegeuziana migongo hali
ambayo imekuwa inaathiri taaluma katika shule hizo.
Kaimu mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kidugalo yenye wanafunzi 427 Getruda Turuka alisema katika shule hiyo tofali zaidi ya 20,000 zimefyatuliwa na kuchomwa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kukabiliana na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa ambapo shule hiyo ina vyumba vinne kati ya 13 vinavyohitajika.
Licha ya kwamba tofali kwa ajili ya ujenzi zimekamilika, hata hivyo serikali ya kijiji cha Kidugalo ilipanga kuanza ujenzi wa vyumba vya madarasa mapema, lakini uongozi wa Halmashauri uliwazuia kujenga kwa madai kuwa hakuna uwezo wa kuwasaidia vifaa vya viwandani ambavyo ni bati, misumari na saruji.
Walimu katika shule ya msingi
Kidugalo wakionyesha tofali ambazo zimeandaliwa kwa ajili ya ujenzi wa
vyumba viwili vya madarasa kwa lengo la kukabiliana na upungufu katika
shule hiyo
Said Juma na Tamimu Mwela ni wenyeviti wa vitongoji vya Lilunde na
Namwaya wanasema tofali zimekamilika na walitaka kuanza ujenzi
wamekwamishwa na Halmashauri kuwazuia kuanza ujenzi katika shule ya
msingi Kidugalo kwa madai kuwa Halmashauri hivi sasa haina fedha.
Katika shule ya msingi Mkapa ambayo haikuwa na nyumba hata moja ya mwalimu, hivi sasa kuna ujenzi wa nyumba ya mwalimu ambayo inaweza kuchukua familia mbili.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Hans Mwailima anasema kamati ya shule kwa kushirikiana na uongozi wa kijiji umeamua kuanza ujenzi wa nyumba ya mwalimu hali ambayo inaweza kupunguza tatizo la nyumba kwa walimu ambapo hivi sasa walimu wote 10 wanaofundisha katika shule hiyo akiwemo mwalimu mkuu wamepanga.
Hata hivyo amesema shule hiyo yenye wanafunzi 261 ina vyumba vinne tu kati ya mahitaji ya vyumba nane, madawati yaliopo ni 62 kati ya mahitaji ya madawati 106.
Katika shule ya msingi Rwinga yenye wanafunzi 436, kamati ya shule kwa kushirikiana na serikali ya kijiji wamefyatua tofali zaidi ya 25,000 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya kusomea ili kuepukana na wanafunzi 187 wa darasa la tatu na awali kusomea kwenye vibanda viwili vya nyasi vilivyojengwa katika shule hiyo.
Hawa ni wanafunzi katika shule ya
msingi Kidagulo ambao wanasafiri umbali mrefu kwa lengo la kutafuta maji
hali ambayo inaathiri taaluma
Mwalimu mkuu msaidizi katika shule hiyo Hamza Ngonyani amesema kamati
ya shule na serikali ya kijiji wamehamasisha michango ambapo kila mzazi
alitoa mchango wa shilingi 2000 na kufanikisha kufyatua na kuchoma
tofali ambazo zinaweza kujenga vyumba viwili vya madarasa.
Hata hivyo Ngonyani alibainisha kuwa changamoto kubwa iliyopo hivi sasa ni upatikanaji wa vifaa vya kiwandani zikiwemo bati na theluji kutoka Halmashauri ya wilaya ambayo imesema hivi sasa haina pesa za kusaidia kukamilisha ujenzi huo hivyo wameshauriwa kuacha kuanza ujenzi.
Katika shule ya msingi Selous hakuna hatua zozote ambazo zimechukuliwa kwa lengo la kukabiliana na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa ambapo shule hiyo ina wanafunzi zaidi ya 100 wanaosoma katika vibanda vya nyasi.
Baadhi ya walimu wanaofundisha katika shule hiyo ambao hawakutaka kutaja majina yao walidai kuwa baada ya vyombo vya habari kutoa habari kuhusiana na shule hiyo viongozi kutoka Halmashauri walifika,lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika zaidi ya vibanda vilivyopo kuviboresha kwa kuezeka nyasi ili kukabiliana na mvua za masika.
Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo yenye kata 14 ina shule za msingi 107 kati ya hizo shule 105 zinamilikiwa na serikali na shule mbili ni za watu binafsi na mashirika ya dini.
CREDIT: FIKRA PEVU
Post a Comment