Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Liberata Mulamula na Viongozi wa Baraza la Watanzania waishio Marekani (DICOTA) (hawapo pichani) mara baada ya kukutana nao Hotelini kwake kwa ajili ya kupata taarifa za maandalizi ya Mkutano wa Mwaka wa Baraza hilo atakaoufungua leo tarehe 03 Oktoba, 2014 mjini Durham, North Carolina. |
Balozi Mulamula, Viongozi wa DICOTA pamoja na Maafisa kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani wakimsikiliza Balozi Sefue (hayupo pichani) |
Na Mwandishi Wetu
Mkutano
wa Tano wa Mwaka wa Baraza la Watanzania waishio Marekani (DICOTA 2014)
utafunguliwa rasmi na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue tarehe
03 Oktoba, 2014 mjini Durham nchini Marekani.
Kaulimbiu
ya mkutano wa mwaka huu ni “Kuwawezesha Watanzania waishio ughaibuni
(Diasporas) kufikia Mabadiliko ya Kiuchumi na Kijamii Kule Waliko na Nyumbani”.
Mkutano
huu ambao utahudhuriwa na Watanzania kutoka Majimbo yote ya Marekani,
Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Kimarekani, unalenga kuwakutanisha
wadau hao na wajumbe kutoka Serikalini, Taasisi za Umma na Sekta Binafsi
ili kubadilishana mawazo na uzoefu na kuangalia namna bora ya kutumia
fursa na rasilimali zilizopo katika kukuza uchumi na kupata maendeleo
endelevu ya Jumuiya hiyo ya Diaspora na Taifa kwa ujumla.
Wakati wa Mkutano huu mada mbalimbali za ueleimishaji zitatolewa kwa
lengo la kueleza kwa kina fursa mbalimbali za uwekezaji, biashara na
utalii zilizopo nchini. Mada hizo ni pamoja na Uhamiaji na Uraia,
Mchakato wa Katiba mpya, Vitambulisho vya Uraia kwa Dispora, Mifuko ya
Hifadhi za Jamii na Pensheni, masuala ya Ardhi na Nyumba, umuhimu wa
Bandari ya Dar es Salaam kwa Diaspora, Usajili wa Makampuni na
upatikanaji wa Leseni za Biashara kwa Diaspora, masuala ya Kodi, Masoko
ya Mitaji na Hisa, masuala ya Nishati ya Mafuta na Gesi, Bima, Uwekezaji
katika Kilimo na mada kuhusu Uchumi na Fedha zinazotumwa kutoka nje na
Diaspora (Remittances).
Baraza
la DICOTA lilianzishwa rasmi mwaka 2008 na kikundi cha watu 30 wakiwa
na lengo la kushirikiana na Serikali na Sekta Binafsi katika kuleta
maendeleo endelevu kwa kutumia ujuzi, elimu, maarifa na mitaji
waliyoipata wakiwa ughaibuni. Baraza hilo linaongozwa na Dkt. Ndaga
Mwakabuta na Katibu wake ni Bi. Lyungai Mbilinyi.
Mkutano
wa kwanza wa DICOTA ulifanyika mwaka 2009 mjini Houston, Texas
ukifuatiwa na ule wa mwaka 2010 uliofanyika mjini Minneapolis,
Minnesota. Mkutano wa Tatu ulifanyika mwaka 2011 mjini Dulles, Virginia
ukifuatiwa na mkutano wa mwaka 2012 uliofanyika Chicago, Illinois.
Mbali
na Balozi Sefue, Viongozi Waandamizi wengine kutoka Serikalini
wanaohudhuria mkutano huu ni pamoja na Mhe. Liberata Mulamula, Balozi wa
Tanzania nchini Marekani, Bw. Alphayo Kidata, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bibi Rosemary Jairo, Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa na Bi. Susan Mzee, Mshauri wa masula ya
Diaspora kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.
Post a Comment