BASATA WAMPONGEZA DIAMOND NA WASANII WALIOTEULIWA TUZO ZA AFRIMA
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kama msimamizi na mratibu wa sekta ya Sanaa nchini linapenda kutoa pongezi za dhati kwa Msanii wa muziki wa kizazi kipya Nassib Abdul maarufu kama Diamond kwa kushinda tuzo ya Msanii bora wa mwezi wa kituo cha televisheni cha MTV Base kinachorusha matangazo yake kutoka Afrika Kusini na kuyafikia maeneo mengi duniani.
Aidha, Baraza linampongeza msanii huyu na wenzake Peter Msechu na Vannessa Mdee kwa kuchaguliwa kushindania tuzo mbalimbali katika tuzo za "All Africa Music" (Afrima) ambapo nyimbo zaidi ya 2025 kutoka kwa wasanii mbalimbali barani Afrika zinatarajiwa kushindanishwa na washindi kupatikana.
Kuteuliwa na kushinda kwa Wasanii wa Tanzania katika tuzo mbalimbali za Afrika na duniani ni ishara kwamba muziki wetu unakubalika ndani na nje ya Tanzania.
Baraza linatoa wito kwa wasanii na wadau wote wa muziki kuzidisha ubunifu, bidii na weledi katika kazi wanazozifanya ili wasanii wengi zaidi waweze kuchomoza katika tuzo na majukwaa mbalimbali ya kimataifa kwa lengo la kulitangaza na kukuza soko la kazi zao kimataifa.
Ni matumaini ya Baraza kwamba wasanii wataendelea kutambua umuhimu wa kufuata sheria, kanuni na taratibu za kutambuliwa na Serikali.
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini
Godfrey Mngereza
KAIMU KATIBU MTENDAJI
Post a Comment