WAJUKUU wa marehemu Sabina Ngalu (77) wameibua kutuko makaburini
kufuatia kuzama ndani ya kaburi la marehemu huyo na kugoma kutoka
wakidai kwamba mpaka walipwe shilingi laki moja (100,000), Uwazi lina
mkanda mzima.
Wajukuu wa bibi huyo wakiwa kaburini. Tukio hilo la aina yake
lilijiri mwishoni mwa wiki iliyopita katika Kitongoji cha Nyamwanza Kata
ya Sima wilayani Sengerema mkoani Mwanza muda mfupi baada ya mwili wa
marehemu kuwasili eneo la mazishi kwenye shamba lake ukitokea Kanisa la
Roman Katoliki Parokia ya Yesu Kristo Mfalme la mjini Sengerema.
Sababu za wajukuu hao kung’ang’ania ndani ya kaburi hilo walitaka
wapewe ng’ombe mmoja au pesa hizo taslimu kwa mjibu wa mila na desturi
za kabila la Kisukuma jambo ambalo lilipingwa na baadhi ya wanandugu
waliodai mila hizo zilipitwa na wakati.
Kufuatia wajukuu hao kuendelea kugomea ndani ya kaburi, kaka wa
marehemu, Enosi Ngalu alikwenda kukata fimbo na kuwashukia kisha
kuwacharaza viboko wote huku nao wakisisitiza hawatoki mpamka
‘kieleweke’.
Padri na wananchi wakiwa makaburini. Baadhi ya wajukuu walioonja joto
la jiwe ya kuchapwa viboko ni Andrea Mabula, Sabina Bukuru, Johari
Bukuru, Asha Bukuru, Faida Bukuru, Yuves Petro, Semeni na kiongozi wao,
Enos Ntilaga.
Kitendo cha wajukuu hao kuendelea kugoma kutoka kaburini kilimchefua
Padri Nicodemus Mayalla ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Yesu Kristo
Mfalme, Sengerema ambaye aliamua kuondoka eneo la maziko huku
akiwataarifu polisi kuhusiana na vurugu hizo.
Kufuatia hali hiyo, mmoja wa waombolezaji alizama mfukoni na kutoa
kiasi hicho cha pesa na kuwapa ndipo walipokubali kutoka dani ya kaburi
hilo ili mazishi yaendelee.
Ili kuonesha alikerwa na kitendo hicho, Padri Mayalla ambaye kwa
wakati huo alikuwa amewekwa chini na baadhi ya ndugu wakimsihi kutosusia
mazishi hayo, aligoma kurejea kaburini kuongoza ibada ya mazishi.
Jeneza lenye mwili wa bibi huyo likishushwa kaburini. Baada ya vuta
nikuvute, hatimaye Padri Mayalla alikubali kuendelea na ibada lakini
aliwataka wajukuu hao kurudisha pesa waliyochukua na kuwaomba radhi wana
mtaa huo na ndipo yeye aweze kurudi kaburini.
Wajukuu hao waliitwa mbele ya padri huyo na mbele ya wana mtaa,
wakaomba samahani ikiwa ni pamoja na kurudisha kitita hicho cha pesa
paroko huyo naye akarejea kaburini na kuongoza ibada ya mazishi.
Hata hivyo, wakati ibada ikiendelea polisi zaidi ya wanne kutoka
Kituo cha Polisi Sengerema wakiwa na bunduki aina ya Sub Machine Gun
(SMG) na mabomu ya machozi walifika eneo la tukio ili kuhakikisha amani
na utulivu vinatawala.
Polisi akiwa eneo la tukio. Cha kushangaza, saa baada ya kutoka
makaburini, wajukuu hao waliwahi nyumbani kwa marehemu, Mtaa wa Mlimani,
Kata ya Nyatukala wilayani Sengerema na kuanzisha timbwili jingine kwa
kuficha chakula na vyombo vya kupakulia wakidai warudishiwe pesa yao
waliyoirejesha makaburini kwa shinikizo la baba paroko.
Baada ya timbwili hilo kukolea, mmoja wa wafiwa alizama mfukoni na
kutoa shilingi laki moja na kuwakabidhi wajukuu hao ambao walirudisha
chakula jikoni na taratibu za waombolezaji kupata chakula ziliendelea.
Post a Comment