HALIMA MDEE ALALA KATIKA GEREZA LA SEGEREA JIJINI DAR ES SALAAM BAADA YA KUKOSA DHAMANA
MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (35) na wanachama wenzake wanane wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana walipelekwa rumande baada ya kushindwa kukamilisha taratibu za dhamana katika kesi inayowakabili ya kutotii amri halali ya Polisi na kufanya mkusanyiko bila kibali.
Mdee ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) pamoja na wanachama hao, walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Wengine waliosomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda ni Rose Moshi (45) Mkazi wa Kinondoni B, Renina Peter maarufu kama Lufyagila mkazi wa Kinondoni Mkwajuni, Anna Linjewile (48) mkazi wa Mbezi Luis na Mwanne Kassim (32) mkazi wa Pugu Kajiungeni.
Wengine ni, Sophia Fangel (28) mkazi wa Mbezi Beach, Edward Julius (25) mkazi wa Msasani, Martha Mtiko (27) mkazi wa Mikocheni 'A' na Beatu Mmari (35) mkazi wa Kinondoni Mkwajuni.
Mawakili wa Serikali, Bernard Kongola, Salum Mohamed na Hellen Mushi wakisaidiana kusoma mashitaka, walidai Oktoba 4, mwaka huu, katika mtaa wa Ufipa, bila kuwa na uhalali washitakiwa hao walikiuka amri halali ya kutawanyika iliyotolewa na Mrakibu wa Polisi (SP) Emmanuel Tillf kwa niaba ya Jeshi la Polisi.
Katika mashitaka mengine inadaiwa siku hiyo katika eneo hilo, kwa pamoja, walifanya mkusanyiko usio halali kwa lengo la kutembea kwenda Ofisi ya Rais.
Washitakiwa walikana mashitaka. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 21 mwaka huu itakapotajwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.
Hakimu Kaluyenda alisema watapata dhamana endapo kila mmoja atasaini hati ya dhamana ya Sh milioni moja, kuwa na wadhamini wawili, mmoja kati yao awe anafanyakazi katika taasisi inayotambulika kisheria atakayewasilisha barua kutoka kwa mwajiri na kitambulisho cha kazi.
Upande wa Jamhuri uliomba Mahakama ikague nyaraka za dhamana zilizowasilishwa na wadhamini. Wote walirudishwa rumande hadi leo kwa ajili ya kukamilisha taratibu za dhamana.
Waliondolewa mahakamani hapo saa 10:45 jioni wakiwa kwenye magari manne yaliyokuwa na askari zaidi ya 30 pamoja na gari la maji ya kuwasha na kupelekwa katika Gereza la Segerea.HABARILEO
Post a Comment