PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: Dampo la Pugu Kinyamwezi hatari kwa afya ya wakazi maeneo hayo
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
WAKAZI wanaoishi kandokando ya dampo kunakomwagwa taka zinazotoka katika Manispaa za jiji la Dar es Salaam katika eneo la Pugu Kinyamwezi,...



WAKAZI wanaoishi kandokando ya dampo kunakomwagwa taka zinazotoka katika Manispaa za jiji la Dar es Salaam katika eneo la Pugu Kinyamwezi, wako hatarini kukumbwa na maradhi mbalimbali kutokana na harufu kali inayotoka kwenye dampo hilo na kusababisha kuzagaa kwa inzi.

Licha ya kuwepo kwa hali hiyo, FikraPevu imeshuhudia Huduma za Afya zikiendelea kutolewa katika Zahanati iliyopo kandokando mwa dampo hilo, ijulikanayo kama Zahanati ya Ananda Marga pamoja na shule ya awali ya Ananda Marga bila kujali harufu mbaya na kuzagaa kwa inzi hao.



Zahanati inayohudumia mamia ya wakazi wa eneo hilo inayokadiriwa kuwa umbali wa takribani hatua 15 kutoka ukingo wa dampo hilo



Katika mahojiano ya FikraPevu na wagonjwa waliokuwa wakisubiri kupata huduma katika zahanati hiyo leo Oktoba 22, 2014, wameeleza kuwa adha wanayoipata ni pamoja na kuathiriwa na harufu mbaya pindi wanapofika katika eneo hilo kwa ajili ya kupata huduma za kijamii pamoja na kukutana na inzi.

“Wakati mwingine inatuwia vigumu kupata huduma; inabidi turudi majumbani, hii harufu inatukera sana unakuta wakati mwingine inzi ni wengi unapokula chakula huoni raha yake na ndani hakukaliki” alieleza mmoja wa wagonjwa hao.

Sophina Abel, mkazi wa eneo hilo ameeleza kuwa mvua ikianza kunyesha hali inazidi kuwa mbaya zaidi na kwamba hali hiyo inahatarisha afya za familia zenye watoto wadogo wanaozungukwa na dampo hilo kwa kuugua ugonjwa wa pumu na magonjwa mengine.



Deogratius Ako, mkazi wa Majohe Kichangani, anasema kumekuwepo na mgogoro wa muda mrefu baina ya Halmashauri ya Jiji na wakazi wanaozunguka dampo hilo, wakitaka lihamishwe na kwamba zoezi hilo limekuwa gumu kwani pamoja na kulijadili kwa pamoja na viongozi wa maeneo husika limeonekana kuwa gumu kwani wanapigwa mabomu ya machozi na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na mgambo wa jiji pale wanapoandamana kila mara kushinikiza kuhamishwa kwa dampo hilo.

Wakazi wa Gongo la Mboto wakizungumzia kadhia hiyo, wameeleza kuwa Serikali inatakiwa kutengeneza teknolojia ya kibaiolojia ya kutandaza ardhini taka zote kwa ajili ya kudhibiti maji taka na taka ngumu na kwamba tatizo la baadhi ya watu huokota taka ambazo ni mifuko ya plastiki yenye kemikali na kurudisha mtaani, hawalitilii maanani ikiwa kuna kuhatarisha usalama wa afya zao.

“Tatizo la maji taka na taka ngumu limekuwa changamoto katika maeneo yetu hususani tuliopo mijini na kuathiri mazingira kwa kiwango kikubwa na moja ya athari ya maji taka inavyoachwa ikaingia kwenye mifereji na mito inaua viumbe hai”.

Wala mabaki ya vyakula

Katika hali ya kushangaza, FikraPevu imeshuhudia vijana zaidi ya 100 wakiwa wametawanyika katika maeneo tofauti kwenye dampo hilo wakitafuta mabaki ya vyakula yanayopelekwa kwenye dampo hilo kwa ajili ya kula na kunywa vinywaji mbalimbali bila kuwa na hofu ya kuugua magonjwa ya aina yoyote.

“Kama unavyotuona hapa tunakula kila kinachofaa kula na hatuumwi kwasababu Mungu anatujua kuwa ndio sehemu yetu tunayopatia chakula, mimi nipo hapa huu ni mwaka wa pili siumwi wala nini, tunalala hapa na kuamkia hapa pia wakati mwingine tunakusanya chupa za maji zilizotumika na sponji za madogoro tunajaza kwenye viroba na kuuzia watu wanaokuja kununua kuanzia shilingi 150 kwa kilo moja”.

Wahudumu katika Zahanati pamoja na shule jirani, wamenukuliwa na FikraPevu wakieleza kuwa dampo hilo halikuwepo wakati huduma hizo zikianza na kwamba mmiliki wa zahanati na shule hiyo hana shida na dampo hilo bali analilia kadhia wanayoipata wenyeji wa eneo husika.



Mtafiti Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu Cha Ardhi jijini Dar es Salaam, Dk. Shaban Mgana, amesema kupitia teknolojia ya kibaiolojia taka ngumu au maji taka yanayozalishwa majumbani yanaweza kutumika kama mboji na gesi asilia ya kupikia majumbani na serikali kuweza kuondokana na tatizo la taka ngumu.

Ofisa Uhusiano wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Gaston Makwembe, amesema serikali haiwezi kulaumiwa wala namna ya kuwasaidia wakazi wa karibu na dampo hilo kwani wanafunika taka kwa kifusi na kupuliza dawa jambo ambalo linakinzana na hali ilivyo kwa sasa.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imekuwa ikisisitiza wananchi kuweka mazingira safi hususani yanayowazunguka lakini katika eneo hilo hali inaonekana kuwa tofauti kutokana na harufu mbaya iliyopo inayohatarisha afya za wakazi hao.

Tafiti zinaonyesha kuwa tatizo la taka ngumu lililopo nchini, limekuwa likichangia kwa kiasi kikubwa magonjwa ya milipuko ikiwemo kuhara damu na kipindupindu na kupelekea vifo vya wananchi kutokana na kutokuwa na mfumo bora na rahisi wa kuweza kuwafikia wananchi katika maeneo yao.



Taka ngumu zikimwagwa katika dampo hilo na magari ya Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top