PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: TANZANIA YASHINDWA KUFIKIA MALENGO YA MILLENIA SEKTA YA AFYA
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
SERIKALI ya Tanzania imeshindwa kukabiliana na tatizo la vifo vya mama na mtoto wenye umri chini ya miaka mitano, kutokana na uzazi un...




SERIKALI ya Tanzania imeshindwa kukabiliana na tatizo la vifo vya mama na mtoto wenye umri chini ya miaka mitano, kutokana na uzazi unaofanyika chini ya kiwango bila kuboresha miundombinu ya barabara, majengo, vitendea kazi vya kitaaluma pamoja na kushindwa kufikia malengo ya milenia namba nne na tano ifikapo 2015 ikiwa imesalia miezi kadhaa bila kukamilika kwa malengo hayo.

Takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa wanawake wengi katika nchi za Afrika ikiwamo Tanzania, hupoteza maisha kutokana na tatizo la ujauzito ambapo inakadiriwa kuwa wanawake 3,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na matatizo yatokanayo na uzazi ukiwemo ugonjwa ya fistula huku wanawake 19 wakifa kila siku nchini kutokana na matatizo hayo.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Bagamoyo mkoani Pwani, Dkt. Masidia Rotahiwa, ametaja matatizo ya upungufu wa watumishi wa idara ya afya, vifaa tiba na bajeti ndogo katika hospitali hiyo kuwa vinachangia kuzorotesha idara ya afya na kuainisha tatizo la vifo vya wajawazito wilayani humo kuwa vinafikia wastani wa vifo 68 kwa kila wanawake laki moja, wanaojifungulia katika Hospitali hiyo.

Ameitaka serikali kufuatilia takwimu za wagonjwa badala ya wakazi wa eneo husika ili kutatua tatizo hilo, kwa kuainisha bajeti ya idara yake na kutengewa bajeti ya takwimu ya watu 40,000 ambapo amesema Ofisi yake inatoa huduma hiyo kwa zaidi ya watu elfu sitini kila mwaka.

“Changamoto kubwa ni ya kuongezeka kwa tatizo la vifo vya wanawake wakati wa kujifungua kutokana na ukosefu wa damu salama na ya uhakika kwa wakati muafaka, lakini tuna mpango wa kujenga vyumba vya upasuaji katika maeneo ya Chalinze na Miono”

Tafiti na takwimu

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kati ya wanawake 19 wanaokufa kila siku nchini wakati wa kujifungua imebainika kuwa zaidi ya watoto 700 hubaki katika hali ngumu ya maisha huku wakikabiliwa na magonjwa yanayojitokeza wakati wa uzazi.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali hapa nchini, Dkt. Donan Mmbando, amesema serikali imeanza kuandaa rasimu ili kuongeza kasi ya kupunguza vifo, kwa kujenga vyumba vya upasuaji kwa kuanzia mikoa ya Pwani na Dodoma na kuwa suala la kufikia malengo ya milenia kwa sasa serikali haiwezi kutoa taarifa ya moja kwa moja kabla ya kumalizika kwa muda wa malengo hayo.

Tafiti zinaonyesha kuwa Tanzania bado haifanyi vizuri katika kupunguza vifo vya wajawazito, kwani bado akina mama 454, kati ya 100,000, wanapoteza maisha, licha ya serikali kuweka suala hilo katika mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), ambalo hadi sasa taarifa zinaonyesha kutofikia malengo na kuwa katika utekelezaji wake kila halmashauri ilitakiwa kuwa na vyumba vya upasuaji katika vituo vyake vya afya ambavyo hadi sasa katika maeneo hayo imeripotiwa kutofikia lengo hilo.

Awali Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete, Mei 31, 2014 aliwahi alikaririwa katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano kuhusu afya ya mama na mtoto uliofanyika mjini Toronto, Canada akisema Tanzania imefanikisha lengo la kupunguza vifo vya watoto pamoja na mapambano dhidi ya malaria na ukimwi kama yalivyoainishwa na Umoja wa Mataifa kwa juhudi za serikali.

Pamoja na mambo mengine Rais Kikwete, alipokea msaada wa dola za Marekani 3.5 bilioni ambazo ni zaidi ya Shilingi 5.6 trilioni kutoka kwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Stephen Harper, kwa lengo la kuimarisha lishe na kupunguza magonjwa huku akisema kuwa serikali imeweka sera nzuri za afya na kuboresha huduma za afya na uzazi nchini kwa kuongeza bajeti ya afya kutoka shilingi 271 bilioni kwa mwaka 2007 hadi shilingi trillion 1.4 kwa mwaka 2013, ambapo licha ya kutengwa kwa bajeti hiyo vifo hivyo vinaendelea kutokea katika maeneo mablimbali nchini.

“Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa kiwango kikubwa kwai hapo awali vilikuwa 115 kwa 1,000 na vya watoto wachanga chini ya miaka mitano vilikuwa 191 kwa 1,000 lakini kwa sasa vifo hivyo vimefikia watoto 21 kwa 1,000 na watoto chini ya miaka mitano vifo vimepungua hadi kufikia 54 kwa 1,000”.

Utafiti uliofanywa na taasisi ya Tanzania Knowledge Network hivi karibuni imeonyesha kuwa vifo hivyo vinatokana na idadi ndogo ya watoa huduma katika vituo vya afya, kukithiri kwa rushwa, umaskini, na uongozi mbaya kutokana na gharama za usafiri, gharama za huduma kinyume cha sheria na kutokuwa na vituo vya kutosha vyenye huduma za dharura.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika lisilo la kiserikali la SIKIKA ya mwaka 2008 ilisema mpango wa serikali uliolenga kupungaza vifo vya mama wajawazito kutoka 578 mpaka 265 kwa vizazi hai 100,000 na vifo vya watoto wachanga kutoka 32 hadi 19 kwa kila vizazi hai 1000 ifikapo mwaka 2010, iligundua kuwa maeneo muhimu yaliyoainishwa katika mpango huo ikiwa ni pamoja na kuelimisha jamii kuhusu vidokezo vya hatari vinapotokea pamoja na kuchukua hatua za dharura kuokoa maisha ya mama, ambapo hadi mwaka 2010 asilimia kubwa ya mpango huo ulikuwa haijafanikiwa.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top