WAZIRI wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Mansour Yusuph Himid, amefikishwa Mahakamani Zanzibar, akishitakiwa kumiliki bastola na bunduki zenye risasi nyingi zaidi ya kiwango kinachotakiwa.
Habari kutoka Zanzibar zinaeleza kwamba Mansour ambaye aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi ( CCM ) kabla ya kuvuliwa uanachama kwa sasa amejiunga na Chama cha Wananchi (CUF) na anatajwa kuweza kuwania uongozi kupitia chama hicho.
Imeelezwa kwamba Mansour amefikishwa mahakamani Jumanne Agosti 5, 2014 mjini Zanzibar akisomewa mashitaka matatu ikiwemo shitaka la kumiliki silaha za moto kinyume cha sheria namba 34 kifungu cha kwanza na cha pili, ambayo inaeleza wazi kuwa ni marufuku mtu kumiliki silaha aina ya bastola akiwa Zanzibar.
Bastola aliyokutwa nayo Mansour ilikutwa ikiwa na risasi 295 wakati kisheria kwa wamiliki wa upande wa Tanzania bara anatakiwa kuwa na risasi 25 tu. Kibali cha bastola hakitambuliwi Zanzibar.
Mansour pia ameshitakiwa kwa kukutwa na bunduki aina ya Short Gun ikiwa na risasi 112 ikiwa kiwango cha juu cha risasi zinazotakiwa kisheria. Kisheria mmiliki wa bunduki kubwa anatakiwa kuwa na risasi zisizozidi 50.
Mtuhumiwa alikana mashitaka yote na Hakimu Hamisi Ramadhani Abdalah Shaban alisema ya kuwa kosa hilo kisheria halina dhamana na mtuhumiwa akirudishwa rumande hadi Agosti 18, 2014 kesi hiyo itakapotajwa tena.
Taarifa kutoka Mahakamani hapo zinaeleza kuwa mawakili wa upande wa utetezi baada ya mteja wao kusomewa mashtaka hayo hawakupinga uamuzi huo.
Hata hivyo nje ya mahakama wamesema wanampango wa kwenda katika Mahakama Kuu Zanzibar kudai dhamana ya mteja wao.
Kukamatwa kwa Mansour
Mansour, ambaye ni mtoto wa muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, Brigedia Jenerali Yusuph Himid, alikamatwa nyumbani kwake Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar, baada ya kufanyiwa upekuzi mkali na kikosi cha upelelezi.
Mansour alikamatwa pia na Kompyuta mpakato (laptop), pamoja na vifaa vya mawasiliano ambavyo vinaendelea kufanyiwa uchunguzi.
Mansour alikuwa mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki mjini Zanzibar na awali aliwahi kuwa Waziri katika serikali ya Rais Amani Karume na baadae DK. Ali Mohamed Shein.
Mansour ni mume wa dada wa Rais Mstaafu Karume kama ambavyo Karume ni mume wa dada yake Mansour.
Post a Comment