Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu duniani (UNFPA), Dkt Natalia Kanem akizungumza wakati wa maadhimisho hayo ya siku ya kimataifa ya vijana duniani kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Kushoto ni Mgeni Rasmi kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Bibi Venerose Mtenga na kulia ni Mtaalamu wa Programu za Vijana kutoka UNFPA, Tausi Hassan.
*********
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI Kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo imeahidi kukuza na kuboresha misingi ya kuwashirikisha vijana katika utekelezaji wa sera mbalimbali, programu na mikakati ya maendeleo.
Akisoma hotuba kwa niaba ya Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Bibi Sihaba Nkinga, wakati wa maadhimisho ya siku ya vijana duniani kwenye viwanja vya Chuo Kikuu Dar es Salaam, Bibi Venerose Mtenga amesema kwamba lengo la kuwashirikisha vijan ni kuhakikisha kuwa sauti zao zinasikika na kufanyiwa kazi.
“Katika kutekeleza eneo hili Tanzania inalenga kuweka fursa zitakazowawezesha vijana kukuza utaalamu na ujuzi utakaowawezesha kufanikiwa katika kipindi cha mpito kutoka ujana kwenda katika utu mzima,” amesema Bibi Mtenga.
Amesema kwamba Tanzania kama sehemu ya dunia inatambua changamoto maalum zinazowakabili vijana walioko katika mazingira hatarishi pamoja na umuhimu wa kuhakikisha kuwa vijana wanahusishwa kikamilifu katika malengo ya maendeleo.
Bi Mtenga aliongeza Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa karibu na vijana pamoja na wadau wa maendeleo ili kuunga mkono programu za elimu ya afya kwa vijana walioko ndani na nje ya shule.
Alilisitiza kwamba Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo wataendelea kuunga mkono taasisi za mafunzo rasmi na zisizo rasmi ili kukuza uwezo na uelewa miongoni mwao katika masuala ya afya ya akili na mwili kwa ujumla.
“siku ya vijana duniani inatambua na kuthamini kuwa kipindi cha ujana kinaambatana na mabadiliko makubwa na ya haraka na safari ya kutoka utotoni kufikia utu mzima,”
“Safari hiyo inaweza kuwa ngumu na yenye changamoto nyingi na hivyo kuhitaji utulivu na ukomavu wa akili, hapa Tanzania, kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya vijana, kijana ni mtu yeyote mwenye umri kati ya miaka 15 hadi 35,” aliongeza.
Amesema kwamba katika takwimu za kitaifa hapa nchini nusu ya idadi ya watu ni vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Mgeni Rasmi kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Bibi Venerose Mtenga akizungumza wakati wa maadhimisho hayo ya siku ya kimataifa ya vijana duniani, kushoto kwake, ni Mwakilishi wa UNFPA, Dkt. Natalia Kanem.
Bibi Mtenga aliendelea kusema kwamba msisitizo mkubwa unawekwa katika kuhakikisha vijana wanakuwa na fikra chanya ambazo ni za kimaendeleo na zinazoleta mabadiliko chanya kwa jamii.
Kwa Upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu duniani (UNFPA), Dkt. Natalia Kanem amesema kwamba siku ya vijana duniani ni nafasi nyingine kwa vijana kukutana pamoja na kujadiliana matatizo na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.
Amesema kwamba vijana kwa kushirikiana na makundi mbalimbali ya kitaifa na kimataifa katika kupambana na changamoto za matumizi ya pombe kupita kiasi, dawa za kulevya na mimba za utotoni.
“kwa pamoja serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na mashirika ya kimataifa wana wajibu wa kushirikiana na vijana katika kuwasaidia kufikia malengo yao mbalimbali katika harakati za kujiletea maendeleo,” amesema Dkt. Kanem.
Dkt Kanem aliongeza kwamba ni muhimu kwa vijana kutambua kwamba bila kuwa na afya nzuri ya akili ni vigumu kupiga hatua za kimaendeleo na kuondokana na umaskini wa kipato.
Amesema kwamba katika mkutano unaokuja wa viongozi duniani watatumia nafasi hiyo kuwakumbusha viongozi wa dunia umuhimu wa kuwekeza kwa vijana kama taifa la kesho.
Dkt.Kanem alifafanua umuhimu wa vijana na jamiii kwa ujumla kutumia mitandao ya kijamii katika kupashana habari za afya ya uzazi na mambo yanayowahusu vijana kwa ujumla.
Wakati huo huo, Katika mashindano ya mpira wa kikapu timu zilizoshiriki ni timu saba kati ya hizo tano ni za wanaume na pili za wasichana.
Post a Comment