Kitendo cha Bunge Maalumu la Katiba kukusanya maoni ya makundi na wananchi mbalimbali, kimepokewa kwa hisia tofauti, baadhi ya wasomi wakisema ni kinyume cha sheria na kuonyesha kutapatapa huku Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba akisema linafanya kazi ambayo tayari tume yake ilishaifanya.
Hata hivyo, Katibu wa
Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad amesema litaendelea kupokea mapendekezo
kutoka kwa watu na makundi mbalimbali hadi hapo litakapohitimisha kazi
yake.
Kwa muda sasa,
wawakilishi wa taasisi mbalimbali wamekuwa wakifika Dodoma kuwasilisha
mapendekezo yao wakitaka yazingatiwe kwenye Katiba Mpya kwa maelezo ya
kutoonekana katika rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Suala hilo limezua
mjadala hasa katika mitandao ya kijamii ambako watu mbalimbali wamekuwa
wakihoji sababu za Bunge hilo kufanya kile kinachotafsiriwa kuwa ni
‘kukusanya maoni’, kazi ambayo tayari ilishafanywa na Tume ya Mabadiliko
ya Katiba.
Akitetea hoja hiyo,
Hamad alitetea akisema wananchi, watu au taasisi zinazotoa mapendekezo
yao zinashirikiana na wabunge katika mchakato wa kile kinachoendelea
bungeni hivi sasa.
“Tutaendelea kupokea
maoni ya wananchi kwa sababu na sisi tunaendelea kujadili, kwa hiyo
kadri makundi yatakavyoleta maoni yao, tutayapokea na kuyapitisha kwenye
mchakato wa kuyawezesha kuzingatiwa kama yataonekana yanafaa,” alisema
Hamad.
Warioba na wasomi
Akizungumzia hatua hiyo,
Jaji Warioba aliponda kitendo cha kukusanywa upya kwa maoni hayo
akisema yalishachukuliwa na Tume yake na kuingizwa katika Rasimu ya
Katiba.
“Nyaraka zote za maoni,
yakiwamo ya makundi hayo tuliziwasilisha, sasa wanakusanya maoni mapya
ili iweje? Wanatakiwa kufuata maoni ya wananchi na si ya makundi na kama
wanafanya hivyo basi maoni ya makundi hayo yakusanywe hadharani ili
wananchi wayasikie ili nao waweze kuchangia,” alisema jana.
Alitolea mfano wa maoni
yaliyotolewa na Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT), kwamba ni
makosa kuchukua maoni hayo na kuyaacha yaliyotolewa nawananchi.
Post a Comment