Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis (PICHANI)amekubali kumuondolea sakramenti ya upadri, Raymond Mosha wa Jimbo Katoliki la Moshi ikiwa ni miaka 20 tangu padri huyo aombe kuachana na daraja hilo.
Barua
ya uamuzi wa Papa Francis ilisomwa juzi katika parokia na vigango vyote
vya Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi katika ibada zilizofanyika katika
makanisa ya jimbo hilo.
Miongoni
mwa parokia ambazo barua hiyo ilisomwa ni Karanga ambako Paroko wake,
John Matumaini alitoa tangazo hilo katika ibada zote. Uamuzi huo ambao
ni nadra kutolewa na Papa, unamaanisha kuwa sasa padri huyo yuko huru
kuoa na kuwa na familia.
Hata
hivyo, wakati uamuzi huo ukitangazwa rasmi juzi, tayari Padri Mosha
ambaye ni profesa wa falsafa na maadili katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela Arusha, ana mke na watoto watatu ambao kwa sasa wako vyuo vikuu.
Padri Mosha alisema aliandika barua kuomba kuondolewa daraja hilo mwaka 1994 kabla ya uamuzi kutolewa juzi.
Katika
orodha ya mapadre 185 wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi iliyopo katika
tovuti ya jimbo hilo, jina la Padri Mosha linaonekana likiwa ni namba
23.
Akizungumzia
hatua hiyo, Padri Mosha alisema: “Ninafurahi kufunguliwa kifugo hiki na
hii itanifanya niishi kama Mkristo. Kwa vile hawajaniondolea sifa ya
kutoa huduma kama vile ibada za mazishi, sakramenti ya mwisho na
ubatizo, nitaendelea kutoa kwa wahitaji kwa sababu ninaupenda ukristo.
“Nashukuru
sasa nimekuwa muumini wa kawaida nitaweza kufunga ndoa kanisani kwa
kuwa nilikuwa nimefunga ndoa ya kisheria tu kwa DC.”
Kuhusu
kwa nini aliamua kuacha upadri, Profesa Mosha alisema ni baada ya
kufanya kazi hiyo kwa miaka 20 na akaona ipo haja ya kuwa na familia
lakini kanisa lilikuwa haliruhusu.
“Sasa
kwa kuwa kanisa haliruhusu mapadri kuoa ndiyo maana nikaamua kuandika
barua ambayo hata hivyo, imechukua muda mrefu kujibiwa na tayari nina
watoto watatu wako chuo kikuu.
Post a Comment