PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: MWANAFUNZI DARASA LA 3 ALIWA NA MBWA HADI KUFA pitia hapa habari hiyo ya kusikitisha
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
MWANAFUNZI wa darasa la tatu ka...



MWANAFUNZI wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Ludewa iliyopo katika mkoa wa Njombe, Ibrahim Faraja (9), amekufa kwa kuliwa baadhi ya nyama za mwili wake na Mbwa wawili wanaosadikika kuwa na ugonjwa wa kichaa cha Mbwa kwa kukosa chakula kwa muda mrefu.
Taarifa zinasema tukio hilo limetokea Agosti 8, saa saba mchana katika eneo la Ikulu, ambapo marehemu akiwa pamoja na wenzake wawili wasiotambuliwa majina mara moja walikuwa wakipita njia karibu na nyumba ya, Bosco Lingalangala, kwenda kuchuma matunda aina ya mapera ndipo walipoanza kukimbizwa na Mbwa hao ambapo wenzake wawili walifanikiwa kukimbia na yeye kuanza kuburuzwa na Mbwa kichakani.
Katika tukio hilo mashuhuda na wakazi wa Kitongoji cha Ibani katika kata ya Ludewa, wamefafanua kuwa wakiwa ndani walisikia kelele za watoto jirani na eneo wanaloishi huku wakimwita mwenzao marehemu bila mafanikio.
Padri
Mchungaji akiendesha ibada ya mazishi ya Marehemu
Taarifa kutoka ndani ya Hospitali ya wilaya ya Ludewa, zinasema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha makubwa katika sehemu za paja la mguu wake wa kulia likiwa limeliwa na kuondolewa nyama pamoja na nyama za kwenye makalio.
Mmiliki wa Mbwa atoa Vitisho
Habari za kuaminika kutoka mkoani humo zinadai kuwa mmiliki wa Mbwa waliouwawa ametishia kuidhuru familia ya marehemu baada ya kusababisha Mbwa wake kuuwawa na Polisi ambao waliwapiga risasi kutokana na agizo la Jeshi la polisi wilayani humo.
Diwani wa kata ya Ludewa, Monica Mchilo (CCM), amesema yeye binafsi ametishiwa na mmiliki wa Mbwa hao tangu kuripotiwa kwa tukio hilo kwa kupigiwa simu na mmiliki wa mbwa hao kuwa “Umewaruhusu wananchi wafanye maamuzi ya kuua Mbwa wangu lakini tutakutana tu mimi sio wa aina yako”.
Moto
Wananchi wakichoma moto Mbwa hao baada ya kuuwawa kwa kupigwa risasi na Jeshi la Polisi
 Hata hivyo, amesema licha ya kuwataka wananchi kuwa watulivu wakati sheria inachukua mkondo wake vitisho ambavyo amevipokea kutoka kwa mmiliki huyo na malalamiko ya wananchi juu ya usalama wa maisha yao vimetowesha hali ya amani katika eneo hilo.
“Tumeitisha mkutano na wananchi wamesema hawataki kuishi pamoja na huyo mmiliki wa hao Mbwa kutokana na mwendendo wake anavyoenenda licha ya kuwa ni mzawa wa eneo hili ila hitimisho litapatikana kwenye kikao kijacho ambacho hatujajua kuwa tutakifanya lini”.
Kamanda wa polisi mkoani Njombe, Fulgensi Ngonyani, amesema usalama wa wananchi hao uko salama na kuwa Jeshi hilo limejipanga kukabiliana na vitisho hivyo kwani  Jeshi hilo limeanza utaratibu wa kumhoji mmiliki wa Mbwa hao.
Afisa Mganga wa wilaya hiyo, Simoni Haule, amekaririwa na FikraPevu akisema Mbwa hao walikuwa hawajapata chanjo ya kuzuia ugonjwa wa kichaa cha mbwa kwa zaidi ya miaka miwili.
FikraPevu  imemtafuta mmiliki wa Mbwa hao, Bosco, ambapo hakupatikana mara moja ili kuzungumzia suala hilo baada ya simu yake ya mkononi kuita bila kupokelewa.
Imeelezwa kuwa Mbwa hao hufungiwa kwenye banda maalamu na mmiliki huyo na hupewa nyama mbichi kwa kurushiwa na wahudumu, na kuwa siku ya tukio walifunguliwa na kuanza kuzunguka katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kujitafutia chakula wenyewe baada ya kukosa kwa muda mrefu bila kupatiwa chakula.
Akizungumza kwa niaba ya familia Baba Mzazi wa marehemu, Faraja Chipungahelo, amesema amepokea simu zenye vitisho kutoka kwa mmiliki huyo na kuwa tayari ameripoti Polisi na kuahidiwa kuwa suala hilo linashughulikiwa.
“Nimetoa taarifa polisi lakini kuna mambo mengi ambayo huyu bwana amekuwa akiyafanya hata kabla ya hili tukio na ukienda pale Polisi hawamfanyi kitu lakini sisi tunasimama na Mungu atatutetea katika hili”
Upande mwingine hofu imetanda Urambo tokana na mbwa wenye kichaa 
KUNDI la Mbwa wenye Kichaa limezuka katika Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, na kuifanya wilaya hiyo kufanya msako wa kuua Mbwa wanaozagaa mtaani ili kudhibiti ugonjwa huo kufuatia mtu mmoja kung’atwa na kufa kwa ugonjwa huo na kusababisha hali ya taharuki kwa baadhi ya wakazi wake.
Afisa Mifugo wa Halmashauri hiyo, Dkt. Liobu Boya, amesema Mbwa hao wanawapa ugumu wa kuwawinda kwa kuwa baadhi ya watu huwafungia ndani pindi wanaposikia msako uko mitaani mara kwa mara.
Amesema hadi sasa wamewauwa mbwa wapatao ishirini (20), na kuwa wameamua kufanya msako wa kuwaua mbwa hao kwa siku nne mfululizo, ambapo kwa siku ya jana na leo wamesema hawajafanikiwa kuona mbwa wengine wanaozagaa mtaani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Adam Malukwi, amesema ni lazima zoezi la kuwaua mbwa hao liendelee ili kuwadhibiti mbwa wote wanaozurura sanjari ambao wanasababisha madhara kwa binadamu na mifugo kuwangata na kufa kwa kuambukizwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa.
Akizungumza na blog hii  mmoja wa watu waliojeruhiwa kwa kung’atwa na Mbwa hao, Yona Elisante, amesema kuwa Mbwa hao wamekuwa wakiwang’ata watu wazima na watoto hivyo kupelekea kutibiwa kwa gharama kubwa na wakati mwingine hushindwa kupata fedha za matibabu.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi mkoani Tabora wameitaka serikali kuharakisha zoezi la utoaji chanjo kwa mbwa hao ili kupunguza tatizo hilo na kama ikishindikana wananchi wapewe ruhusa ya kuwaua kwa njia mbalimbali zinatazo wezesha kuondoa tatizo hilo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwanzugi katika Wilaya ya Igunga, Samweli Hashimu, amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusema kuwa mpaka sasa watu watatu katika kijiji hicho wamejeruhiwa kwa kung’atwa na mbwa hao huku akisema wanaendelea kuwa kutishio kwenye mtaa huo na viunga vyake.
Katika kipindi cha hivi karibuni baadhi ya matukio ya watu kung’atwa na Mbwa katika maeneo mbalimbali nchini yaliripotiwa katika kipindi hicho ambapo tafiti zilionyesha kuwa ugonjwa huo unaongoza kwa kuua watu wengi duniani licha ya jitihada zinazofanywa na Serikali kwa kutoa chanjo ya kuchanja mbwa hao bure katika maeneo mbalimbali nchini.
chanzo FIKRA PEVU

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top