Meneja
wa Benki CRDB Tawi la Babati Mkoani Manyara, Ronald
Paul akizungumza na waandishi wa habari ambapo kwa mara ya kwanza Tawi
hilo lilianza kutoa huduma ya fedha kwa wateja wake jana na linatarajia
kuzinduliwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda au Rais Jakaya Kikwete.
Mkuu
wa Mkoa wa Manyara, Elaston Mbwilo akiwa na wadau mbalimbali wa mkoa
huo, wakiwa kwenye Tawi la Babati la Benki ya CRDB ambalo
jana lilianza kutoa huduma ya fedha kwa wateja wake, wa pili kulia ni
Mkuu wa Wilaya ya Babati Khalid Mandia, akifuatiwa na Katibu wa CCM Mkoa
wa Manyara, Ndeng'aso Ndekubali na kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa
huo, Omary Chambo na Meneja wa Benk ya CRDB Kanda ya kaskazini Chiku
Issa.
kikazi zaidi dada yetu Jamila omary ndani ya uzinduzi wa tawi
Wananchi wa Mkoa wa Manyara,
wametakiwa kutumia fursa ya kuwepo kwa huduma ya benki ya CRDB Tawi la Babati, kwa
kujiwekea akiba na kuchukua mikopo kwa lengo la kujinufaisha kiuchumi na kuongeza
pato la Taifa.
Mkuu wa mkoa wa Manyara, Elaston Mbwilo
aliyasema hayo wakati wa zoezi la benki ya CRDB tawi la Babati, lilipoanza
kutoa huduma ya fedha kwa wateja wake na yeye kuwa mtu wa kwanza kuweka fedha
kwenye tawi hilo.
Mbwilo aliwataka wananchi wa mkoa huo
kufungua akaunti za fedha kwenye benki tofauti ikiwemo CRDB, NMB, NBC, Posta na
Exim, ambazo zipo mjini Babati, kuliko kuweka kwenye benki moja na kuitegemea
yenyewe pekee.
“Waswahili wanasema usiweke mayai yote
kwenye kapu moja, hivyo tutumie fursa hii kwa kuweka akiba katika benki tofauti
tofauti, hapa unaweka sh200, kule sh300, pengine sh100 ndiyo nidhamu ya fedha
ilivyo,” alisema Mbwilo.
Hata hivyo, alisema Waziri Mkuu Mizengo
Pinda au Rais Jakaya Kikwete mmoja wao ndiye atakayekuja kulizindua rasmi Tawi
hilo na alitoa wito kwa benki hiyo ya CRDB kuanzisha matawi mengine kwenye wilaya
za mkoa wa Manyara.
“Siku za nyuma tulikuwa tunaona gari la
benki linakuwa hapa kwa wiki mara moja ila sasa mmeweza kuweka Tawi hapa Babati,
sambaeni na sehemu nyingine huko wilayani msogeze huduma hizi karibu na jamii,”
alisema Mbwilo.
Naye, Meneja wa CRDB Tawi la Babati Ronald
Paul aliwataka wafanyabiashara, watumishi, wakulima na wafugaji wa mkoa huo kutumia
fursa ya kuwepo kwa benki hiyo kwa ajili ya kupata huduma za kifedha ikiwemo
kuweka akiba.
“Jamii itumie nafasi hii kwa kuweka na
kutoa fedha na pia hapa Babati ni kwenye barabara kuu hata viongozi wengi wanapita
kuelekea Dodoma, hivyo watatumia fursa hii ya kuwepo kwa tawi letu kupata
huduma ya fedha,” alisema Paul.
Post a Comment