Dar es Salaam.
Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vimeanza maandalizi ya kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi ya urais, gazeti hili limebaini.
Kadhalika, vyama hivyo ambavyo ni Chadema, NCCR Mageuzi na CUF vinakusudia kuwa na mgombea mmoja wa nafasi za wabunge na madiwani, ikiwa ni hatua ya kuzikabili nguvu za chama tawala, CCM.
Habari zilizolifikia gazeti hili zinasema tayari viongozi wakuu wa vyama hivyo wamekubaliana kuanza mchakato huo na wameandika mapendekezo na kuyapeleka katika sekretarieti za vyama vyao kwa ajili ya kufanyiwa uchambuzi.
Chanzo chetu kilidokeza kuwa kamati ya wataalamu kutoka vyama hivyo tayari imeundwa ili kuandaa taratibu zitakazotumika katika kufanikisha mkakati huo.
Wenyeviti wa vyama hivyo walipoulizwa kwa nyakati tofauti kuhusu mpango huo hawakukubali moja kwa moja, badala yake walisema ni mapema mno kuzungumzia suala hilo katika vyombo vya habari.
Ukawa ni umoja ambao uliviunganisha vyama vyenye malengo yanayofanana katika Bunge Maalumu la Katiba na vimekuwa vikishinikiza kuzingatiwa kwa mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba hususan muundo wa Muungano wenye serikali tatu, tofauti na serikali mbili za sasa.
Umoja huo pia uliwaongoza wajumbe wa Bunge Maalumu ambao ni wanachama wake kutoka nje kususia mchakato wa Katiba Mpya kutokana na kile walichodai kuwa ni kutokuridhishwa na jinsi mambo yanavyokwenda.
Taarifa za kuwapo kwa mpango wa kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu ujao, zimekuja siku chache tangu kufichuliwa kwa mpango mwingine wa kuundwa upya kwa Baraza la Mawaziri kivuli ambalo litawajumuisha wabunge wa vyama hivyo katika Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Baraza la kivuli la sasa linawajumuisha wabunge kutoka Chadema pekee, ambacho kinaunda Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni tangu kuanza kwa Bunge la 10, Novemba 2010.
Mwenyekiti wa Chadema ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema atapanga upya baraza lake katika siku za mwanzo za Bunge la Bajeti, linalotarajiwa kuanza Mei 6, mwaka huu mpango ambao umeungwa mkono na wenyeviti wa CUF na NCCR Mageuzi.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema uamuzi huo ni hatua kubwa katika ushirikiano na kwamba tayari alikwishawaarifu wabunge wa chama chake wawe tayari kushiriki katika baraza hilo.
Wenyeviti wa vyama
Mbowe alisema: “Hivi sasa suala la sisi kuungana kwa maana ya kuwa na nguvu ya pamoja halikwepeki. Siasa ni dynamic (zinabadilika), fikra za jana ni tofauti na fikra za leo kwa hiyo ni ukweli usiopingika kwamba sisi wapinzani tunahitajiana kwa manufaa ya watu wetu na nchi yetu.”
Hata hivyo, alisema ni mapema kuzungumzia uwezekano wa ushirikiano wao katika vyombo vya habari na kwamba wakati ukifika kila kitu kitawekwa wazi.
Kwa upande wake Profesa Lipumba alisema: “Ningefurahi kama tungeweza kufikia kiwango hicho cha ushirikiano maana kama unavyoona hatuwezi kusonga tusiposhikamana na kuwa wamoja, lakini hilo siwezi kulizungumzia kwa sasa maana muda mwafaka bado.”
Aliongeza: “Ni kweli Katiba imetuunganisha na huu ni mwanzo mzuri ambao unaweza kutoa mwanga kwamba huko mbele tutakwenda vipi, tumeona kwamba Serikali haina nia njema kwenye suala hili la Katiba, hivyo tukiendelea kutengana hatutaweza kuukabili udhalimu huu.”
Alipoulizwa wataweza kushirikiana vipi na Chadema hali CUF wakiwa washirika wa CCM katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar, Profesa Lipumba alisema mazingira yaliyowafanya kuingia katika ubia huo yanafahamika kwani ulikuwa ni uamuzi wa Wazanzibari kupitia kura ya maoni.
“Kuwamo katika SUK siyo tatizo kwa sasa, siku zilizopita wenzetu walikuwa hawajatuelewa lakini sasa nadhani tunakubaliana kwamba kuwamo kwenye Serikali huko Visiwani siyo kikwazo tena cha kushirikiana na wenzetu,” alisema.
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia alisema muungano wa vyama hivyo kupitia Ukawa limekuwa darasa kwa viongozi wakuu wa vyama husika kutafakari walikotoka, walipo na wanakokwenda. Hata hivyo, alisema ni mapema sana kuzungumzia suala la kuungana kwao hadharani.
“Tunapata nafasi ya kutafakari na kujifunza kwa kurejea tulikotoka kwa mfano hebu tuifikirie NCCR Mageuzi ya 1995 na ya sasa, CUF ya 2000 na 2005 na CUF ya leo na Chadema ya miaka iliyopita na Chadema ya sasa, haya yote yanatupa fursa ya kutafakari kwa kina tunakotaka kuupeleka upinzani katika nchi yetu,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Kwa hiyo suala la kuungana siyo la kujadili kwa sababu ndiyo mahitaji ya sasa, mjadala pengine ni kwamba tunaungana vipi, katika maeneo gani na kwa madhumuni gani?”Alisema katika siasa, chochote kinaweza kutokea na kwamba mfano mzuri ni Kenya... “Hakuna aliyekuwa akiwaza kwamba leo Rutto (William) angekuwa Makamu wa Kenyatta (Uhuru) kwenye Serikali ya Kenya,” alisema.
Post a Comment