 |
| John Magufuli |
Baadhi ya wanasiasa na wachambuzi wa mambo ya kisiasa wamemkosoa Rais
John Magufuli kwa kutohudhuria mikutano ya Kimataifa ukiwemo mkutano wa
Umoja wa Afrika (AU), uliofanyika Addis Ababa nchini Ethiopia hivi
karibuni wakidai kuwa ulikuwa muhimu sana kidiplomasia.
Wameeleza kuwa mkutano huo wa AU uliofanyika siku mbili nchini Ethiopia
ulikuwa muhimu sana kwa kuzingatia utamaduni wa mikutano hiyo
kuwakaribisha viongozi wapya wa nchi wanachama.
“Kama Mkuu wa nchi, Rais Magufuli alipaswa kuhudhuria mkutano huo ili
akutane na viongozi wenzake na kubadilishana nao mawazo. Nadhani hayuko
sahihi kwenye hili,” Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholas Mgaya aliliambia
gazeti la The Citizen.
“Kwa namna hii, Tanzania inapoteza mengi, taswira yetu inafifia kwenye
ngazi za kimataifa. Kiongozi wetu anapaswa kuona umuhimu wa kuhudhuria
kwenye vikao kama hivyo vya kimataifa vya ngazi za juu,” aliongeza
Mgaya.
Naye mhadhiri Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco) ambaye ni mtaalam wa
masuala ya kisiasa, Profesa Gaudence Mpangala aliunga mkono na kueleza
kuwa mkutano huo ulikuwa na umuhimu sana kwa Rais Magufuli kuhudhuria
akiwa na ujumbe wa viongozi wachache.
“Kama Rais Magufuli amepanga kupunguza gharama, angeenda na watumishi
wachache. Lakini mkutano huo ulikuwa muhimu sana kwake na Taifa,”
alisema Profesa Mpangala.
Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Ikulu, Gerson Msigwa
alieleza kuwa Rais Magufu alimtuma Makamo wa Rais, Bi. Samia Suluhu
kuiwakilisha nchi kwa kuwa alikuwa na majukumu mengine nchini. Kwahiyo
nchi iliwakilishwa vyema kwenye mkutano huo.
“Kama Rais hakuhudhuria ina maana alikuwa na majukumu mengine. Lakini
aliwakilishwa na Makamo wa Rais. Kwahiyo kila kinachohusu Tanzania
kitafanyiwa kazi ipasavyo,” Msigwa aliliambia gazeti la The Citizen.
Aidha alisema kuwa bado kuna mikutano mingi ya Umoja wa Afrika mbeleni ambayo Rais Magufuli atahudhuria.