PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: SERIKALI KUTAIFISHA MALI ZA KAMPUNI YA TANZAM 2000 ZILIZOPO NDANI YA PORI LA AKIBA MOYOWOSI/KIGOSI BAADA YA ILANI YA SIKU 7 - DK. KIGWANGALLA
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akikagua mazingira ya Pori la Akiba Moyowosi/Kigosi alipotembelea pori hilo ju...


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akikagua mazingira ya Pori la Akiba Moyowosi/Kigosi alipotembelea pori hilo juzi katika wilaya ya Bukombe mkoani Geita ambapo amegiza itolewe ilani ya siku 7 kwa kampuni ya Tanzam 2000 iliyokuwa ikifanya utafiti wa madini ya dhahabu ndani ya pori hilo iondoe mali zake zote na endapo itakaidi zitaifishwe kuwa mali ya Serikali. Kushoto kwake ni Meneja wa Pori hilo, Benjamin Kijika na Kaimu Mkurugenzi Mkuu TAWA, Mabula Misungwi.

Na Hamza Temba-Geita
..........................................................
Kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzam 2000 iliyokuwa ikifanya utafiti wa madini ya dhahabu katika eneo la Luahika ndani ya Pori la Akiba Moyowosi/Kigosi imetakiwa kuondoa vifaa na mitambo yake katika eneo la hilo ndani ya siku saba kwa amri ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla.

Dk. Kigwangalla ameiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA kutoa ilani ya siku saba kwa kampuni hiyo iondoe vifaa na mitambo yake katika eneo hilo na endapo muda huo utapita bila kufanya hivyo mali hizo zitataifishwa na kuwa mali ya Serikali kwa kuwa wao ni wavamizi kwa mujibu wa sheria.

Waziri Kigwangalla ametoa agizo hilo juzi alipotembelea pori hilo katika wilaya ya Bukombe mkoani Geita ambapo alihitimisha ziara yake ya siku 25 aliyoipa jina la Pori Kwa Pori kwa ajili ya kukagua shughuli za uhifadhi nchini na kutatua changomoto zake.

Alisema uwepo wa vifaa na mitambo ya muwekezaji huyo ndani ya hifadhi hiyo imekuwa kishawishi kikubwa kwa wachimbaji wadogo wa madini kuvamia maeneo hayo wakiamini kuwa eneo hilo lina dhahabu na kwamba bado linaruhusiwa kwa shughuli za uchimbaji.

Awali Meneja wa Pori hilo, Benjamin Kijika alisema kampuni hiyo ilipewa kibali na Wizara ya Malisili na Utalii kwa ajili ya kufanya utafiti wa madini ya dhahabu katika eneo hilo kwa mwaka 2005 hadi 2010 na kuongezewa muda hadi 2012.

Alisema wakati kibali hicho kinatolewa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 ambayo inazuia tafiti kama hizo na shughuli nyingine za kibinaadamu kwenye maeneo ya hifadhi ilikua bado haijatoka.

Alisema baada ya hapo wizara haikutoa tena kibali kwa kampuni hiyo licha ya wizara ya madini kuipa kibali cha kuchimba dhahabu katika eneo hilo mwaka 2013. Aliongeza kuwa kwa nyakati tofauti Wizara ya Maliasili imeitaka kampuni hiyo iondoe mali zake zote ndani ya eneo hilo, agizo ambalo bado halijatekelezwa mpaka sasa.

Kwa upande wake aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Josephat Paulo Maganga alisema atasimamia utekelezaji agizo hilo la Waziri Kigwangalla ili eneo hilo liendelee kuhifadhiwa kwa mujibu wa sheria.

Alisema hifadhi hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya uvamizi wa mara kwa mara wa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu hususan katika eneo la Kigosi Kaskazini na hivyo kupelekea uharibu mkubwa wa mazingira katika hifadhi hiyo.

Alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo pori hilo limeanzisha kambi mbili za ulinzi katika eneo hilo kwa ajili ya kudhibiti uharibifu huo ambapo mpaka sasa kesi 24 zenye wachimbaji haramu 52 zimeshafikishwa mahakamani huku kukiwa na vielelezo kadhaa ambavyo ni pamoja na baiskeli 102, viroba vya mchanga unaosadikika kuwa na madini ya dhahabu na vifaa vya uchimbaji.

Pori la Akiba Moyowosi/Kigosi ni muunganiko wa mapori mawili yenye ukubwa wa kilometa za mraba 21,060. Pori la Moyowosi lipo katika wilaya za Kibondo na Kakonko (Kigoma) na Pori la Kigosi katika wilaya ya Biharamulo (Kagera), Bukombe na Mbogwe (Geita), Kahama (Shinyanga) na Kaliua (Tabora).

Pori hili lina umuhimu mkubwa kiikolojia na kiuchumi kwakuwa pia ni ardhi oevu ambayo ni chanzo kikubwa cha maji ya ziwa Nyamagoma na Sagara ambayo huingiza maji mto Malagarasi na hatimaye ziwa Tanganyika, maji hayo hutumika kwa matumizi mbalimbali ya majumbani na kilimo. Pia hifadhi hiyo ni  makazi muhimu ya wanyamapori adimu kama Nzohe ambao huliingizia Taifa fedha za kigeni.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akimuagiza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, Mabula Misungwi (Kulia) kutoa ilani ya siku 7 kwa kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzam 2000 ili itoe mali zake zote katika eneo la Pori la Akiba Moyowosi/Kigosi alipotembelea pori hilo juzi katika wilaya ya Bukombe mkoani Geita na endapo muda huo utapita zitaifishwe kuwa mali na Serikali.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akikagua vifaa na mitambo ya kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzam 2000 katika eneo la Luahika ndani ya Pori la Akiba Moyowosi/Kigosi alipotembelea pori hilo juzi katika wilaya ya Bukombe mkoani Geita ambapo amegiza itolewe ilani ya siku 7 kwa kampuni hiyo iondoe mali zake zote na endapo itakaidi zitaifishwe kuwa mali ya Serikali,  Nyuma yake ni Meneja wa Pori hilo, Benjamin Kijika.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akikagua vifaa na mitambo ya kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzam 2000 katika eneo la Luahika ndani ya Pori la Akiba Moyowosi/Kigosi alipotembelea pori hilo juzi katika wilaya ya Bukombe mkoani Geita ambapo amegiza itolewe ilani ya siku 7 kwa kampuni hiyo iondoe mali zake zote na endapo itakaidi zitaifishwe kuwa mali ya Serikali,  Kulia ni Meneja wa Pori hilo, Benjamin Kijika.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akioneshwa vielelezo (mchanga wa madini ya dhahabu na baiskeli) walivyokamatwa navyo wachimbaji wadogo wa madini katika eneo Pori la Akiba Moyowosi/Kigosi na Meneja wa Sekta ya Kigosi Kaskazini, Salum Kulunge alipotembelea pori hilo juzi katika wilaya ya Bukombe mkoani Geita ambapo amegiza itolewe ilani ya siku 7 kwa kampuni ya Tanzam 2000 iliyokuwa ikifanya utafiti wa madini ya dhahabu ndani ya pori hilo iondoe mali zake zote na endapo itakaidi zitaifishwe kuwa mali ya Serikali.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top