Msuva amejiunga na timu hiyo Julai 29, mwaka jana kwa dau la dola 150,000, sawa na zaidi ya Sh milioni 337 akitokea Yanga, lakini sasa ukitaka kumpata, Waarabu wanamthaminisha kwa euro 475,000, sawa na zaidi ya Sh bilioni 1.3.
Mpaka sasa amefanikiwa kufunga mabao sita kwenye ligi ya nchi hiyo huku akifunga mabao manne katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mbali ya mabao hayo, Msuva amefanikiwa kucheza mechi 16 za ligi na moja ikiwa ni ya Ligi ya Mabingwa Afrika hali iliofanya thamani yake kuongezeka.
Kwa mujibu wa mtandao mmoja maarufu nchini Morocco ambao unahusika kutoa taarifa za thamani ya wachezaji, dau la Msuva sasa ni euro 475,000.
Dau hilo ambalo limeonekana kupanda kwa Msuva, pia unaweza kusajili kikosi kizima cha Simba ambacho kilitajwa kuwa na thamani ya Sh bilioni 1.3.
Kuongezeka kwa thamani ya mshambuliaji huyo, kumetokana na kuonyesha uwezo mkubwa kwenye ligi ya Morocco tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Yanga msimu uliopita ambao aliondoka akiwa ni mfungaji bora wa msimu wa 2016/17 kwa kufunga mabao 14 akiwa sawa na mshambuliaji wa Ruvu Shooting, Abdulrahman Mussa.
Mkuu wa msafara wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 20 ya Morocco, Mohammed Raiza, amelimbia Championi Jumatatu kuwa, kwa upande wake anaamini mshambuliaji huyo bado ana nafasi kubwa ya kuweza kufika mbali kutokana na uwezo mkubwa anaouonyesha kwenye ligi ya nchi hiyo.
“Tunamfahamu huyo mchezaji, ni mzuri katika soka la kulipwa kwa sababu amekuwa akijituma na kuitangaza nchi vizuri, nadhani amekuwa balozi bora kwa Tanzania kutokana na kile ambacho amekuwa akifanya na klabu yake, naamini kama ataendelea hivi atafika mbali.
“Lakini tunapokuwa katika suala la soka ngazi ya taifa kidogo inakuwa tofauti hata kiuchezaji kwa sababu makali ambayo anayaonyesha katika timu yake inakuwa ni tofauti na anapokuwa katika timu ya taifa na jambo zuri kwake licha ya kwamba Tanzania tunaifahamu siku nyingi katika soka,” alisema Raiza.
Post a Comment