Mkurugenzi huyo atakayekuwa ameiongoza CRDB kwa miaka 21 atakapostaafu, amesema uamuzi huo anaufanya kupisha damu mpya kuendeleza mafanikio ya benki hiyo kubwa nchini.
“Si vizuri kung’ang’ania madaraka. Tunao wakurugenzi tuliowaandaa kwa muda mrefu ambao wanaweza kuendeleza nitakapoishia. Ninapisha damu changa nami nitaendelea kuwa mwanahisa wa kawaida,” amesema Dk Kimei leo Alhamisi Desemba 28,2017.
Kwa utaratibu wa benki hiyo, mchakato wa kumpata mkurugenzi mtendaji huchukua miezi 18 lakini Dk Kimei ameongeza mwezi mmoja na kuifanya 19 ili kuipa bodi ya wakurugenzi nafasi zaidi ya kukamilisha hatua hizo.
Amesema ingawa upo mfumo mzuri wa kurithishana madaraka ndani ya benki hiyo, lakini mwenyekiti na bodi wana uhuru wa kumchagua mtu mwenye sifa za ziada kutoka nje na kushirikiana na familia ya benki kuendeleza mafanikio.
“Katiba yetu inataka Mtanzania ndiye aiongoze CRDB. Ninaiamini timu niliyoshirikiana nayo tangu niingie hapa. Hata benki nyingine zinazotafuta wakurugenzi watendaji, ningezishauri zije CRDB,” amesema.
Ndani ya muda uliobaki kabla mkurugenzi mpya hajakaribishwa, Dk Kimei amesema angependa kuona inapata faida kama ya mwaka 2015 ilipotengeneza Sh187 bilioni ikiongezeka kutoka Sh148 mwaka 2014.
Post a Comment