Kiongozi
wa msafara wa wawakilishi wa kampuni ya Henan Juren Crane Group kutoka
Jimbo la Henan nchini China, Wang Yuheng (wa pili kulia) akisisitiza
jambo wakati alipokutana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa
Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), Bw. Henry Mwatwinza
Mwimbe (kulia). Tukio hili lilifanyika jana, Alhamisi, Novemba 16, 2017
jijini Dar es Salaam.
Na Daniel Mbega
WANANCHI
wa mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga na Simiyu wanaweza
kujikwamua kiuchumi kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji ifikapo mwaka
2019 kutokana na kuwepo kwa mpango wa uwekezaji unaolenga kuchimbia
visima virefu pamoja na mabwawa katika maeneo mbalimbali nchini
Tanzania.
Kaimu
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika
Tanzania (TFC Ltd), Bw. Henry Mwantwinza Mwimbe, amesema hayo jana
baada ya kukutana na wawakilishi wa kampuni ya Henan Juren Group ya
China, ambayo imeonyesha nia ya kuwekeza kwa ubia nchini kwa
kutengeneza zana mbalimbali za kilimo ikiwa ni pamoja na kuchimba visima
katika maeneo yaliyo kame.
Lengo
la uwekezaji huo, kwa mujibu wa Mwimbe, ni kuwakwamua wakulima kiuchumi
kwa kuwa na kilimo endelevu cha umwagiliaji badala ya kutegemea mvua,
ambazo zimekuwa hazina uhakika kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi
yanayotokana na uharibifu wa mazingira.
“Wanachama
wetu karibu asilimia 80 wanajihusisha na kilimo, hivyo tunaona itakuwa
ni vyema kama tutabadilisha namna ya uendeshaji wa kilimo hiki ili
kilete tija kwao na kwa taifa kwa ujumla.
“Katika
maeneo mengi mvua zinanyesha mara moja kwa mwaka na wakati mwingine
siyo za kutosha, matokeo yake wananchi wanashindwa hata kupata mavuno
yanayojidhi matumizi ya nyumbani, achilia mbali ziada ya kuuza sokoni,
lakini kilimo cha umwagiliaji kina uhakika na kinaweza kuendeshwa wakati
wote wa mwaka,” alieleza Mwimbe.
Alisema
kwamba bado wapo katika hatua za awali kuhusu mchakato huo na
akafafanua kwamba, mradi huo utawahusisha wanachama wote nchini walio
kwenye ushirika ambao watashirikishwa.
Hata
hivyo, alisema mradi mama ni kuunganisha (assembling) zana za kilimo
kutoka China kama matrekta na mashine nyingine zinazoendana na kilimo
watakazoziuza kwa wakulima wa ndani pamoja na nchi jirani, lakini
wanaona kwamba hilo litafanikiwa ikiwa wakulima watajengewa uwezo hasa
kwa kuwa na uhakika wa maji ili kuendesha kilimo cha umwagiliaji.
Mkalimani,
Dkt. Chikira Ismail Msangi, akifasili kuhusu azma ya wawekezaji hao
katika kuanzisha kampuni ya ubia itakayounganisha zana za kilimo kama
matrekta na mitambo ya uchimbaji visima na umwagiliaji hapa nchini.
Kulia ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa Shirikisho la Vyama vya
Ushirika Tanzania (TFC), Bw. Henry Mwimbe. Tukio hili lilifanyika jana,
Alhamisi, Novemba 16, 2017 jijini Dar es Salaam.
“Vijijini
watu wana matrekta lakini yanatumika mara moja tu kwa mwaka kwa sababu
ya kutegemea mvua, kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji ni wazi kwamba
wakulima watahitaji nyenzo zaidi ili kurahisisha kilimo chao, lakini
lazima kwanza maji yapatikane.
“Israel
ni nchi ya jangwa, lakini leo ukienda imebadilika kutokana na kuwepo
kwa visima vilivyochimbwa pamoja na mabwawa na wanalima mazao mengi
yenye ubora na kuyasafirisha duniani kote, sisi Tanzania tunayo ardhi ya
kutosha ambayo tunashindwa kuitumia kwa kuwa tu mahali pengi hakuna
vyanzo vya uhakika vya maji.
“Shinyanga,
Simiyu, Tabora, Singida, Dodoma na Manyara ni mikoa ambayo ina shida
kubwa ya maji japo ina ardhi kubwa, lakini kama watachimbiwa visima
wanaweza kufanya kilimo kwa uhakika na kuwavutia hata vijana
wanaokimbilia mijini kutafuta ajira,” alisema.
Mwimbe
alisema kwamba, katika maeneo ambayo yana mito na vijito kama ya mikoa
ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Rukwa, Katavi na mingineyo, wanaweza
kuchimbiwa mabwawa makubwa ya kuvuna maji ya mvua ambayo yatatumika
kwenye kilimo cha umwagiliaji wakati wa kiangazi.
Wachina wako tayari
Hii ni mitambo itakayounganishwa hapa nchini ambayo ni maalum kwa shughuli za ujenzi na uchimbaji wa mabwawa ya maji.
Bw.
Henry Mwimbe (kulia) Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC
akionyesha kufurahishwa na picha za mitambo ya uchimbaji mabwawa. Tukio
hili lilifanyika jana, Alhamisi, Novemba 16, 2017 jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi
wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC, Bw. Henry Mwimbe (kulia), alitazama
zana na mitambo mbalimbali ambayo itaunganishwa hapa nchini katika
uwekezaji wa pamoja baina ya TFC na kampuni ya Henan Juren Cranes Group
kutoka China. Tukio hili lilifanyika jana, Alhamisi, Novemba 16, 2017
jijini Dar es Salaam.
Uchunguzi wa MaendeleoVijijini unaonyesh a
kwamba, wawekezaji hao kutoka China wako tayari kwa mradi huo na kwamba
wanaweza kukaa chini na TFC kuangalia namna gani utakavyoendeshwa.
Mmoja
wa wawakilishi hao, Wang Yuheng, alisema lengo kubwa ni kuleta
teknolojia ya wakulima wa chini ili kuinua kilimo chao kilete tija na
ikiwezekana wazalishe bidhaa wanazoweza kuzisafirisha nje ya nchi.
“Tunataka
kuja kuwaletea teknolojia wakulima wa hali ya chini, tunajua zana za
kilimo zinaweza kurahisisha kilimo chao, lakini tutazungumza na TFC ili
kuona vipaumbele vyao vingine katika kilimo ni nini, mbali ya
upatikanaji wa maji,” alisema Wang.
Wang
alisema kwamba, zana zote hizo zitakuja kuunganishwa hapa hapa Tanzania
badala ya kuziingiza zikiwa tayari, hali ambayo itasaidia pia taifa
kuingiza fedha za kigeni pamoja na kutoa ajira kwa vijana wa Tanzania
pamoja na kujifunza ujuzi mbalimbali.
Maofisa
wengine walioongozana na Wang ni Si Yongbin, Si Guanlei na Zhai Qinwu
ambao kila mmoja ni mtaalam wa teknolojia mbalimbali.
Watembelea EPZA
Wawakilishi hao wa kampuni ya Henan Juren Group,
jana walitembelea Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji (EPZA) jijini
Dar es Salaam ambapo walionyesha kuridhishwa kwa kiwango kikubwa na
maelezo waliyopewa kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo nchini.
Mkuu
wa Mawasiliano ya Umma wa EPZA, Nyanda Shuli, aliwatoa mashaka kwamba
hakuna urasimu wowote kwa wawekezaji, wawe wa ndani au wa nje, na
kuwahakikishia kwamba mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania ni rafiki.
“Tunayo
maeneo mengi ya uwekezaji hapa nchini na kilimo kinapewa kipaumbele
kikubwa kwa sababu ndicho kinachozalisha malighafi za viwanda, ardhi
inayofaa kwa kilimo imetumika kwa asilimia 35 tu, hivyo bado kama taifa
tunahitaji kuwekeza zaidi ili tuzalishe bidhaa za kuuza nje,” alisema
Nyanda.
Mkurugenzi
wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC, Henry Mwimbe (wa pili kushoto)
akijadiliana jambo na baadhi ya wadau katika makao makuu ya Mamlaka ya
Maeneo Maalum ya Uwekezaji Tanzania (EPZA) jijini Dar es Salaam jana,
Alhamisi, Novemba 16, 2017.
Bw.
Nyanda Shuli (wa pili kulia mwenye miwani), Mkuu wa Mawasiliano ya Umma
wa Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji Tanzania (EPZA), akifafanua
jambo kwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC, Bw. Henry Mwimbe
(wa tatu kushoto) pamoja na ujumbe wa kampuni ya Henan Juren Cranes
Group kutoka China walipotembelea makao makuu ya EPZA jana Alhamisi,
Novemba 16, 2017.
Bw. Nyanda Shuli akifafanua jambo katika mkutano huo.
Mkurugenzi
wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC, Bw. Henry Mwimbe (kulia) na ujumbe wa
wawekezaji kutoka China wakimsikiliza kwa makini Bw. Nyanda Shuli wa
EPZA (hayupo pichani).
Ofisa
Mwandamizi wa Promosheni wa EPZA, Bi. Nakadongo Fares (kulia)
akisisitiza jambo kwa ujumbe wa wawekezaji kutoka China na viongozi wa
Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) wakati walipotembelea
makao makuu ya EPZA, Ubungo External, jijini Dar es Salaam, jana
Alhamisi, Novemba 16, 2017.
Nyanda
aliongeza kwamba, kuna maeneo ya kutosha kwa uwekezaji huko Bagamoyo
ambayo yako chini ya EPZA hasa kutokana na ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo
itakayokuwa mkombozi kwa Watanzania kiuchumi.
“Pale
zitakuja meli kubwa na mizigo, lakini tunataka zikipakua mizigo hiyo
ziondoke na mizigo mingine kutoka hapa, kama Watanzania watakuwa
wamezalisha bidhaa hata zitokanazo na mazao ya kilimo itakuwa fursa
kubwa kupeleka nje,” alisema.
Kwa
upande wake, Ofisa Mkuu wa Promosheni, Bi. Nakadongo Fares, alisema
kuna unafuu mkubwa kwa wawekezaji kutoka nje wanaopitia EPZA kuliko kama
wakija wenyewe moja kwa moja, kwani mamlaka hiyo inayo maeneo tayari
yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji wa kila aina.
“Uunganishaji
wa matrekta unafanyika hapa pamoja na viwanda vya kuongeza thamani ya
mazao ambayo yanasafirishwa nje kwa ubora wa hali ya juu, tunashauri
hata mitambo na zana zenu mje mziunganishie hapa hapa ili kutoa na ujuzi
kwa Watanzania,” alisema Bi. Fares.
Kuhusu Henan Juren Group
Kampuni ya Henan Juren Crane Group ipo
katika Mtaa wa Weizhuang Industrial Park, katika kitongoji cha
Changyuan, jijini Xinxiang katika Jimbo la Henan katika Bara China, na
inaongozwa na Bw. Jason Zhang.
Kampuni
hiyo, ambayo awali ilijulikana kama Henan Juren Crane Co., Ltd,
ilianzishwa mwaka 1987 ikijihusisha zaidi na utengenezaji wa crane,
lakini sasa inazo kampuni tanzu kama Henan Juren Crane Services Co.,
Ltd., Henan Juren Advertisement Co., Ltd. na Hexin Machinery &
Electronic Co., Ltd ambayo inajihusisha zaidi na utengenezaji na zana
mbalimbali zikiwemo za kilimo na umeme.
Kampuni
hiyo ina mtaji wa Yuan za Kichina RMB120,000,000 (takriban Dola za
Kimarekani 18,108,561.60), na rasilimali zenye thamani ya Yuan
200,000,000 (sawa na Dola 30,180,936.00) ambapo inazo karakana tatu
katika wilaya ya kusini, wilaya ya kaskazini na wilaya mpya huku
ikimiliki eneo lenye ukubwa wa meta za mraba 460,000 na wafanyakazi
zaidi ya 1,200.
Kwa mujibu wa rekodi za mwaka 2001, uchunguzi unaonyesha kwamba, mapato yalikuwa kati ya Dola 2.5 milioni na Dola 5 milioni.
Hizi ni crane na madaraja maalum yanayoundwa na kampuni ya Henan Juren Cranes Group inayotaka kuwekeza nchini.
Makao makuu ya kampuni ya Henan Juren Cranes Group katika Jiji la Xinxiang katika Jimbo la Henan nchini China.
Imeandaliwa na www.maendeleovijijini. blogspot.com. +255 656 331974.
Post a Comment