Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula
amesema bomoabomoa inayoendelea katika baadhi ya maeneo nchini inatokana
na ujenzi holela na kutofuata ramani za mipango miji.
Mabula amesema sababu hizo ndizo zinawasababishia hasara wananchi ya kuvunjiwa makazi.
“Watu wengi wamejenga katika maeneo yasiyo rasmi hasa mjini,” alisema na kuongeza:
“Jambo hili linachangia vilio kwa kiasi kikubwa hasa unapofika wakati wa kuweka miundombinu ya maeneo husika.”
Naibu waziri huyo alisema hivyo akimaanisha vilio vinavyotokana na watu kubomolewa makazi yao.
“Wakati huo wahusika kama Dawasco (Shirika la Majisafi na Maji taka Dar
es Salaam) au Tanroads (Wakala wa Barabara)hujikuta wanalazimika kuvunja
baadhi ya nyumba zilizopo katika maeneo yao ili waweze kufanya kazi
iliyokusudiwa,” aliongeza Mabula.
Sababu hizo za bomoabomoa alizitoa jana wakati wa maadhimisho ya siku ya makazi duniani iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Tayari baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam waliojenga pembezoni mwa
Barabara ya Morogoro wamepoteza makazi yao baada ya Tanroads kubomoa
nyumba ili kupisha mradi wa barabara ya kisasa ya njia sita.
Katika hotuba yake, naibu waziri huyo aliwaonya watu wanaoendelea
kujenga kiholela katika maeneo yaliyopangwa akisema urasimishaji
unaoendelea nchini hauwatagusa wale ambao tayari maeneo yao yana mipango
kabambe.
Alisema kuwa urasimishaji huo usiwe chachu ya watu kuendelea kujenga holela kwa kufikiri wizara itarasimisha makazi yao.
Pia, alisisitiza kwamba hawatarasimisha maeneo ambayo tayari yana mpango
kabambe wa uendelezaji mji (master plan), hivyo watakaojenga bila
kufuata utaratibu na bomoabomoa ikiwakuta hawatahangaika nao.
Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Ujenzi wa Nyumba Mwenge, Hilary
Mdaki alisema mbali na kuzingatia ujenzi wa nyumba katika maeneo yaliyo
ndani ya mipango miji, changamoto mbalimbali zimekuwa zikiwakwamisha
katika kufikia malengo yao ikiwamo ugumu wa upatikanaji wa ardhi.
About Author
Journalist , Enterpreneur, Lecturer and Blogger. Email :ngoboleaa@gmail.com.
Advertisement
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment