Kituo cha Sheria
na Haki za Binadamu kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la IDLO kimezindua
mradi wa Kuwajengea Uwezo wa Kisheria Wasichana na Wanawake Wadogo mkoani
Shinyanga ili Kuweza Kuiwajibisha Jamii Kutoa Huduma Bora za Afya ya UKIMWI.
Katika uzinduzi wa
mradi huo uliofanyika Septemba 14 katika manispaa ya Shinyanga na Septemba 15 katika
Halmashauri ya Mji wa Kahama, makundi lengwa ya mradi huo ikiwemo wasichana na
wanawake wadogo, wazazi, viongozi wa serikali na Jamii kwa ujumla yameonyesha
kuvutiwa na malengo na matokeo tarajiwa ya mradi huo.
Akizungumza kwa
niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga wakati wa kuzindua mradi huo Afisa Tawala wilaya
ya Shinyanga Bw. Charles Maugila amesema ujio wa mradi huo katika Manispaa ya
Shinyanga ni wa kufurahiwa kwani mkoa wa Shinyanga kwa ujumla unakabiliwa na changamoto
kubwa ya kukithiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na maambukizi ya Virusi vya
UKIMWI hususani kwa wasichana na wanawake wadogo. “Kumekuwa na miradi mingi
inayolenga kukabiliana na ukatili wa kijinsia na UKIMWI lakini mradi huu ni wa
kipekee kwa vile unalenga kuwajengea uwezo wa kisheria wasichana na wanawake
wadogo ambao ndio wahanga wakubwa wa ukatili wa kijinsia na maambukizi ya Virusi
vya UKIMWI waweze kuwajibisha jamii kwa
kudai huduma bora za afya ya UKIMWI” Alisema Maugila.
Kwa niaba ya Mkuu
wa Wilaya ya Kahama, Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Bw. Anthony Ndanya ameitaka Jamii ya Kahama
kushiriki kikamilifu na kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huo ili
kuweza kufikia malengo ya mradi huo na kupata matoke tarajiwa.
Akizungumza kwa
niaba ya Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Mkurugenzi wa
Fedha na Utawala, Bw. Ezekiel Massanja alisema “kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za
Binadamu Tanzania 2016, ukatili wa kijinsia ukijumuisha ukatili wa majumbani,
ukatili wa kingono, mimba za utotoni, ndoa za utotoni pamoja na vitendo vingine
vya kikatili kwa watoto na wanawake vimezidi kuongezeka maradufu mbali na
kuwepo kwa sheria zinazolinda kundi hilo. Moja ya matokeo ya changamoto za
ukatili kwa wanawake ni kuambukizwa virusi vya UKIMWI”.
“Sambamba na
ongezeko la vitendo vya kikatili, Jamii inakosa uwezo wa kuwawajibisha
watekelezaji wa vitendo vya kikatili na kushindwa kukabilianan na madhara ya
ukatili wa kijinsia kutokana na ukosefu wa elimu ya sheria na namna ya kudai
upatikanaji wa huduma bora za afya” – Aliongeza Massanja.
Mradi huu ni moja
ya miradi mingi ya Dreams Innovation Challenge inayotekelezwa nchini. Mradi umejikita kuwajengea uwezo wasichana wa
miaka 15 hadi 24 na jamii kwa ujumla juu ya masula ya kisheria, afya na ukatili
wa kijinsia. Mradi unalenga kuwapa uwezo wasichana kuiwajibisha jamii pale haki
zao za msingi zinapokosekana hasa kwenye masuala ya afya ya UKIMWI.
Lengo kuu la mradi
ni kuimarisha uwezo wa jamii kuboresha huduma za afya ya UKIMWI kwa wasichana
na wanawake wadogo kupitia mbinu ya uwezeshaji kisheria na uwajibikaji kijamii.
Mradi unalenga
kufikia jumla ya wasichana 1000 wenye umri kati ya miaka 15 – 24. Wasichana 500
Shinyanga na 500 wilayani Kahama. Wanufaika wengine ni pamoja na wanaume ambao
ni wapenzi wa wasichana hao, wazazi, watoto, vyombo vya sheria, wahudumu afya
pamoja na jamii yote kwa ujumla.
Baadhi
ya wasichana na wanawake wadogo watakaofikiwa na mradi katika picha ya
pamoja wakati wa uzinduzi wilayani Kahama.
Afisa
Tawala wilaya ya Shinyanga Bw. Charles Maugila akikata utepe kuashiria uzinduzi
wa mradi wa Dreams Innovation Challenge wilayani humo.
Post a Comment