BAADA ya vipengele vya hotuba yake kupingwa kwa muda mwingi na kiti kumpa dakika mbili za kumalizia hotuba hiyo jana, Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, alisema wenye hatia ni waoga.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama, jana walitumia muda mwigi kupinga vipengele vya maoni ya upinzani, hivyo kufanya Lissu aongezewe dakika 30.
Hata alipopewa nusu saa ya ziada na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, ili amalizie hotuba yake, AG na Mhagama waliendelea kupinga baadhi ya hoja hizo, hivyo nusu saa hiyo kumalizika Lissu akiwa bado hajasoma sehemu kubwa.
Ndipo Chenge alipompa dakika mbili Lissu kumalizia kusoma hotuba hiyo. Hata hivyo, Lissu baada ya kupokea taarifa hiyo ya Mwenyekiti alisema “wenye hatia siku zote ni waoga” na kuondoka.
Ilikuwa siku ya pili mfululizo kwa msemaji wa upinzani kukatisha uwasilishaji hotuba.
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ally Saleh, juzi alisusa kuendelea kusoma hotuba yake kwa madai kuwa hakuna uhuru wa kujieleza katika chombo hicho cha kutunga sheria.
Saleh alikatiza hotuba hiyo, baada ya kutakiwa kufuta kauli iliyohoji uhalali wa Dk. Ali Mohammed Shein kukalia kiti cha Rais wa Zanzibar.
Hata hivyo, Masaju alisema maneno yaliyotamkwa na Saleh hayako katika uhalisia na kusema Saleh anapaswa kurekebisha kauli yake kwa sababu Rais Dk. Shein alishinda uchaguzi mkuu kihalali.
Kutokana na ushauri wa AG, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, alisema maneno yaliyomo katika hotuba ya upinzani yaliyosomwa na mbunge Saleh ni lazima ayatoe kwa sababu si maneno sahihi na hayako katika uhalisia.
Hoja zilizowafanya AG na Waziri Mhagama kila wakati kuomba taarifa kwa mwenyekiti wa Bunge Chenge jana, zilihusu muda wa Kaimu Jaji mkuu, mchakato wa katiba mpya, ukiukwaji wa haki za binadamu, utekaji nyara na utesaji na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kutotimiza wajibu wake.
KAIMU JAJI MKUU
Akisoma hotuba hiyo, Lissu alisema Mahakama ya Tanzania haina kiongozi wake kamili ambaye ni Jaji Mkuu tangu aliyekuwa Jaji Mkuu, Chande Othman, astaafu Januari Mosi, mwaka huu.
Alisema Rais John Magufuli hajateua Jaji Mkuu kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Othaman na badala yake amemteua Profesa Ibrahim Juma kukaimu.
Alisema Rais Magufuli amevunja katiba ya nchi kwa kushindwa kumteua Jaji Mkuu takriban miezi mitano tangu kustaafu kwa Jaji Mkuu na hiyo ni kwa sababu ibara ya 118 (4) haikutungwa kwa lengo la kumwezesha Rais kuteua Kaimu Jaji Mkuu bila kikomo cha muda.
“Ibara ya 118 (4) ya Katiba, Rais anaruhusiwa kuteua Kaimu Jaji Mkuu iwapo itatokea kiti cha Jaji Mkuu kitakuwa wazi, au Jaji Mkuu hayupo Tanzania, au Jaji Mkuu atashindwa kutekeleza kazi yake kwa sababu yoyote na hapo Rais ataona haja ya kumteua Kaimu Jaji Mkuu,” alisema Lissu.
Alisema Kaimu Jaji Mkuu ni nafasi ya muda inayoshikiliwa na mtu mwenye sifa za kuwa Jaji Mkuu kabla nafasi hiyo haijajazwa na Jaji Mkuu kamili.
Alisema Mahakama ya Tanzania ni mhimili mkuu wa tatu wa dola hivyo kutokuwa na kiongozi wake kamili kwa miezi mitano kunatoa taswira potofu kwamba Mahakama ina hadhi hafifu au chini ikilinganishwa na mhimili mingine mikuu ya dola.
Alisema kitendo hicho pia kinatoa taswira potofu kwamba pengine Kaimu Jaji Mkuu wa sasa hatoshelezi nafasi hiyo, au miogoni mwa majaji wote wa rufani au wa Mahakama Kuu ya Tanzania au mawakili na wanasheria wengine wa nchi hakuna hata mmoja mwenye uwezo au sifa za kuwa Jaji Mkuu.
“Kambi ya Upinzani imetaka Waziri amshauri Rais Magufuli amthibitishe Kaimu Jaji Mkuu Profesa Juma kwenye nafasi hiyo au vinginevyo ateue Jaji Mkuu kamili wa Tanzania,” alisema Lissu.
Ndipo AG alipoomba utaribu kwa Mwenyekiti wa Bunge na kusema Katiba ya nchi haijaeleza kikomo cha Rais kuhusu uteuzi wa nafasi ya Jaji Mkuu.
Naye Waziri Mhagama alisimama na kusema hotuba ya Lissu inazungumzia mienendo ya Rais ambayo ni kinyume cha kanuni ya 61 (1).
KATIBA MPYA
Lissu alisema Aprili 30, 2015 Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliwaahidi wananchi kuwa ndiyo ingekuwa siku ya kufanyika kwa kura ya maoni kuhusu katiba iliyopendekezwa.
Alisema baada ya hapo na kwa kipindi kilichobakia cha utawala wa Rais Kikwete, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali waliendelea kusisitiza kwamba kura hiyo ya maoni ingefanyika.
Alisema kura hiyo haikufanyika hadi Rais Kikwete anaondoka madarakani na "ndiyo maana nilisema katika maoni yangu ya mwaka juzi kuwa kwenye 'signature issue' ya utawala wake, yaani katiba mpya, huyu ni Rais aliyeshindwa na ni Serikali iliyoshindwa kutekeleza katiba mpya."
Baada ya kueleza hayo, AG alisimama kuomba utaratibu na kusema: “Hayo maneno anayosema, Serikali haijashindwa, wala Rais hajashindwa, maneno aliyoyaweka yamekaa vibaya, naomba yaondoke kwa sababu yanakiuka kanuni ya 64.”
Mwenyekiti Chenge alisimama na kumtaka Lissu ayaondoe maneno hayo lakini Lissu hakuyaondoa.
HAKI ZA BINADAMU
Lissu alisema Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi anapotosha wananchi anaposema suala la haki za binadamu linazingatiwa nchini.
Alisema badala ya kupungua matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama yameendelea kuongezeka.
Alisema matukio yaliyowahi kutoka miaka ya nyuma ya ukiukwaji wa haki za binadamu hayajatatuliwa wala wahusika kuchukuliwa hatua; akitolea mfano mauaji dhidi ya viongozi wa kidini na waumini sehemu ya ibada yaliyotokea Zanzibar mwaka 2012 na 2013, kutokumatwa aliyehusika na shambulio la bomu katika kanisa la Katoliki Arusha, mauaji ya Daudi Mwangosi na mtu aliyemteka Absalom Kibanda.
Mara baada ya kusema hoja hiyo, Waziri Mhagama alisimama na kuomba utaratibu na kusema masuala hayo anayoyazungumzia Lissu yapo mahakamani na yalishatolewa ufafanuzi bungeni hivyo yanapaswa kuondolewa.
“Lissu pia amezungumzia mambo ambayo yamewagusa watu ambao wanatoa haki ambayo kinyume na kanuni ya 61 (1) (c). Pia nimeipitia hotuba ya upinzani yapo maeneo yanahusiana na mienendo na kesi zilizopo mahakamani ambayo ni kimyume na kanuni ya 61 (c), hivyo naomba Mwenyekiti uyatoe,” alisema Mhagama.
Katika kuitikia hoja hiyo, mwenyekiti Chenge alisema “Lissu nakuomba kuanzia maneno 'signature issue hadi iliposhindwa naomba uyaondoe, kisha ufuate mtiririko mzuri.”.
HAKUPATA MUDA
Japokuwa Lissu hakupata muda wa kusoma sehemu iliyobaki ya hotuba yake, kipengele za utekaji nyara na utesaji kilikuwapo.
Hotuba hiyo inadai sheria za jinai zimesisitiza kuwa utekaji nyara kwa lengo la kuua au kuumiza mtu ni kosa kubwa la jinai.
Aidha, hotuba hiyo inadai mamlaka ya uendeshaji wa mashtaka ya jinai yamekasimiwa kwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka( DPP) kwa mujibu wa ibara ya 59B(2) ya katiba.
Inadai hatua ya DPP kutomchukulia hatua za kijinai Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kitendo cha kijinai cha kuvamia kituo cha Clous Media Group pamoja na kushindwa kumchukulia hatua aliyemtolea bastola aliyekuwa Waziri wa Habari, Nape Nnauye hadharani hiyo inathibitishwa na kushindwa kwake kuchukua hatua za kijinai dhidi ya wale wote waliokula njama za kumfungulia mashtaka ya uongo na kumfunga mbunge Peter Lijualikali.
Hotuba inamtaka Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, kulieleza bunge kama DPP bado anastahili kuendelea kushikilia nafasi hiyo muhimu wakati ameshindwa kutekeleza majukumu yake
Post a Comment