CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM) kupitia chuo chake cha Sayansi za Mawasiliano na Elimu Angavu, kimetengeneza mfumo wenye uwezo wa kuhakiki taarifa na hotuba mbalimbali na kubainisha kama ni halisi au zimechezewa na wahalifu wa kimtandao.
Mkuu wa Kitivo cha Elimu Ang’avu wa chuo hicho, Profesa Leonard Mselle aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano uliowashirikisha wadau wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) juu ya utafiti wa masuala ya usalama wa mtandao uliofanywa na chuo hicho.
Profesa Mselle alisema mwaka 2013, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) walitoa tangazo la kushindana kuandika makala ambazo zitasaidia maendeleo ya ICT na chuo hicho kilishindana na moja ya mada ambazo tulifanyia kazi ni masuala ya usalama wa mitandao.
“Tumeshafanya hiyo kazi na sasa ni mwaka wa tatu lakini mojawapo ya malengo ambayo tulisema tungewekeza katika huu utafiti ni kuweza sisi wenyewe kutengeneza mifumo au mitambo ambayo itahakikisha kwamba kuna usalama wa mitandao,” alisema Profesa Mselle.
Alisema, “suala la usalama wa mitandao ni pana sana, mitambo ambayo unatakiwa kutengeneza ili kuweka usalama nayo ni ya aina nyingi sana… hapa sisi tuna mitambo ambayo inahakikisha uhalali wa taarifa.”
Akitolea mfano, alisema picha au sauti zinazochukuliwa zinaweza kuharibiwa na kupeleka ujumbe ambao ni tofauti kwa kutumia mifumo ya kidijitali hivyo wao wametengeneza mfumo ambao utaonesha kwamba taarifa hiyo, picha au sauti fulani imeharibiwa na siyo halali.
Alisema wanashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Polisi, Majeshi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili kuhakikisha masuala ya matumizi ya mifumo ya kidigitali yapo katika hali ya usalama.
Mapema akifungua mkutano huo, Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) inayochapisha magazeti ya Daily News, Sunday News, Habarileo na SpotiLeo, Dk Jim Yonazi alisema suala la usalama wa mtandao ni jambo muhimu hasa kwa kuzingatia teknolojia inakua kila siku.
Dk Yonazi alisema kama hakutakuwa na usalama juu ya mitandao kuna hatari mbalimbali ambazo zinaweza kujitokeza kutokana na matumizi ya mtandao.
“Usalama wa mitandao ni jambo muhimu la kutiliwa mkazo hasa katika zama hizi za kidigitali kwa kuwa uwepo wa usalama katika matumizi ya mitandao ni sawa sawa na kuhakikishia dunia usalama duniani kote,” alieleza Dk Yonazi.
Katika hatua nyingine, Dk Yonazi alisema kampuni ipo tayari kushirikiana na chuo hicho na kuwapa nafasi maalumu kwa ajili ya kuandika mafundisho na elimu itakayochapwa kwenye magazeti ya kampuni hiyo ili kuelimisha umma usalama wa mitandao.
Post a Comment